Kutana na mjasiriamali anayewapa furaha wanawake kwa bidhaa za asili-2
- Ni mshauri na mjasiriamali aliejikita kubadili muonekano wa wanawake na wasichana.
- Atoa njia za kuepuka matumizi ya vipodozi vyenye kemikali hatarishi.
Dar es Salaam. Leo tunaendelea na sehemu ya pili ya makala haya kuhusu urembo wa ngozi na vipodozi sahihi kuboresha muonekano wa wanawake.
Tofauti na wauzaji na watengenezaji wengine wa bidhaa za urembo Hellen Hamisi hutoa ushauri wa matumizi sahihi ya bidhaa za urembo hata usiponunua bidhaa kwake.
Kinachosababisha afanye hayo yote ni nia ya dhati ya kubadilisha jamii ya Watanzania kutoka katika matumizi ya vipodozi vyenye kemikali ambavyo vimegharimu muonekano, hata maisha ya watu wengi.
Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) imeyataja matumizi ya kemikali hatarishi zinazopatikana kwenye vipodozi kama mojawapo ya chanzo cha kansa mbalimbali ikiwemo ya ngozi.
Bidhaa nyingi za urembo zilizopo sokoni kwa sasa zina kiwango kikubwa cha kemikali za aina mbalimbali zinazoboresha muonekano lakini kuacha madhara kwa watumiaji.
“Matumizi ya vipodozi vyenye kemikali yana madhara makubwa sana ambayo yanakuja kuonekana baada ya muda mrefu baada ya miaka 10 au 20. Kwa hiyo simshauri kabisa mtu atumie,”anasema Hellen.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) iliyotolewa Februari 3, 2022 kansa ya ngozi ni miongoni mwa aina za kansa zilizojitokeza zaidi kwa mwaka 2020 ambapo visa 1.2 milioni vya kansa ya ngozi vimeripotiwa ndani ya mwaka huo.
Mbali na visa hivyo WHO inasema takribani watu milioni 20 walipoteza maisha kwa aina mbalimbali ya kansa ikiwemo kansa ya ngozi.
Hellen anaeleza madhara mengine ya kutumia vipodozi vyenye kemikali ni pamoja na kupata matatizo ya homoni kwa wanawake, kuzeeka mapema, kuchakaza ngozi na kupata michirizi na makunyanzi.
Vipodozi visipotumika kwa sasa usahihi vinaweza kusababisha madhara kwa ngozi ya binadamu. Piacha | Shutter Stock.
Jinsi ya kuepuka matumizi ya vipodozi vyenye kemikali hatarishi
Baada ya kuona athari za kutumia vipodozi vyenye kemikali najua unajiuliza unawezaje kuepukana na matumizi ya vipodozi hivyo na kuhamia kwenye bidhaa za asili?
Hellen ambaye pia amesomea taaluma ngozi (dermatologist) anasema hatua ya kwanza kabisa ya kuepukana na matumizi ya vipodozi vyenye kemikali ni kujua aina ya kipodozi unachonunua kabla ya kukitumia
Kuna wimbi kubwa la wanawake na wasichana waliojiingiza kwenye masuala ya kujichubua na matumizi ya vipodozi vyenye kemikali vilivyo waharibia ngozi zao kwa sababu tu hawakujua.
Hellen alikuwa mmoja wa wahanga wa jambo hili, ugonjwa wa tetekuwanga aliupata ukubwani ulimuachia madhara makubwa yaliyomfanya atumie kila kipodozi bila kujua madhara yake.
“Hiki ni kitu ambacho mimi nilikikosa mwanzoni ambacho natamani kila mtu ajue aina ya bidhaa na nini inaenda kufanya kwenye mwili wake kabla ya kutumia,” anasema Hellen.
Ukiona uelewa wako ni mdogo kuhusu bidhaa ya urembo unayotaka kutumia, tafuta mtu ambaye ana ufahamu wa aina ya kipodozi au bidhaa unayotaka kununua akushauri.
