Wazee, vijana wanavyopiga madili ya kutengeneza majiko Tanzania
- Wanatengeneza majiko yanayotumia mkaa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.
- Bado wanafanyia kazi kwenye mazingira duni ikiwemo pembezoni mwa makaburi.
- Serikali yaahidi kuwaboreshea mazingira ya biashara.
Dar es Salaam. Pembezoni mwa makaburi ya Mwananyamala kwa kopa jijini Dar es Salaam, ndipo utamkuta mzee huyu wa makamo akiendelea na shughuli ya kutengeneza majiko ya mkaa ili kujipatia kipato.
Mzee Ally Migomba maarufu kwa jina la Ally Majiko amefanya kazi hiyo nusu ya maisha yake tangu alipoanza miaka 40 iliyopita.
“Tangu mwaka 1982 nimalize darasa la saba nimekuwa nikifanya kazi hii, nilianzia eneo la mbele kando ya barabara mpaka sasa tumehamishiwa huku pembezoni mwa makaburi,” anasema Mzee Migomba
Mzee huyo aliyefundishwa kazi hiyo na kaka yake anasema kazi hiyo hajawahi kuiacha licha ya kuwa kwa miaka yote hiyo mazingira anayofanyia kazi hiyo ni duni.
Nukta Habari (www.nukta.co.tz) ilimkuta mzee huyo akifanyia kazi zake eneo la wazi karibu kabisa na moja ya kaburi lilipo katika makaburi hayo yaliyopo Kata ya Mwananyamala Wilaya ya Kinondoni.
Hiyo ina maana kuwa wakati wa mvua mzee huyo hulazimika kusitisha shughuli zake kwa sababu hana nyumba ya kufanyia shughuli zake, licha ya kuwa wenzake wenye mabanda ya mabati katika eneo hilo humsaidia kuifadhi vifaa na majiko anayotengeneza kila siku.
Migomba ni miongoni mwa Watanzania wengi waliojiajiri katika shughuli mbalimbali ili kujipatia kipato lakini wanakabiliwa na mazingira yasiyo rafiki ya kuendeshea biashara zao kutokana na ukosefu wa mitaji na teknolojia za kisasa.
Hata hivyo, fundi huyo anayetengeneza majiko yanayotumia nishati ya mkaa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani anasema pamoja na changamoto hizo, kazi hiyo ndiyo imekuwa ikimuingia kipato cha kutunza familia kwa miaka yote hiyo, japokuwa siyo kikubwa.
“Manufaa yangu siyo makubwa, sema mtu ukishazoea kazi umezoea…maisha yanaenda japo siyo kivile, wanangu wamesoma mpaka kidato cha nne,” anasema Migomba.
Kwa siku, hutengeneza majiko sita mpaka 10, na kila jiko huliuza Sh3,000 hadi Sh5,000 ambapo huingiza wastani wa Sh18,000 mpaka Sh40,000 kwa siku.
Abdallah Botea mmoja wa watengeneza majiko katika eneo la Mwananyamala kwa Kopa. Picha| Daudi Mbapani.
Awafungulia fursa vijana
Kwa kipindi chote alichokaa katika eneo hilo la makaburi amekuwa msaada mkubwa katika kurithisha maarifa na ujuzi alionao kwa vijana kutoka maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam.
Shauku yake ni kuona vijana wanapunguza utegemezi na kujiajiri katika utengenezaji wa majiko hayo yanayotumia mkaa kidogo, jambo linalosaidia kupunguza ukataji wa miti, licha ya kuwa baadhi yao siyo waaminifu na humuibia vifaa na majiko yake.
“Wanafunzi naletewa lakini wananiibia, wameniibia vikorokoro vingi kwa hiyo sasa hivi sitaki tena masuala ya kufundisha,” anasema Migomba.
Pembeni anapofanyia kazi Mzee Migomba, yupo kijana mwingine Selemani Salehe ambaye naye anapiga madili ya kutengeneza vifaa hivyo vya kupikia.
Salehe ambaye ameajiri kijana mmoja wa kumsaidia anamiliki banda dogo lilizungushiwa mbao na mabati chakavu huku na anamiliki mashine ya kuchomelea mageti.
Salehe mwenye uzoefu wa takriban miaka 10 ya utengenezaji majiko katika eneo hilo la makaburi anasema awali alikuwa hana muelekeo wa maisha lakini biashara hiyo imempa matumaini mapya.
“Ninaendesha maisha kupitia biashara hii hata nimeweza kununua mashine ya kuchomelea inayoniwezesha kuboresha majiko yangu,” anasema Salehe.
Kwa siku moja, Salehe anaweza kutengeneza majiko hadi 15 ambapo kila jiko huuza kati ya Sh5,000 hadi Sh10,000 kutegemea na ukubwa.
Miongoni mwa wateja wa majiko hayo ni wakina mama ambao huyatumia kwa ajili ya mapishi nyumbani. Wengine ni wafanyabiashara wanaoenda kwake kuchukua majiko na kuyauza sokoni.
