Kitendawili: Kwa nini ‘ngada’ inalimwa zaidi Tanzania licha ya operesheni kali za dawa za kulevya?
- Mashamba ya bangi yaongezeka takriban mara mbili ndani ya miaka minne kutoka 49 mwaka 2018 hadi 87.
- Arusha, Morogoro, Mara na Ruvuma ni miongoni mwa mikoa inayolima zaidi zao hilo.
Dar es Salaam. Mapema Agosti mwaka huu Serikali ya Tanzania ilitangaza kukamata magunia 131 ya bangi, kilo 120 za mbegu za bangi na kuteketeza jumla ya hekari 489 za mashamba ya bangi mkoani Morogoro, katika moja ya operesheni kubwa za kutokomeza dawa za kulevya iliyowahi kufanyika nchini.
Katika operesheni hiyo Kamishna wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Aretas Lyimo anasema wakulima hao wa bangi hufanya uharibifu mkubwa wa mazingira kwa kuchepusha maji pamoja na kukata misitu ili kufanya kilimo cha zao hilo haramu.
Watu 18 walikamatwa katika operesheni hiyo iliyoshika mjadala katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii baada ya mamlaka hiyo kueleza kuwa watuhumiwa hao walikuwa wakifanya kilimo katika mazingira ambayo si rahisi kufikika.
Hili ni miongoni mwa matukio makubwa ya kudhibiti dawa za kulevya ndani ya miaka mitano, jambo linaloashiria kuwa washirika wa dawa hizo hatari kwa afya ya binadamu wanaendelea kuzalisha licha ya jitihada za Serikali na wadau kuzidhibiti.
Mashamba ya bangi yaongezeka takriban mara mbili
Mwaka 2021 tani 22.74 za bangi zilikamatwa nchini Tanzania ikiwa ni ongezeko la asilimia 72 ya kiasi kilichokamatwa mwaka 2020.
Aidha, takwimu za uhalifu nchini zilizopo katika kitabu cha hali ya uchumi mwaka 2022 kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonesha mashamba ya bangi yameongezeka takriban mara mbili ndani ya miaka minne kutoka 49 mwaka 2018 hadi kufikia mashamba 87 mwaka 2022.
Soma zaidi
-
Vijana katikati ya mapambano ya kuachana na dawa za kulevya Tanzania
-
Ujuzi wa kidijitali unaoweza kuwatoa vijana kimaisha
Hata hivyo, swali linalogonga vichwa vya wengi ni kwa nini kilimo cha zao hilo haramu kinaendelea kushamiri licha ya hatua za kisheria kuchukuliwa?
Mahitaji ya pesa, ukosefu wa ajira watajwa
Baadhi ya wataalamu na baadhi ya wakazi wa mikoa inayoongoza kulima bangi wanasema sehemu kubwa ya vijana hujiingiza katika kilimo cha zao hilo haramu kujipatia kipato kutokana na ukosefu wa ajira.
John Shio mkazi wa jijini Arusha ameiambia Nukta Habari kuwa isingekuwa fedha hakuna kijana ambaye angejiingiza kwenye biashara hiyo ambayo iwapo utabainika unajihusisha adhabu yake ni faini na kifungo cha miaka thelathini au vyote kwa pamoja.
“Katika mkoa huu (Mara) ongezeko la kilimo cha bangi limechangiwa na baadhi ya watu kutegemea zao hilo kuwapatia pesa ndogondogo kukidhi mahitaji yao ya kila siku,” anasema Charles Mashoto, mkazi wa mkoa wa Mara.
Mkoa anaokaa Charles ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa kulima zao hilo Tanzania.
Mashoto anasema watu wanaojikita kwenye biashara ya dawa za kulevya wamekosa ubunifu wa kutafuta vyanzo halali vya fedha jambo linalowafanya wakimbilie huku wapate fedha za mseleleko.
Bangi hulimwa maeneo yasiyofikika
Hata hivyo, baadhi ya wakazi wa mkoa wa Morogoro akiwemo Paskali Mengi, wanaamini jiografia ya baadhi ya maeneo yao hususani yaliyopo milimani inaweza kuwa sababu inayofanya mashamba ya bangi kuongezeka kwa kuwa si rahisi kugundulika.
“Wakulima wa bangi hawalimi karibu na mashamba ya mazao ya chakula ama kibiashara, bali huingia ndani kabisa ya mapori au nyuma ya milima pasipoweza kufikika kwa urahisi, huko huanza wao kufyeka na kuanzisha kilimo cha zao hilo haramu,” Mengi ameiambia Nukta habari.
Maeneo ambayo wahalifu hao hulima, kwa mujibu wa Mengi, si rahisi kufikika kirahisi na vyombo vya dola ambavyo kwa sehemu kubwa vinakabiliwa na uhaba wa watumishi.
Ni wazi kuwa, maeneo hayo yanahitaji oparesheni za mara kwa mara, elimu kwa jamii inayozunguka maeneo husika pamoja na kuhamasisha maadili mema kwa jamii ili kukomesha kabisa kilimo cha bangi.
Eveline Kivuyo, Mkurugenzi msaidizi wa kituo cha kutibu uraibu wa madawa ya kulevya cha Moshono kilichopo jijini Arusha ameiambia Nukta habari kuwa Kama Serikali ikiboresha miundombinu na kupekeleka huduma za jamii katika maeneo hayo itawasaidia vijana wengi kuachana na kilimo cha bangi.
“Wakiboreshewa miundombinu na kupewa elimu juu ya kilimo cha kisasa, kupewa pembejeo pamoja na kufahamishwa madhara ya kilimo hicho itawasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza ongezeko la bangi,” amesema Kivuyo.

Serikali inafanya nini kutokomeza bangi?
Lyimo anasema Serikali inaendelea kufanya oparesheni za kutafuta, kuzuia na kuteketeza zao hilo ambapo kuanzia mwaka 2017 mpaka mwezi Juni, 2023 jumla ya hekari 2,274 na tani 712.81 za bangi ziliteketezwa.
Aidha, Katika maadhimisho ya kupinga matumizi ya madawa ya kulevya duniani yaliyofanyika Julai 3, 2023 jijini Arusha, Lyimo alieleza kuwa mamlaka yake kwa kushirikiana na wadau wa kilimo watatoa mapendekezo ya mazao mbadala hususan katika maeneo yanayolima bangi zaidi ili kusaidia kuwaingizia kipato.
DCEA inaeleza kuwa bangi hulimwa zaidi katika mikoa ya Arusha, Manyara, Mara, Morogoro, Njombe, Iringa na Ruvuma, huku ile inayolimwa Arusha ikitajwa kuwa na athari zaidi.
“…serikali inaendeleza ushirikiano na sekta binafsi na za kimataifa zinazosaidia mapambano dhidi ya dawa za kulevya, utoaji wa elimu kwa wananchi, ufunguzi wa kliniki, ufunguzi wa ofisi za kikanda na mikoa, kufungua mashtaka kwa watuhumiwa wanajihusisha na utaifishaji wa mashamba ya kilimo haramu,” alisema Lyimo.
Latest