Urembo wa kucha unavyowaweka matatani wanawake
- Wapo ambao kucha zimeoza, kupata fangasi, kubanduka na kubadilika rangi.
- Hali hiyo husababishwa na huduma mbovu, bidhaa zisizo na ubora.
- Pia kushindwa kumudu gharama za huduma za kupaka.
Dar es Salaam. Siyo jambo geni kuona vijana wa kiume wakitembea barabarani hasa katika miji mikubwa kama Dar es Salaam wakiwa wamebeba vikapu vyenye nyenzo za urembo wa kucha.
Katika vikapu hivyo wanaweka rangi za kucha za aina mbalimbali, vibao vya kusugulia magaga na taulo zikining’inia mabegani ili kuwahudumiwa wateja wao mitaani.
Kwa vijana hao ni ajira lakini kwa wanawake ni urembo ili kupata muonekano mzuri wa kucha. Kucha hizo za vidoleni na miguuni husafishwa vizuri kwa maji na kisha kupakwa rangi tofauti kulingana na mahitaji ya muhusika.
Licha ya vijana hao kuzunguka mitaani kusaka wateja, wengine wamejiongeza na kuwa na ofisi maalum ambazo hutoa huduma hizo.
Hata hivyo, siku za hivi karibuni kumeibuka mijadala hasa katika mitandao ya kijamii kuhusu athari za kiafya ambazo zinaweza kumpata mtu anayepaka kucha rangi.
Baadhi ya wanawake ambao wamekuwa wakipata huduma hiyo, wameripoti kupata madhara ikiwemo kucha kuoza, kupata fangasi za kucha na wakati mwingine kucha zao kubadilika rangi.
Siyo hayo tu, wengine huenda mbele zaidi na kuvimba vidole ikifuatiwa na majipu yanayotoa usaha na kucha kubanduka.
Madhara hayo yanaweza kuwapata pia wanaobandika kucha bandia kwenye vidole.
Fangasi za kucha husababishwa na kutokubandika kucha kwa usahihi au kukaa na kucha bandia kwa muda mrefu. Picha| Naturopathy.
Hata hivyo, madhara hayo hutofautiana kati ya mtu na mtu kutegemeana muda na kiwango cha rangi alichopaka. Pia aina ya rangi na kukosea masharti ya upakaji kunaweza kuchangia hali hiyo.
“Mara ya kwanza sikujua sababu (nilipopaka rangi), nilishtukia tu kucha zinabanduka zenyewe. Sijajikwarua popote, zinatoka tu bila sababu,” anasema Shinuni Masoud, mkazi wa Mwananyamala mkoani Dar es Salaam ambaye amewahi kupata madhira hayo.
Shinuni anadai kilichosababisha hali hiyo ni aina ya hina (henna) aliyokuwa akitumia ambayo haikua rafiki wa kucha zake.
“Hapo ndipo niliposoma mahali kuwa aina ile ya hina niliyokuwa nikipaka imewafanyia hivyo hivyo na watu wengine, niliacha kupaka na hadi leo, sijabanduka kucha tena na ni zaidi ya mwaka umepita,” anasema Shinuni ambaye ni mwanamuziki.
Kwa warembo wengi bado hawafahamu madhara hayo yanasababishwa na nini. Wanadhani shida hiyo inasababishwa na mzio wa kemikali zilizopo kwenye rangi na kuwashuku watoa huduma kuchanganya kemikali zisizostahili kwenye rangi.
Elizabeth Reginald, mkazi wa Dar es Salaam ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa rangi zimeharibu kucha zake. Siyo yeye tu, hadi mama yake mdogo.
Reginald ambaye amepaka rangi za kucha kwa miaka tisa anasema awali kucha zake zilikuwa nzuri na wala hakuhitaji kupaka rangi wala kubandika kucha bandia.
“Nilikuwa ninaweza kupaka rangi tu na rangi ikaonekana kwenye kucha zote bila shida. Baada ya miaka mingi ya matumizi ya rangi za kucha na kucha bandia, kucha zangu zimeharibika,” anasema Elizabeth ambaye kucha zake zimekuwa ndogo na nyeusi kiasi cha kutokuonekana.
