Kasi ya ukopeshaji sekta binafsi yapaa mara tatu

March 13, 2019 7:08 am · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Zaidi ya robo ya mikopo iliyokopeshwa ndani ya kipindi cha mwaka moja ilielekezwa kwa watu binafsi ikifuatiwa na shughuli za biashara.
  • Kiwango cha riba za benki za biashara kwa sekta binafsi chashuka kidogo.

Dar es Salaam. Ukopeshaji Sekta binafsi umeanza kurejea kwa kasi baada ya mikopo kwa sekta hiyo kupaa zaidi ya mara tatu ndani ya mwaka mmoja hadi asilimia 7.3 Januari mwaka huu kutoka asilimia 2.1 iliyorekodiwa Januari 2018.

Katika hotuba yake ya Mapendekezo ya Serikali ya mpango wa maendeleo wa Taifa na ya kiwango na ukomo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/20 kwa wabunge Machi 12, 2019, Waziri wa Fedha na Mipango Dk Philip Mpango amesema mikopo kwa sekta binafsi iliendelea kuimarika kutokana na utekelezaji wa sera ya kuongeza ukwasi kwenye uchumi pamoja na jitihada zilizochukuliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika kuchochea ongezeko la mikopo kwa sekta hiyo.

“Sehemu kubwa ya mikopo kwa sekta binafsi imeendelea kuelekezwa katika shughuli binafsi ikiwa ni asilimia 27.9 ya mikopo yote ikifuatiwa na shughuli za biashara zilizopata asilimia 18.4, uzalishaji viwandani (asilimia 11.6) na kilimo asilimia 7.8,” amesema Dk Mpango.

Miaka miwili iliyopita kasi ya ukopeshaji wa sekta binafsi ilishuka kidogo kutokana na kuongezeka kwa kiwango cha mikopo chechefu katika sehemu kubwa ya benki nchini.


Soma zaidi:


Mwaka 2017 kiwango cha ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi, kwa mujibu wa Kitabu cha Hali ya Uchumi mwaka 2017 kiliongezeka kwa kasi ndogo ya asilimia 1.7 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 7.2 uliokuwa umerekodiwa mwaka 2016 kutokana na tahadhari iliyochukuliwa na benki za biashara kuepuka uwezekano wa kupata hasara baada ya kuongezeka kwa mikopo chechefu.

Mbali na kuongezeka kasi ya ukopeshaji katika sekta binafsi, Dk Mpango amesema riba za mikopo ya benki za biashara kwa sekta binafsi zimeendelea kupungua kutoka wastani wa asilimia 17.8 mwaka 2017 hadi wastani wa asilimia 17.4 mwaka 2018.

Hata hivyo, kumekuwa na malalamiko miongoni mwa watumiaji wa huduma za kifedha nchini kuwa riba inayotozwa na benki hizo za biashara ni kubwa mno kiasi cha kuwafanya washindwe kupata mikopo inayoweza kusaidia kuendesha biashara zao.

Enable Notifications OK No thanks