Mbali na hayo wanawake na wasichana wanaotaka kuepuka madhara ya vipodozi vyenye kemikali ni lazima wazipende ngozi zao asilia na kuwa na uvumilivu wakati wanatumia bidhaa za asili kwani matokeo yake ni ya taratibu ukilinganisha na bidhaa zenye kemikali.
”Miili yetu imeumbwa na seli na matokeo ya taratibu hivyo lazima hata matokeo yawe ya taratibu,” anasema Hellen.
Zinazohusiana
-
Urembo wa kucha unavyowaweka matatani wanawake
-
Kutana na mjasiriamali anayewapa furaha wanawake kwa bidhaa za asili
-
Gharama utakazolipa unapoamua kujichubua ngozi
Changamoto anazozipitia
Waswahili wanasema hakuna mafanikio yasiyo na changamoto, hata kwa mjasiriamali huyu mambo hayakuwa rahisi mpaka kufikia kutengeneza bidhaa 50 kwa siku.
Changamoto kubwa aliyowahi kuipitia ni kuaminika na wateja,ili ufanikiwe kwenye biashara hii ya urembo ni lazima upate watu wanaokuamini.
“Changamoto kubwa niliyokutana nayo ni mtu kuniamini hasa ikiwa zinatengenezwa hapa nchini,” anasema Hellen.
Mbali na changamoto hiyo kwenye kutengeneza bidhaa napo kuna maswaibu yake. Hellen anasema ameshawahi kutengeneza bidhaa na haikuleta mabadiliko yoyote kwa mtumiaji.
Jambo zuri ni kwamba bidhaa hiyo ilikuwa kipindi cha majaribio ilikuwa bado haijaenda kwa wateja hivyo aliweza kutafiti upya na kuitengeneza kwa usahihi.
Upatikanaji wa malighafi za bidhaa za urembo hapa nchini bado ni changamoto si kwa Hellen tu bali kwa wauzaji na watengenezaji wa bidhaa za asili, huwalazimu kutoa pesa zaidi ili kuzipata.
“Kama ni mtu anayeanza biashara kama hii ya kwangu upatikanaji wa malighafi huwa ni changamoto, tunapata malighafi kwa gharama kubwa,” anasema Hellen.
Kwa sasa Hellen hana ofisi maalum anatumia mitandao ya kijamaii kama Instagram na Facebook kujitangaza na kupata wateja kwa njia ya mtandao (Online store).
Changamoto huja pale wateja wanapotaka kuonana nae kwa ajili ya ushauri inabidi awafuate walipo jambo ambalo linakula muda wake na pengine angekuwa na ofisi angeweza kuhudumia wateja wengi zaidi.
Majani ya mti wa mlonge yakisagwa vizuri ni malighafi nzuri ya kutengeneza vipodozi vya asili kwa ajili. Picha| Istock.
Awafunda wasichana
Mwanasayansi huyo aliyepo masomoni kuongeza ujuzi wakutengeneza bidhaa za asili anaumizwa na uweppo wa mabinti wasio na uthubutu wa kujaribu mambo mapya na wanaokata tamaa na kughairi ndoto zao kutokana na changamoto mbalimbali.
Licha ya kushindwa kumalizia shahada yake ya udaktari Hellen hakukata tamaa na aliamua kugeukia tasnia ya urembo ili kujipatia kipato na kuendesha maisha yake.
“Usiogope kuanza upya, wasichana wengi tunaogopa kuanza upya, bila kujua uoga wako ndio umaskini wako. Pale unapoogopa ndiyo unaposhindwa kufanikiwa,” anasema Hellen.
Kuanzisha biashara na kuiingiza sokoni alafu ukakosa wateja au kupata wateja pungufu na mategemeo kunaweza kukatisha tamaa.
Kwa kutambua uwezo wake huo anatamani wasichana wengine wajifunze kwake wasikate tamaa ilimradi wana uhakika na wanachokifanya na wanakipenda.
“Kitu cha kwanza cha kuwashauri wasichana wenzangu ni kutokata tamaa, yaani unapopata changamoto ndiyo mwanzo wa kupiga hatua siyo unapata changamoto ndiyo unalala,” anasema Hellen ambaye pia hufanya huduma ya kusambaza bidhaa maeneo waliyopo wateja wake.