Kampuni za kompyuta zinavyosukumia mbali matumizi ya ‘CD’, ‘DVD’
- Matoleo mengi ya kompyuta mpakato, hayana sehemu ya kuwekea CD au DVD.
- Lengo la kutotumia teknolojia hiyo ni kupunguza uzito na kuongeza ufanisi wa kompyuta husika.
- Mbadala wake ni vifaa huru vya kuhifadhia kumbukumbu au mtandao.
Dar es Salaam. Mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanazidi kuongeza bidhaa mpya kwenye uso wa dunia huku yakizidi kutelekeza zile za zamani zisizoendana na kasi ya mabadiliko hayo.
Mabadiliko hayo yanaweza kuonekana kwenye nyanja tofauti ikiwemo utengenezaji wa kompyuta ambazo tangu ugunduzi wake, zinakuja na muonekano na muundo tofauti.
Maboresho hayo yanawezesha kompyuta kuwa nyepesi na kuondoa baadhi ya sehemu zake ambazo zimerahisisha utendaji wa shughuli mbalimbali za binadamu.
Kati ya teknolojia iliyopo hatarini kusahaulika ni ile ya “Optical drive” ama kwa lugha nyepesi inajulikana kama deki ya “CD” na “DVD” kwenye kompyuta mpakato.
Teknolojia hiyo ambayo kwa mara ya kwanza ilionekana kwenye kompyuta aina ya Compaq (16-bit COMPAQ SLT/286) inazidi kutoweka katika ulimwengu wa kompyuta kwani makampuni mengi ya kutengeneza kompyuta yakiwemo HP, Apple na Lenovo yanaondoa teknolojia hiyo kwenye bidhaa zake.
Siyo tu kompyuta hazina sehemu ya kuwekea DVD, bali hata deki za kawaida zinazotumia bidhaa hiyo, matumizi yake yamepungua sana kwenye jamii. 
Kati ya teknolojia iliyopo hatarini kusahaulika ni ile ya “Optical drive” ama kwa lugha nyepesi inajulikana kama deki ya “CD” na “DVD” kwenye kompyuta mpakato. Picha| Mtandao.
Huenda unajiuliza ni kwanini kila uonapo kompyuta za kisasa, hauoni sehemu za kuweka CD wala DVD na unajiuliza nini kipya kitakuja baada ya teknolojia hiyo kutoweka kabisa. Kwa nini teknolojia hiyo inatoweka kwa kasi?Na nini mbadala wake?
Mahitaji ya nafasi kubwa
Wakati teknolojia ya DVD ikiwa na uwezo wa kuhifadhi “data” hadi Gigabyte (GB) 8.5 tu ambazo kwa wapenzi wa filamu huenda ukahifadhi filamu takribani tano zenye ukubwa wa GB2, teknolojia imeibua “Flash drive” ambazo zinakuja na ukubwa wa hadi Telabaiti (TB) mbili.
TB2 ni sawa na GB2,000 na hivyo kumpa mawanda mapana zaidi mtu anayehifadhi kumbukumbu nyingi. Mbali na hapo, ipo teknolojia ya “External drive” ambayo inapatikana kwa ukubwa wa hadi Terabaiti 16 sawa na GB elfu 16.
Wepesi na udogo
Kwa mujbu wa tovuti ya “Digital trends”, kompyuta mpakato ya Acer Swift 7 ndiyo kompyuta nyepesi zaidi kwani ina uzito wa kilo 0.88 tu na hivyo kuvutia watu wengi kwani hakuna apendaye kubeba mzigo mzito mgongoni wakati wa safari.
Hata hivyo, makampuni mengi yanazidi kuboresha bidhaa hizo kulingana na mahitaji ya wateja wake, Kwa sasa kompyuta za Apple za Macbook Air na matoleo mengine ya Mac, hayana kabisa teknolojia ya CD na DvD.
Zinazohusiana
- Window 95 yaja kivingine baada kutoweka sokoni kwa miaka 18
- Microsoft kuwezesha upigaji simu kwa kompyuta
Hata hivyo, kila teknolojia inayoibuka inakuja na changamoto zake. Kwa kompyuta ambazo hazina sehemu ya kuwekea CD, zinampatia mtumiaji gharama za kununua kifaa cha huru za kutunza taarifa “Flash Drive” na hata “External disk” ambazo zinakuja na gharama kubwa zaidi.
Uhifadhi wa kumbukumbu mtandaoni
Hapo awali, watumiaji wengi wa kompyuta walihitaji CD kwa ajili ya kuhifadhi taarifa mbalimbali lakini kutokana na uwepo wa hifadhi za mtandaoni kama Google drive na I cloud, hakuna tena haja ya teknolojia hiyo.
Mtandao umekuwa njia urahisi kuliko hata teknolojia ya CD ambapo upotevu na uharibikaji zilikuwa ni baadhi ya changamoto zilizoikumba teknoljia hiyo.
Lakini ukitunza kumbukumbu zako mtandaoni, hata CD au kompyuta ikiharibi au kupotea, data zako utazikuta mahali salama.
Kompyuta mpakato ya Acer Swift 7 ndiyo kompyuta nyepesi zaidi kwani ina uzito wa kilo 0.88. Picha| Acer.
Licha ya kuwa kompyuta mpya zinakuwa na uwezo mkubwa wa kumbukumbu, bado zinawapa watumiaji wake tahadhari ya kuwa na benki nyingine ya kumbukumbu kwa ajili ya usalama.
Hitaji hilo ni kwa dharura pale kompyuta itakapoharibika bila matarajio. Hivyo ni kusema, unahitaji takribani Sh643,000 kununua External drive yenye TB mbili ambayo ni gharana ya ziada na ya juu zaidi ikilinganishwa na CD zilizouzwa kwa takribani chini ya Sh 5,000.
Baadhi ya watumiaji, wamesema hawana tatizo na kuondolewa kwa teknolojia hiyo kwenye kompyuta zao kwani hawakuzitumia hivyo hazikuwa na maana.
Sharifa Miraj ambaye ni Mwanamuziki anayetumbuiza sehemu mbalimbali jijini Dar es salaam amesema mbali na kuweka ripoti yake ya chuoni kwenye CD, hajawahi kutumia teknolojia hiyo tangu anunue kompyuta yake mwaka 2016.
“Kazi zangu natumia flash kwa sababu ni rahisi kutumia, CD haifai uanze kuhamisha hizo kazi sidhani hata kama ninaweza. Japo najua ilikuwa inampa mtumiaji mawanda mapana ya matumizi,” amesema Miraj.
Latest
