Kwa nini hisa za Yetu Microfinance hazibadiliki DSE baada ya kuwekwa chini ya uangalizi?
- Hisa zake hazijashuka wala kupanda tangu Disemba 12.
- Ni kwa sababu ya kusitishwa kwa shughuli za benki hiyo.
- BoT iliiweka chini ya uangalizi kutokana na upungufu mkubwa wa ukwasi na mtaji.
Dar es Salaam. Iwapo wewe ni miongoni mwa wafuatiliaji wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) utakuwa umebaini kuwa bei ya hisa za benki ya Yetu Microfinance hazijabadilika licha ya kuwekwa chini ya uangalizi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutokana na upungufu mkubwa wa ukwasi na mtaji.
Kwa kawaida, baadhi ya hisa za kampuni zilizoorodheshwa DSE bei zake hupanda au kushuka baada ya kutangazwa jambo linaloweza kuwapa matumaini zaidi wawekezaji au kuwakatisha tamaa. Haikuwa hivyo kwa Yetu Microfinance.
Disemba 12 mwaka huu BoT iilisitisha shughuli za kibenki za taasisi hiyo ya fedha kwa siku 90 na utendaji wa Bodi ya Wakurugenzi na uongozi wake.
“Katika kipindi kisichozidi siku tisini (90) kuanzia siku ya taarifa hii, shughuli za utoaji wa huduma za kibenki za Yetu Microfinance Bank Plc zitasimama ili kuipa nafasi Benki Kuu kutathmini hatua za kuchukua ili kupata ufumbuzi wa suala hili,” alisema Gavana wa BoT, Professa Florens Luoga katika taarifa kwa umma.
Pamoja na changamoto zinazoikabili benki hiyo, hisa zake zimeendelea zimeendelea kuwa katika kiwango kilekile cha tangu BoT itangaze kuiweka chini ya uangalizi mapema wiki iliyopita.
Kwa mujibu wa ripoti ya siku ya DSE ya Disemba 16, 2022, hadi soko linafungwa hisa moja ya Yetu Microfinance ilikuwa inauzwa kwa Sh510 huku bei hiyo ikibaki kama ilivyo tangu benki hiyo ilipowekwa chini ya uangalizi Disemba 12.
Pia katika kipindi hicho, hakukuwa na mauziano yeyote ya hisa katika kipindi cha wiki moja.
DSE katika ripoti hiyo, imeeleza kuwa hadi Ijumaa jioni, mtaji wa Yetu Microfinance katika soko hilo ulikuwa Sh6.18 bilioni na haujashuka wala kupanda tangu Jumatatu.
Soma zaidi:
Nini kinasababisha hali hiyo?
Hata hivyo, hali hiyo si bahati mbaya. Mtaalam wa masuala ya uchumi na fedha, Benard Mumwi ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa benki ikiwekwa chini ya uangalizi wa BoT maana yake shughuli zake zote zinasitishwa ikiwemo uuzaji wa hisa.
“Kampuni ikiwekwa chini ya uangalizi, shughuli zake zinasitishwa ikiwemo hizo za hisa mpaka pale muafaka utakapofikiwa,” amesema Mumwi na kubainisha kuwa ndiyo sababu hisa na mataji wa benki hiyo haujabadilika tangu iwekwe chini ya uangalizi.
Mumwi amesema hatua zilizochukuliwa na BoT kwa Yetu Microfinance ni kuipunguzia mzigo wa madeni benki hiyo na kutoa fursa kwa mtu aliyechaguliwa (kampuni ya bima) kusimamia shughuli ya tathmini ya mali na madeni yaliyopo ili kuwalipa wateja na wanahisa wake waliowekeza.
“Ukiruhusu hisa ziuzwe unaiongezea benki mzigo wa madeni na wakati huo tayari haiwezi tena kulipa hivyo busara ni kusitisha shughuli zake ili wateja wapate fedha walizowekeza,” amesema mtaalam huyo wa kujitegemea.
Amesema huo ni utaratibu wa kawaida kwa BoT ambao umeelezwa na Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 na kanuni zake ambapo huchukuliwa kama benki imepungukiwa mtaji na ukwasi kwa kiasi kikubwa ili kulinda usalama wa sekta ya fedha.
Kusuasua kwa utendaji na uendeshaji wa benki hiyo iliyoanzishwa Disemba 23, 2013 kulijidhihirisha zaidi mwaka jana baada ya kiwango cha hasara kuongezeka mara 21 ndani ya miezi 12.
Yetu Microfinance ilipata hasa ya Sh1.12 bilioni mwaka 2021 kutoka hasara ya Sh54.9 milioni kipindi kama hicho mwaka juzi kwa mujibu wa ripoti ya mwaka ya fedha kwa kipindi kilichoishia Disemba 31, 2021.
Benki Kuu kama mlezi wa benki zote nchini imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuhakikisha kunakuwa na ustahimilivu wa sekta ya fedha ikiwemo kushauri benki kuungana ili kupunguza matatizo ya kifedha na wakati mwingine kuziweka chini ya uangalizi zile zenye changamoto ya mtaji.
Mwaka 2017, benki ya kijamii ya Mbinga ilifungwa kutokana na kupungukiwa mtaji na mwaka uliofuata benki nyingine tano (Efatha, Covenant Bank for Women (Tanzania), Njombe Community Bank, Kagera Farmers’ Cooperative Bank na Meru Community Bank) nazo zilifungwa.
Mapema mwaka 2020, BoT iliziunganisha Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB) na Benki ya Posta (TPB) na kuunda Benki ya Biashara Tanzania (TCB).