Kompyuta tano za mezani za kutupia macho 2023
- Ni pamoja na iMac M1 2021 pamoja na Dell XPS 8950
- Nyingi zimefanyiwa maboresho makubwa ili kukidhi ushindani.
Dar es Salaam. Inaweza ikakushangaza kidogo kuona nazungumzia kompyuta za mezani (desktops) katika zama hizi ambazo matumizi ya kompyuta mpakato (laptops), vishkwambi (tablets) pamoja na simu janja yamechukua nafasi zaidi kutokana na kukua kwa teknolojia.
Kwa mujibu wa tovuti ya Cnet ya nchini Marekani ambayo huchapisha habari za teknolojia hivi sasa ni hudusi tu (moja ya tano) ya kompyuta zinazouzwa duniani ni za mezani.
Hii ni kumaanisha idadi ya watu wanaotumia desktop inazidi kupungua siku baada ya siku, ingawa bado haituzuii kutizama kompyuta bora ambazo mtumiaji anaweza kuzitupia macho kwa mwaka huu 2023.
Ifuatayo ni orodha ya kompyuta tano ambazo tovuti ya Cnet imezifanyia majaribio na kuona zinafaa kutupiwa macho kutokana na ubora wake, kasi ya kuchatakata, uwezo wa kuhifadhi vitu pamoja na gharama yake:
5. Origin PC 5000 T
Namba tano inashikwa na kompyuta hii ambayo ni maalumu kwa ajili ya michezo (games), ambayo inatengenezwa na kampuni ya Origin Cop ya nchini Marekani.
Kwa mujibu wa tovuti ya teknolojia, kompyuta hizi za magemu huwa na bei kubwa kutokana na uwezo wake mkubwa unaohitajika ili kufanya kazi kwa ufanisi.
Tofauti kubwa iliyopo kati ya kompyuta za michezo na kompyuta za kawaida ni kwamba kompyuta za magemu huja na kadi bora za picha za hali ya juu (GPU) pamoja na kuwa na prosesa zenye uwezo mkubwa.
Kompyuta hii ina prosesa ya AMD Ryzen 5 5600 pamoja na kadi ya picha (GPU) ya NVIDIA 8GB ambayo itakuwezesha kucheza michezo yako vyema.
Pamoja na kwamba ukinunua kompyuta hii utapewa kicharazio na vifaa vya kusikilizia bure, itakulazimu kuwa na Sh11.8 milioni za Tanzania au Dola 5,000 za Marekani ili kuinunua.
Soma zaidi:
- Jinsi ya kufanya mitandao ya kijamii isikuharibie mahusiano yako
-
Mbinu tano za kudhibiti matumizi makubwa ya intaneti kwenye ‘smartphones’
4. Apple Mac Mini M1 (2020)
Kama unataka Kompyuta ya bei rahisi kutoka kampuni ya Apple basi Mac Mini M1 ndio suluhu. Apple ni miongoni mwa Kampuni za kwanza kuanza kutumia vichakata (Processor) vya M1 ambazo zinasifika kwa kasi yake.
Unaweza kuipata kompyuta hii ukiwa na Sh1.6 hadi 2.1 milioni kutegemeana na aina katika maduka ya Apple ambapo bei huwa inaongezeka wastani wa Sh100,000 mpaka Sh200,000 katika maduka ya kawaida.
3. HP Envy 34 All-in-One PC
Kampuni ya Apple na Microsoft zimeacha kuzalisha kompyuta za mezani zenye kila kitu kwenye skrini yake, ni Kampuni ya Hp peke yake ndio inaendelea kuzalisha kompyuta hizo na bidhaa iliyopo sokoni kwa sasa ni Hp Envy 34.
Kompyuta hizi huwa na kila kitu katika screen (monitor) yaani kichakata kumbukumbu, kadi ya picha, pamoja na kadi ya kuhifadhia vitu na hii huifanya kuonekana kama laptop ingawa yenyewe ni kubwa zaidi na imetengenezwa maalumu kwa ajili ya kukaa mezani.
Baadhi ya sifa za kompyuta hii ni skrini ambayo ina ukubwa wa nchi 34, ambayo huwa na kamera mtandao, nafasi ya kuhifadhi vitu yenye Gigabaiti 1000 (1TB), kichakata chenye ukubwa GB 16 pamoja na kadi ya picha yenye GB sita.
Ili kuipata itakulazimu kuwa na Dola za Marekani 2,300 yaani milioni Sh5.3 za Tanzania, jipange.
Kompyuta za mezani zinasifika kwa kudumu zaidi kutokana na kutohamishika mara kwa mara. Pichal Esau Ng’umbi.
2. Dell XPS 8950
Kompyuta hii inaweza kutumika katika shughuli zote yaani matumizi ya kawaida na michezo (magemu).
Haina umbo kubwa sana hivyo haitochukua nafasi yako, ni kizazi cha 12 cha kompyuta za Hp ambayo ina kichakata cha i9, kadi ya picha ya RTX 3080 pamoja na nafasi ya kuhifadhi vitu yenye ukubwa wa GB 64 mpaka TB 1 ikiwa na nafasi ya kuongeza zaidi.
Pamoja na hizo sifa andaa kitita cha Sh1.8 milioni au Dola za Marekani 800 ili kuipata.
1. iMac M1 2021 (24-inch)
Kampuni ya Apple imefanya maboresho makubwa katika kompyuta zake toleo la 2021 ambapo unene wa skrini (monitor) umeendelea kupunguzwa na kufanana na ule wa ipad huku upana ukiongezwa
Zimetengenezwa na vichakata vya M1 toleo la mwaka 2020 ambavyo vinaifanya kompyuta hiyo kuwa na kasi zaidi katika ufanyaji wa kazi.
Toleo jipya la kompyuta hizi ina skrini ya nchi 24, kamera yenye kuchukua picha kwa ubora wa pikseli 1080 ambao umeongezeka kutoka pikseli 720 iliyokuwepo awali.
Imetengenezwa kwa ajili ya shughuli za vyombo vya habari, biashara na matumizi binafsi ikiwa na sehemu ya kuhifadhia vitu yenye ukubwa wa GB 256 mpaka 512, spika za sauti, maiki kwa ajili ya simu pamoja na uwezo wa kuunga intaneti isiyo na waya (Wi-Fi).
Ili kuipata kompyuta hii ambayo inatumiwa pia chumba cha habari cha Nukta Habari utatakiwa kuwa na Sh3.04 milioni za au Dola 1300 za Marekani.
Miongoni mwa sifa kuu ya desktop hii ni uimara na kudumu, si kwa sababu hutengenezwa vizuri zaidi ya kompyuta mpakato bali ile hali ya kutohamishika mara kwa mara huchangia kompyuta za mezani kudumu kwa muda mrefu zaidi.
Tangazo:

Latest
