Kifo cha aliyeng’atwa na nyoka Babati, Wahudumu wa afya watatu wasimamishwa kazi
- Uchunguzi ukikamilika wahudumu hao watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria
Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Babati Hamisi Malinga amewasimamisha kazi wahudumu watatu wa afya walioshindwa kumhudumia mgonjwa aling’atwa na nyoka baada ya kukosa pesa ya matibabu hali iliyiosabisha kifo chake.
Taarifa ya Kaimu wake, Benedict Ntabagi, iliyotolewa leo Disemba 19, 2024 inabainisha kuwa wahudumu hao wamesimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
“Kufuatia tukio hilo…amewasimamisha kazi watoa huduma watatu wa Kituo cha Afya Magugu (Afisa tabibu, Afisa Muuguzi msaidizi na Mteknolojia wa dawa) kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo ili kupisha uchunguzi wa tukio hili,” imesema taarifa ya Ntabagi.
Taarifa hiyo inakuja ikiwa ni siku nne tangu kutokea kwa tukio hilo lililoibua hisia za Watanzania na viongozi wa Serikali ikiwemo Waziri wa Afya Jenista Muhagama aliyeshangazwa na wahudumu hao wa kituo cha afya Magugu kushindwa kumhudumia mgonjwa kwa kukosa fedha.
Aidha, Ntabagi amebainisha kuwa uchunguzi wa tukio hili unaendelea kufanyika kwa ushirikiano wa timu ya wataalamu wa halmashauri, mkoa na mabaraza ya kitaaluma na hatua kali zitachukuliwa kwa wote watakaobanika kuwa na hatia katika tukio hilo.
Hata hivyo, taarifa hiyo haiwajweka wazi wahudumu hao wa afya watasimamishwa kazi kwa muda gani au uchunguzi wa tukio hilo utacukua siku ngapi hadi kukamilika.
Juliana Obed aliyekuwa mkazi wa kitongoji cha Majengo ‘A’ kijiji cha Magugu, tarafa ya Mbugwe alifariki Disemba 15, akiwa kwenye kituo cha afya cha Magugu baada ya wahudumu hao kukataa asipewe huduma kwa kukosa Sh150,000 iliyohitajika kulipia matibabu yake.
Marehemu huyo alifikishwa kituo hicho masaa takribani sita baada ya kung’atwa na nyoka mkono wa kulia ulioonyesha dalili za kuvimba na kubadilika rangi kwa sababu ya kuenea kwa sumu, hali iliyohitaji apatiwe matibabu kwa haraka ili kuokoa uhai wake.
Wataalamu wa afya wa kituo hicho walishindwa kumpa huduma ya dharura wakati wakisubiri malipo yafanyike kinyume na Sera ya Afya na miongozo yake inayotaka makundi maalum kama vile akina mama wajawazito, watoto chini ya miaka mitano, na wazee wasio na uwezo, wanatakiwa kupata matibabu bure.
Aidha, kwa huduma za dharura, mgonjwa yeyote anatakiwa kutibiwa mara moja na masuala ya malipo yanafuata baada ya huduma kutolewa.