Mambo muhimu ya kufahamu kuhusu kompyuta, programu tumishi

July 11, 2022 7:02 am · admin
Share
Tweet
Copy Link

Utendaji wa kompyuta hutegemea ufanisi wa vifaa vinavyoonekana na visivyoonekana. Picha| Daud Mbapani.


  • Kompyuta inaundwa na vifaa vinavyoonekana (hardware) na visivyoonekana (software).
  • Vifaa hivyo hufanya kazi kwa kutegemeana.

Dar es salaam. Je wewe ni mtumiaji wa vifaa vya kielektroniki zikiwemo kompyuta mpakato na vishkwambi? Inawezekana maneno haya si mageni masikioni mwako na huenda umekuwa ukipata wakati mgumu kuyaelewa na kuyatofautisha.

Maneno hayo ni “hardware” (Vifaa vinavyounda kompyuta) na “software” (programu tumishi)

Nianze kwa kukueleza kwa nini nimeita ‘hardware’ vifaa, ni kwa sababu hivi ni vitu vinavyounda mfumo wa kompyuta na vinavyoshikika kwa mikono.

Software ni programu tumishi kwa sababu hazishikiki kwa mikono lakini ndizo huziendesha hardware zifanye kazi kwa kuzielekeza nini na namna gani ya kufanya.

Kiufupi vifaa hivi ambavyo ni hardware haviwezi kufanya kitu chochote bila programu endeshi yaani software na programu endeshi hazitakuwa na cha kufanya bila ya hardware. 

Vifaa vya Hardware ni vipi?

Hardware inahusisha vifaa vyote vya ndani na nje ya kompyuta ambavyo unaweza kushika na kuona. Baadhi ya vifaa vya nje vya kompyuta ni kicharazio, kipanya, spika na skrini.

Sehemu za ndani za hardware ni pamoja na bodi ya kompyuta, saketi ya uchakataji (CPU), kihifadhi programu tendeshi (RAM) pamoja na kihifadhi data (Hard disc). Vifaa hivi tunaweza kuviita injini ya kompyuta. 


Zinazohusiana: 


Programu endeshi (software)

Hizi ni programu zinazoongoza vifaa vilivyopo kwenye kompyuta. Huwa na mfumo ambao huelekeza vifaa kitu gani na namna gani ya kufanya. Zipo programu zenye mifumo  endeshi ambazo zimetengenezwa kwa ajili ya kuiongoza kompyuta kwa ujumla na zipo programu endeshi ambazo huwa na kazi maalum tu.

Mathalan, programu zenye mifumo endeshi ya kuongoza kompyuta ni kama macOS kwa kompyuta za Apple na Microsoft Windows. 

Mifumo hii inadhibiti spidi ya kompyuta katika kuchakata vitu, utunzaji kumbukumbu, ulinzi na utendaji kazi kwa ujumla. Hizi hufanya kazi pale tu kompyuta inapokuwa imewashwa.

Programu endeshi  ambazo hutengenezwa kwa ajili ya kazi maalum tu ni kama vicheza muziki au video, mfano VLC, programu kwa ajili ya kuandikia pamoja na programu tafutishi kama Chrome au Brave. Hizi hufanya kazi pale tu zinapokuwa zimefunguliwa.

Leo tuishie hapa. Tukutane wiki ijayo katika uchambuzi wa masuala mbalimbali ya teknolojia.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW