Jukwaa la mtandaoni la “Tujibebe” kusaidia vijana lazinduliwa Tanzania
- Jukwaa hilo la mtandaoni linatoa elimu ya maisha kwa vijana kupitia simu za mkononi.
- Maudhui ya jukwaa hilo yamejikita kuboresha afya, elimu na uchumi kwa wasichana.
- Pia linawaleta pamoja vijana kubadilisha mawazo, uzoefu kuhusu mustakabali wa maisha yao.
Dar es Salaam. Huenda kasi ya vijana hasa wasichana wa Tanzania kuelimika na kufaidika na fursa mbalimbali itaongezeka siku za hivi karibuni kutokana na juhudi za wadau kuwawekea mifumo rahisi ya kupata taarifa muhimu kuhusu maisha yao.
Kampuni ya simu ya Vodacom Tanzania kwa kushirikiana na taasisi ya kimataifa ya Girl Effect wamezindua jukwaa jipya la ‘Tujibebe’ linalotoa elimu ya maisha kupitia simu za mkononi ikiwalenga vijana waliopevuka hasa wasichana wenye umri wa miaka kati ya 15 na 19.
Jukwaa hilo la mtandaoni na mtaani litawaunganisha vijana wenye uzoefu katika ujasiriamali kuwahamasisha vijana wengine na kusaidiana kutatua changamoto za maisha huku wakitimiza malengo yao.
Tujibebe linatumia tovuti pamoja na huduma za simu za IVR (Interactive voice response) kutoa mafunzo kupitia simulizi ya sauti kupitia mtandao wa Vodacom.
Maudhui ya Tujibebe yanalenga kuwapa vijana wa Kitanzania taarifa na rasilimali wanazohitaji kufanya maamuzi sahihi ya maisha yao ikiwemo mafunzo ya kuboresha ujuzi, kuanzisha biashara na kusimamia matumizi ya fedha.
Lakini pia ni njia nyingine ya kuwaunganisha vijana ili kupata elimu ya afya itakayowahakikishia mustakabali mzuri wa maisha yao.
Zinazohusiana:
- Vodacom, Google wazindua manunuzi ya ‘Apps’ kwa njia ya simu
- Usiyoyajua kuhusu mtandao wa 5G
- Kampuni ya Tanzania yashinda tuzo za ubunifu wa huduma za kifedha Afrika
Akizingumza leo (Julai 25, 2019) katika uzinduzi wa jukwaa hilo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation, Rosalynn Mworia amesema huduma hiyo itasaidia kuwafikia vijana hasa wa kike na kuwapatia elimu ya kujitambua hasa katika sekta ya afya, elimu na uwezeshaji kiuchumi.
Amesema Tujitambue inatumia teknolojia rahisi ya simu janja na simu za kawaida kuwafikishia vijana maudhui yanayoendana na mtazamo wao wa maisha.
“Sote tunafahamu kwamba teknolojia ya simu ina uwezo wa kubadilisha dunia, tunafuraha sana kuungana na Girl Effect, kupitia mtandao wetu ambapo tutaweza kuwafikia vijana wengi zaidi na kuwafanya wafikie malengo yao,” amesema Mworia.
Watu walioshiriki katika uzinduzi huo wamepata nafasi ya kuangalia maudhui kutoka kwa mabalozi wa ‘Technology Enabled Girl Ambassadors’ (TEGAs) ambao ndiyo kiini cha taarifa na maudhui yanayotumiwa kuhakikisha jukwaa hilo linakidhi mahitaji ya wasichana na vijana wa Tanzania.
Washiriki kutoka taasisi mbalimbali katika uzinduzi wa jukwaa jipya la ‘Tujibebe’ linalotoa elimu ya maisha kupitia simu za mkononi ikiwalenga vijana waliopevuka hasa wasichana wenye umri wa miaka kati ya 15 na 19, jijini Dar es Salaam leo. Picha|Michuzi.
Akielezea faida za jukwaa la Tujibebe, Mkurugenzi Mtendaji wa Girl Effect, Jessica Odede amesema maudhui ya tujibebe yametengenezwa kwa ajili ya kuwaunganisha vijana wote lakini lengo kubwa ni kubadilisha maisha ya wasichana watakaotumia elimu inayotolewa na jukwaa hilo.
“Mara nyingi vijana huwa na maswali mengi kuhusiana na kesho yao, na hawajui mahali pakupata majibu sahihi kuanzia kuwa na ujuzi kwa ajili ya kupata kazi, jinsi ya kupata pesa na pia namna ya kutunza pesa hizo,” amesema Odede na kuongeza.
“Hapo zamani ilikuwa ni vigumu kwa wasichana kupata taaarifa hizi, leo tunazindua tujibebe ili wakiingia kwenye mtandao wapate elimu mtandaoni, sio tu wapakue mambo ya kufurahisha, bali pia waweze kupata mafunzo ambayo yanagusa maisha yao ya kila siku.
Kwa mujibu wa Mworia, Tujibebe imeanza kutekelezwa katika Wilaya ya Temeke, mbali na kutumia simu wanatumia makundi ya vijana waliopo mtaani kubadilishana uzoefu katika kukabiliana na maisha.
Mpaka sasa wameweza kuwafikia vijana takriban 1,000 kwa kuwafikishia taarifa muhimu ambazo zimeanza kubadilisha maisha yao.
Latest