Kiungulia: Unavyoweza kukiepuka, kujitibu
- Ni pamoja na kuepuka uvutaji wa sigara pamoja na matumizi holela ya dawa.
- Wataalamu wa afya wanashauri kula kwa wakati na kwa mpangilio.
Dar es Salaam. Bila shaka umeshawahi kupata au kusikia mtu akisema anahisi maumivu au kukereketwa eneo la kifuani au sehemu ya juu ya koo la chakula. Basi hicho huitwa kiungulia.
Wataalamu mbalimbali wa masuala ya afya wanafafanua kuwa k iungulia si ugonjwa bali inaweza kuwa dalili ya ugonjwa au mabadiliko ndani ya mwili, kama vile ujauzito, vidonda vya tumbo, au mrundikano wa kemikali tumboni.
Hali hiyo hudumu kwa muda wa saa moja hadi mawili wakati mwingine huchukua muda mrefu zaidi kupotea na kusababisha maumivu na kero kwa watu.
Kiungulia husababishwa na nini?
Kwa mujibu wa tovuti ya afya yako inayojihusisha na masuala ya tiba, tumbo la binadamu limesheheni aina mbalimbali ya kemikali ambazo hufanya kazi ya kumeng’enya chakula, hivyo tumbo limetengenezwa katika namna ya kuhimili kemikali hizo.
“Wakati fulani vali ambayo huruhusu chakula kiingie tumboni na kuzuia kisitoke huwa haifungi vizuri na hivyo kuruhusu chakula chenye kemikali kurudi juu na hivyo kuathiri maeneo ya koo ambayo hayana uwezo wa kuhimili kemikali hizo na ndipo kiungulia hutokea, “ inaeleza tovuti hiyo
Hata hivyo, Kelvin Loti ambaye ni daktari katika zahanati ya Arafa iliyopo Mbezi Kibamba jijini Dar es salaam anasema asilimia kubwa ya watu hupata kiungulia kutokana na vyakula wanavyokula pamoja na mtindo wa maisha.
“Kuna sababu nyingi za kiungulia, kiujumla husababishwa na kujaa kwa gesi tumboni pamoja na kemikali (asidi), baadhi ya mambo mengine ni pamoja na kutumia vilevi kupita kiasi, uvutaji wa sigara, kutokuwa na mpangilio mzuri wa kula pamoja na msongo wa mawazo, ” anasema Dk Lotti.
Unawezaje kuepuka kiungulia?
Kula kwa wakati
Dk Lotti anashauri ili kuepuka kiungulia ni vema kujiwekea mpangilio au ratiba ya chakula na kuifuata kwani tumbo linapokuwa halina chakula kwa muda mrefu, kemikali ambazo zipo kwa ajili ya kumeng’enya chakula huanza kushambulia kuta za tumbo ambapo huathiri pia vali ya chini.
Zinazohusiana
Epuka aina fulani za chakula
Kuna baadhi ya vyakula ambavyo husababisha kiungulia kwa baadhi ya watu na huchangia kuongeza gesi kwa wingi tumboni au vina asidi nyingi, hivyo kukwepa chakula cha aina hiyo kunaweza kusaidia.
Vyakula kama vitunguu, matunda ya jamii ya michungwa, chakula chenye mafuta mengi, vinywaji vyenye kafeini ( kahawa na chokoleti) pamoja na Vinywaji vyenye kaboni (soda) ni miongoni mwa vyakula vinavyoweza kusababisha kiungulia.
Hata hivyo Dk Lotti anashauri kula vitu kama ndizi mbivu, parachichi, mchicha, tikiti maji na tangawizi pamoja na kunywa maji mengi kama tiba ya kiungulia.
Kutokunywa dawa bila muongozo wa daktari
Kwa mujibu wa Dk Lotti matumizi holela ya dawa za antibiotiki pamoja na dawa za husababisha kupata kiungulia.
Usivute sigara
Kwa mujibu wa tovuti ya afya yako, kemikali ya nicotine inayopatikana kwenye bidhaa za tumbaku hudhoofisha vali (esophageal sphincter ya chini) ambayo huzuia chakula kinachomeng’enywa kurudi kinywani na hivyo kusababisha kiungulia.
Matibabu
Ukiachana na sababu za mtindo wa maisha, tatizo la kiungulia linapokuwa sugu unashauriwa kutembelea kituo cha afya kwa ajili ya vipimo ili kupewa dawa inayoendana na chanzo cha tatizo lako.