“Ni urembo tu, nilikuwa najaribu,” anasema Elizabeth.
TANGAZO:
Sababu zinazochangia madhara hayo
Siyo watu wote wanaopaka rangi au kubandika kucha bandia wameripoti kupata madhara ya kiafya lakini ni jambo ambalo linatakiwa kuangaliwa kwa ukaribu ili kuwasaidia watu wanaopata huduma hiyo.
Baadhi ya mambo yanayochangia kuharibika kwa kucha ni matumizi ya rangi zisizo na ubora na ambazo hutengenezwa kienyeji bila kuzingatia uwiano mzuri kwa watumiaji.
Hali hii huwakuta zaidi wanawake ambao hawatumii bidhaa ambazo zimethibitishwa ubora wake na kujichukulia rangi za mtaani.
Mkazi mwingine wa mkoani hapa, Noela Alfred, anasema yeye katika kupaka rangi kwake kwa takriban miaka 20, hajawahi kupata changamoto yeyote kwa sababu amechagua kutumia bidhaa bora hata kama anatumia kiasi kikubwa cha fedha kuzipata.
“Mimi ni mpaka rangi mzuri sana, na nina rafiki zangu wengi tu ambao kucha zetu mara nyingi zina rangi lakini hatujawahi kupata shida hiyo,” amesema Noela ambaye hutumia Sh20,000 hadi 30,000 kupata huduma ya kusafisha na kupaka rangi miguu.
Ni muhimu kuzingatia muda ambao rangi inatakiwa kukaa kwenye kucha. wataalamu wanasema, rangi ya “gel” ndio hudumu kwa hadi mwezi mmoja. Picha| Denho Mobile Nail Bar.
Kwa mtoa huduma za rangi za kucha kutoka Kitunda mkoani hapa, Fahad Amiri, kucha kuoza au kubadilika rangi inachochewa na vitu mbalimbali ikiwemo gharama anayolipia mtu kupata huduma.
Amiri amesema, siku zote kizuri kina gharama na hivyo hivyo huduma nzuri pia inahitaji muda na pesa.
“Rangi nzuri ni za jeli (rangi inayodumu muda mrefu kwenye kucha) na zinakaa muda mrefu zaidi. Gharama yake ni Sh30,000 kwa kupaka rangi za mikono na miguu,” anasema Amiri akibainisha kuwa rangi hiyo hupendwa na wengi lakini wengi hushindwa kumudu bei yake.
“Rangi ya jeli ni gharama na inatumia muda mrefu kupaka. Kubandika kucha zake ndio kazi nyingine kabisa,” anasema mtaalam huyo wa kucha mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka mitano.
Pale mteja anapobembeleza kupunguziwa bei, baadhi ya watoa huduma hukubaliana na bei hiyo lakini wanatoa huduma ambayo huwaacha katika madhira yanayowaongezea gharama zaidi za matibabu.
Pia kucha bandia isipobandikwa vizuri kwenye kucha ya asili inaweza kuwa sababu ya mtu kupata madhara ikiwemo kucha kuoza au kubanduka.
“Kubandika kucha inatakiwa ibandikwe mbele kidogo ya ukingo wa kucha. Hiyo huwa inasaidia kucha kupata hewa, na kurefuka bila shida. Hata hivyo hiyo kazi ni ngumu na inahitaji muda mrefu kufanyika.
“Mtu akililia kupunguziwa bei, watu humbandika kucha kuanzia mwanzo wa kucha kwani ni rahisi zaidi na haichukui muda. Kucha inakosa hewa au inashindwa kukua hivyo inaanza kuoza au kubadilika rangi,” anasema Amiri.
Pia ameweka wazi kuwa baadhi ya wasichana wanakaa na kucha kwa muda mrefu kuliko inavyotakiwa na hiyo pia ni changamoto.
Katika makala inayofuata tutaangazia kwa undani dondoo za kutunza kucha, rangi zipi zinafaa na ufanye nini kuepukana na adha ya kucha zako kuharibika.