Soma zaidi:
- Majiko banifu yatakavyopunguza ukataji wa miti Tanzania
- Teknolojia inavyookoa mazingira
- Elimu, mkaa mbadala kupungua ukataji miti ya asili
Kwa nini wafanye kazi karibu na makaburi?
Mzee Migomba na Salehe wanaeleza kuwa wakati wanaanza biashara walilipenda eneo hilo kwa sababu lilikuwa kando ya barabara na upande wa pili kuna soko hivyo ilikuwa rahisi bidhaa zao kuonekana.
Hata hivyo, eneo lao lilichukuliwa na mwekezaji na kuwalazimu kusogea karibu na makaburi ili kuendelea kuwahudumia wateja wao waliozoea kufika hapo kupata bidhaa hizo.
Wanasema hawana mpango wa kuhama hapo kwa sababu wanaamini ni sehemu sahihi ya kupata kipato labda wapate mtaji utakaowasaidia kuboresha mazingira ya kufanyia kazi.
Kibarua kilicho mbele yao
Suala la usalama wawapo kazini ni moja kati ya changamoto kubwa inayowakabili. Wanatumia bati na vyuma kutengeneza majiko, wanapoumia hawawezi kumudu kupata matibabu hospitalini.
“Ukijikata na bati unajikaza unaweka chumvi kwenye kidonda unajifunga kisha unaendelea kufanya kazi…. siwezi kununua dawa za hospitali labda nikiumia pakubwa,” anasema Salehe.
Abdallah Botea anayefanya kazi pamoja na Salehe anasema uwepo wa makaburi katika eneo hilo wakati mwingine hukwamisha shughuli zao. Watu wanapokuja kuzika ni lazima wapunguze au waache kabisa kugonga vyuma ambavyo ni sehemu ya kazi zao.
“Sisi ni binadamu huwezi kufanya kazi wakiwa wanazika, wakati mwingine tunacha kazi na kwenda kuwasaidia kuzika,” anasema Botea.
Changamoto nyingine kubwa inayowakabili ni kukosekana kwa umoja miongoni mwao licha ya kuwepo pamoja kwa muda mwingi hawawezi kushirikiana kufanya maamuzi ya pamoja kama kuomba mikopo katika taasisi za kifedha kuboresha biashara zao.
Huenda hiyo ndiyo sababu kubwa iliyofanya biashara zao zisikuwe katika kiwango kizuri na kuboresha maisha yao.
Majiko hayo yanayotumia mkaa kidogo hutengenezwa na vijana pembezoni mwa makaburi ya Mwananyamala kwa Kopa jijini Dar es Salaam. Picha| Daudi Mbapani.
Wafanye nini kutoka katika mkwamo huo?
Wanyabiashara hao waliokaa katika eneo hilo kwa zaidi ya miaka 10 bado wana safari ndefu ya kujikwamua kimaisha kwa sababu kipato wanachpata huwasaidia kukidhi mahitaji madogo madogo ya maisha huku wakiwa wameridhika na hali hiyo.
Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu Cha Mtakatifu Agustino Tanzania (SAUT) Damas Mushi anasema kinachofanya wajasiriamali wengi kushindwa kuendelea licha ya kufanya biashara kwa muda mrefu ni mazoea mabaya waliyojiwekea.
“Nadhani kinachowasumbua wengi ni mazoea, wanafanya biashara bila malengo wanashindwa kuweka rekodi ya mapato na matumizi,” anasema Mushi ambaye ni mchambuzi na mshauri wa masuala ya kiuchumi.
Mushi anasema namna bora ya kuendesha biashara na kukuza mtaji ni kukopa na kupanua wigo wa biashara au ujasiriamali anaoufanya.
“Waende kwenye taasisi za kifedha huko watakopeshwa na kupata mtaji utakaowawezesha kuboresha ujasiriamali na biashara zao,” anashauri mtaalam huyo.
Tangazo:

Kwa mujibu wa Mushi, hilo halitawezekana kama hawatakuwa na rekodi nzuri ya mapato na matumizi, kwa sababu hata wakienda benki au kutafuta wawekezaji wataomba rekodi hiyo.
Sambamba na hilo watafute wataalamu wazuri watakaowaelekeza jinsi ya kufanya biashara ilete tija, lakini wajifunze kwa waliofanikiwa.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba katika hotuba ya bajeti kuu ya Serikali ameeleza kuwa Serikali itaendelea na jitihada mbalimbali za kuhakikisha wajasiriamali wadogo wanaboreshewa mazingira ya kufanyia biashara.
“Serikali itaendelea kuwatambua na kuwaunganisha na taasisi za fedha ili waweze kupata mikopo nafuu. Vilevile, Serikali itaendelea kutenga maeneo na ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya wajasiriamali wadogo,”alisema Dk Nchemba Juni 14 wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti hiyo.
Latest