Mambo ya kuzingatia wakati ukisherehekea sikukuu ya Eid
- Onyesha furaha kwa wengine hasa wenye uhitaji katika jamii huku ukitenga muda wa kukaa na familia yako.
- Lakini vijana wamekumbushwa kutemba mema ili kudumisha amani na kujiepusha na matendo maovu.
Dar es Salaam. Ni dhahiri kuwa waumini wa dini ya Kiislamu wametimiza nguzo muhimu ya dini yao mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan na sasa wanasherehekea sikukuu ya Eid ul-Fitr.
Eid ul-Fitr ni sikukuu ya kumaliza mfungo na huadhimishwa mwisho wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan. Pia hutumiwa kama siku rasmi ya mapumziko katika mataifa mbalimbali duniani.
Sherehe hizo huanza kwa waumini kukusanyika kwa dua ya kila mwaka ambayo hufanyika muda mfupi baada ya macheo ya asubuhi ambapo hukusanyika katika misikiti na viwanja vya wazi ili kupata mawaidha ya pamoja.
Lakini ni mambo gani waumini wanatakiwa kufanya kipindi hiki cha sikukuu? Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Hamis Mataka anaeleza kwa undani mambo ambayo sheria ya dini imeyaruhusu na iliyokataza kwa waumini wa Kiislamu.
Sheikh Mataka ameiambia www.nukta.co.tz kuwa sheria za dini hazitakiwi kutekelezwa wakati wa mfungo na sikukuu ya Eid pekee bali katika siku zote za maisha ya muumini wa kweli wa dini hiyo.
Huenda umejipanga kufanya mambo mengi ikiwa ni hatua ya kusheherekea Eid, lakini Sheikh Mataka anakukumbusha kuzingatia mambo haya ili upate thawabu:-
Kupata kipato na chakula cha halali
Anasema sheria za dini zinamtaka kila muumini kujipatia kipato kwa njia za halali na kujiepusha na matendo yote ya rushwa na dhuluma. Sambamba na hilo chakula kinachotumiwa na muumini lazima kiwe halali kama kitabu kitakatifu cha Quran kinavyoelekeza.
“Katika kipindi hiki cha sikukuu, thawabu mojawapo ni kupata kipato cha halali na kula chakula cha halali,” amesema Sheikh Mataka.
Zinazohusiana:
- Mambo ya kufanya wakati wa mapumziko ya mwisho wa mwaka
- Jinsi ya kufanya mitandao ya kijamii isikuharibie mahusiano yako
- Zingatia haya wakati ukifanya manunuzi msimu wa sikukuu
Furahi na wengine
Imekuwa kawaida kwa waumini wa dini ya Kiislamu wakati wa mfungo na sikukuu kuwasaidia wenye uhitaji kama wajane, yatima, maskini na watu wenye kipato kidogo katika jamii.
Sheikh Mataka anawakumbusha Waislamu kuendeleza wema wao kwa kufurahi na wengine kwa vile walivyojaaliwa kuwanavyo maana huko ndiko ziliko thawabu za Mwenyezi Mungu.
Kutulia na kuwa karibu na familia
Katika hatua nyingine, Sheikh Mataka anasema familia ni nguzo muhimu katika jamii na wenye wajibu wa kutunza familia wanapaswa kufanya hivyo kama walivyoamrishwa na sheria za dini.
Lakini kipindi hiki cha sikukuu ya Eid ni muafaka kukaa karibu na wanafamilia ili kufurahi na kuonyesha upendo kwa kushiriki chakula cha pamoja.
“Sheria inaagiza muumini kutunza familia yake na kuipatia mahitaji yote. Hii ni thawabu maana familia ni nguzo muhimu,” amebainisha Sheikh Mataka.
Wakati wa sikukuu ni vema wanafamilia wakajumuika pamoja nyumbani ili kuimarisha upendo na amani. Picha| iStock.
Vijana wajiepushe na vitendo vya uasi
Katika sikukuu mbalimbali, vijana hupenda kutembelea maeneo mbalimbali ya starehe ili kufurahi na wale wawapendao.
Lakini Mataka anawaasa vijana wa dini ya Kiislamu kuzingatia mambo waliyoamriwa katika kitabu kitakatifu ikiwemo kujiepusha na mambo maovu ya uasi na kuitumia sikukuu kwa kufanya mambo mema.
“Wajiepushe na uasherati, ulevi na fujo zinazoweza kuhatarisha amani katika jamii,” amesema Sheikh huyo.