Kutana na mjasiriamali anayewapa furaha wanawake kwa bidhaa za asili
- Ni Hellen Hamisi, mjasiriamali, msomi anayechagiza matumizi ya vipodozi vya asili.
- Hutengeneza bidhaa hizo kwa kutumia malighafi ya asili yanayopatikana hapa nchini.
Dar es Salaam. Ni majira ya saa 10 alfajiri, katika nyumba nyingi jijini Dar es Salaam ukimya umetawala kuwaruhusu wakazi wa jiji hilo kumalizia usingizi wa alfajiri.
Hali ni tofauti kwa Hellen Hamisi ambaye tayari ameamka kuanza kufanya kazi zake ili kujiingizia kipato.
Hellen, mkazi wa Mbezi jijini hapa huamka muda huo kila siku kutengeneza bidhaa za urembo za asili kuwaongezea wanawake wa Tanzania sababu ya kujiamini kwa ngozi zao.
Uwepo wa wanawake wenye changamoto za ngozi jijini hapa ikiwemo chunusi, makovu, vipele, na mabaka usoni na sehemu nyingine mwilini kumemfanya aje na ubunifu wa bidhaa hizo ili kunusuru afya zao.
Hiyo ni baada ya kugundua kuwa baadhi yao hutumia vipodozi vyenye kemikali hatarishi ambazo huaharibu ngozi zao.
Utengenezaji wa bidhaa hizo kwa Hellen ni zaidi ya kazi inayomuingizia kipato bali ni sehemu ya maisha yake ya kufanya kile anachokipenda kuhakikisha wanawake wenzake wanakuwa na mwonekano mzuri.

Skrabu nimoja kati ya bidhaa zinazozalishwa na Hellen Hamis, skrabu hii inasaidia kuondoa seli za ngozi zilizokufa na kuboresha muenekano wa ngozi.Picha|Elle Natural/Instagram.
Upendo wake na kazi hiyo ulianza tangu mwaka 2019 akiwa anasoma shahada ya udaktari na baadaye kuendelea na shahada ya masoko Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).
“Ili kujifunza zaidi niliamua kujiendeleza kwa kujiunga na kozi ya mtandaoni ya masuala ya ngozi (dermatology) inayotolewa na Chuo Kikuu cha Arizona kilichopo nchini Marekani,” anasema Hellen.
Mwaka 2021 alianza rasmi kutengeneza bidhaa za urembo ikiwemo mafuta, skrabu, seramu, tiba ya chunusi na vikinga jua kwa kutumia bidhaa za asili.
Bidhaa hizi huzitengeneza kwa kutumia malighafi ya asili yanayopatikana hapa nchini Tanzania na baadhi kutoka nje ya nchi. Malighafi hizo ni pamoja na mimea ya aloe vera, mwani na mnyonyo na vitunza bidhaa (preservatives).
Kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu aanze kazi hiyo hajawahi kuchoka kuamka alfajiri kutengeneza bidhaa hizo ambapo hutumia takribani saa sita kila siku.
“Kwa siku naweza kutengeneza product (bidhaa) 30 mpaka 50 kutegemea na uhitaji wa bidhaa na kupungua kwa bidhaa kwenye soko,” anasema Hellen.
Zinazohusiana
Changamoto inapoleta fursa
Bidhaa hizo zilikuwa msaada kwake wakati alipopapata changamoto ya ngozi. Ilimlazimu kuvalia njuga suala la utengenezaji wa bidhaa hizo rasmi ili ajitibu lakini pia awasaidie wanawake na wasichana wengine wenye changamoto kama yake.
“Nilijiangalia kwanza mimi kisha nikachukua hatua ya kwenda kusomea ili kuweza kutatua matatizo yote ya ngozi kwa wenye changamoto kama yangu,”anasema Hellen.
Kama ilivyo kwa wasichana na wanawake wengine uwepo wa makovu, chunusi au kukosa muonekano mzuri huwapa msongo wa mawazo. Hellen naye alipata changamoto hizo zilizochangia kuja na biashara ya uuzaji wa bidhaa za asili.
“Kilichonisukuma ni mimi mwenyewe niliumwa tetekuwanga katika umri wa ukubwani nikapata changamoto juu ya mabadiliko ya ngozi yangu hasa kwenye makovu,” anasema Hellen.
Katika hatua za muda mrefu za kutatua changamoto za ngozi alizokutana nazo binti huyo anatamani bidhaa zake zilizomtoa kwenye wimbi la kutokujiamini na kukosa furaha zitumike kutatua matatizo ya ngozi kwa wanawake wengine.

Matumizi ya Serum hung’arisha ngozi iliyofiubaa pia hufifisha madoa yaliyosababishwa na chunusi. Picha|Elle Naturally
Anahakikishaje usalama wa bidhaa zake
Usalama wa bidhaa za urembo ni jambo la misingi ambalo huzingatiwa na kila mtumiaji wa bidhaa hizo. Kushindwa kuzingatia jambo hilo kunaweza kumpotezea wateja na kuleta madhara kwa watumiaji wa bidhaa.
“Yani kabla ya kununua bidhaa lazima nihakikishe usalama wake iwe kwa watu waliowahi kutumia au kwa muuzaji mwenyewe ili niwe na uhakika kwamba sitapata madhara yoyote nikitumia,” anasema Josephine Tairo mkazi wa Kimara.
Kuna kundi kubwa la wanawake kama Josephine ambao wanapata madhara mara baada ya kutumia aina fulani ya vipodozi na kuwaacha kwenye makovu ya kudumu.
Hellen mtengenezaji wa vipodozi vya Elle Natural, usalama ni kitu cha kwanza kukizingatia katika utengenezaji wa bidhaa zake.
“Nina hakikisha usalama wa bidhaa zangu kwa kuzingatia usafi wa mahali ninapotengenezea na vyombo vya kutengenezea.
“Huwa tunaweka preservative (kihifadhi bidhaa) kuwezesha bidhaa kukaa kwa muda mrefu lakini haina madhara kwa binadamu,” anaeleza Hellen.
Hellen hufanya majaribio ya bidhaa kabla ya kuanza kuziuza kwa wateja
Kipindi hiki cha majaribio huchukua miezi mitatu ambapo hukusanya taarifa za matokeo kila wiki kutoka kwa walengwa na akijiridhisha usalama wa watumiaji basi bidhaa huwa tayari kwa ajili ya kwenda sokoni.
Tofauti na wauzaji wengine wa bidhaa za urembo mitaani au mtandaoni ambao hawazingatii suala la usalama, bidhaa za urembo za mwanadada huyu zimesajiliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).
Kusajili biashara ya urembo BRELA au kwenye mashirika mengine ya urasimishaji hapa nchini kama Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kumewezesha bidhaa zake kukubalika na wateja wake.
Mbali na kuongeza uaminifu, BRELA wanasema ukirasimisha biashara unapata faida nyingi ambazo ni pamoja na kupanua wigo wa kufanya biashara kubwa, urahisi wa kuitangaza kampuni na kupanua wigo wa wateja ambazo ni ndoto za kila mfanyabiashara.
Usikose sehemu ya pili ya makala haya ambayo itazungumzia madhara ya kutumia vipodozi vyenye kemikali na namna unavyoweza kufanya kuepukana na matumizi ya vipodozi hivyo.
Latest