DCEA kutumia mbinu shirikishi kukabiliana na dawa za kulevya Tanzania

December 8, 2023 11:54 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kupitia kutoa elimu kwa viongozi wa Serikali za mitaa na vijiji.
  • Itasaidia kukabiliana na mbinu mpya za waraibu ikiwemo kutumia dawa tiba kujilevya.
  • DCEA yaonya kuendelea kuchukua hatua kwa wale wote watakaobainija kujihusisha na madawa ya kulevya.

Mwanza. Wadau, jamii pamoja na Serikali wanatakiwa kuongeza zaidi juhudi za kukabiliana na dawa za kulevya nchini Tanzania ili kuepukana na athari zake ikiwemo kupunguza nguvu kazi ya Taifa mara baada ya hivi karibuni kuibuka mtindo mpya wa matumizi ya dawa hizo kwa kutumia dawa tiba.

Awali matumizi makubwa ya dawa za kulevya yalikuwa yakihusisha dawa za heroini, kokeini, bangi, pamoja na mirungi ambapo kutokana na jitihada kubwa za kukabiliana nazo watumiaji wameanza kutumia dawa tiba zenye asili ya kulevya kama mbadala wake.

Dawa hizo aambazo kwa jina lingine hufahamika kama  kemikali bashirifu hutumiwa zaidi hospitalini hususan wakati wa kufanya upasuaji.

Afisa Elimu kwa umma kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini ( DCEA) Dezidel Tumbu, aliyekuwa akizungumza na Watendaji wa kata na Mitaa wa Wilaya ya Ilemela amebainisha kuwa wamebaini matumizi ya dawa hizo kuwa katika kiwango kikubwa ambapo waraibu wanazitumia kama mbadala wa dawa za kulevya.

” Tunashirikiana na ofisi ya mkemia mkuu wa Serikali pamoja na Mamlaka ya Vifaa Tiba( TMDA) kupita kwenye maduka ya dawa za binadamu kuona kama dawa hizo zinachepushwa na kutumika kwa malengo mabaya,” amesema Tumbu jijini Mwanza.


Soma zaidi : Kitendawili: Kwa nini ‘ngada’ inalimwa zaidi Tanzania licha ya operesheni kali za dawa za kulevya?


Kwa mujibu wa Tumbu miongoni mwa viashiria vya mapema vya kubaini ongezeko la matumizi ya madawa ya kulevya katika eneo husika ni pamoja na uwepo wa mateja ( waraibu) wengi kwenye eneo husika, ongezeko la vibaka, michezo ya kamali na upotevu wa vitu vya thamani, vijana kutoonekana mtaani muda mwingi na kupungua kwa shughuli za uzalishaji.

Tumbu amebainisha kuwa mikoa ya Kanda ya Ziwa ni miongoni mwa mikoa yenye matumizi makubwa ya dawa za kulevya  hususan bangi na mirungi ambayo mara kadhaa wamekuwa wakiikamata mashambani.

Pamoja na Sheria kali za kudhibiti madawa ya kulevya bado Tanzania inakabiliwa kwa wingi na vitendo vya kilimo cha mazao hayo haramu.

Mwaka 2021 tani 22.74 za bangi zilikamatwa nchini Tanzania ikiwa ni ongezeko la asilimia 72 ya kiasi kilichokamatwa mwaka 2020.

Aidha, takwimu za uhalifu nchini zilizopo katika kitabu cha hali ya uchumi mwaka 2022 kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonesha mashamba ya bangi yameongezeka takriban mara mbili ndani ya miaka minne kutoka 49 mwaka 2018 hadi kufikia mashamba 87 mwaka 2022.


Soma zaidi : Vijana katikati ya mapambano ya kuachana na dawa za kulevya Tanzania


Kwa mujibu wa Tumbu, Ili kukabiliana na hali hiyo DCEA imeona ni vyema kutoa elimu kwa jamii kupitia kwa viongozi wa kata na mitaa ili iwe rahisi kudhibiti vitendo hivyo vinapotaka kutokea.

“Tukaona pamoja na zoezi la kufanya operesheni za mara kwa mara lakini ni vyema tukatoa elimu kwa jamii kupitia viongozi wa kata na mtaa ambao ndio hukaa na wananchi karibu lengo tukiwaelisha wao tunakuwa tumeisaidia jamii kwa kiwango kikubwa,” amesema Tumbu.

Kwa upande wake Afisa Sheria Mkuu DCEA, Christina Rweshabura amesema katika kipindi cha muda mfupi wamefanikiwa kukamata watu 11 waliokuwa wanajihusisha na kusafirisha bangi, ambapo pia walifanikiwa kukamata magunia 57  ya bangi kavu na gunia  50 za mbegu aina ya bangi.

Sheria ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya Sura ya tano inabainisha kuwa mtu atakayebainika kujhusisha na dawa za kulevya kuanzia kilo 100 atahukumiwa kifungo cha maisha jela.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW