Kampuni ya Tanzania yashinda tuzo za ubunifu wa huduma za kifedha Afrika

September 3, 2018 8:37 pm · Zahara
Share
Tweet
Copy Link
  • Imeibuka ya kwanza katika tuzo za ubunifu wa huduma za fedha barani Afrika.
  • Ni mara ya kwanza kwa Tanzania kushiriki na kushinda katika tuzo hizo.
  • Wadau washauri vijana kuongeza uthubutu na ubunifu katika biashara, teknolojia.

Dar es Salaam. Kwa mara ya kwanza katika historia ya huduma za fedha mtandaoni, kampuni inayochipukia (start-up) ya NALA kutoka Tanzania imeshinda tuzo za Ecobank Fintech Challenge za ubunifu wa huduma bora za fedha barani Afrika kwa mwaka 2018 zilizofanyika Lome, Togo.

NALA ambayo inatoa huduma za miamala na malipo mbalimbali kwa kutumia simu za mkononi imejinyakulia kitita cha Dola za Marekani 10,000 sawa na  milioni 22.7 za kitanzania.

Kampuni ya NALA imebahatika kushinda tuzo hiyo kwa kuchuana na kampuni 11 za Afrika zinazojihusisha na masuala ya ubunifu na teknolojia katika huduma za fedha.

Katika tuzo za mwaka 2017, washindi wa kwanza hadi watatu walitoka Nigeria hivyo kitendo cha NALA kushiriki kwa mara ya kwanza na kushinda kimekuwa ni motisha kwa vijana wenye mawazo ya kibunifu kutoka Tanzania kuingia katika tuzo hizo.

Ushindi wa NALA ulikuwa siyo wa kubahatisha kwasababu imefanikiwa kurahisisha miamala mbalimbali inayofanyika kwa kutumia App moja (Programu) ambayo unaweza kutuma na kupokea pesa, kununua LUKU, kununua vifurushi vya simu bila kubadilisha laini au mtandao.

“Napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mungu kwa kutuwezesha kufikia hatua hii na NALA kushinda tuzo hii ya Ecobank Fintech Challenge,” anaeleza Benjamin Fernandes mwanzilishi wa NALA.


Zinazohusiana: NALA yaja na teknolojia ya kijanja kutuma, kupokea pesa


Ushindi huu unaashiria kuwa wabunifu wa Tanzania waliojikita katika masuala ya teknolojia wanaweza kufika mbali zaidi wakifanya kazi kwa bidii na kuthubutu kushiriki mashindano mbalimbali na kuiwakilisha vyema nchi.

“Hongera sana Benjamin Fernandes, Tanzania inazidi kung’ara kwa weledi na kipawa endelea kuangaza,” ameandika Isaya Yunge kwenye ukurasa wake wa Twitter, ambaye ni mwanzilishi wa Soma App inayowasaidia wanafunzi kupata huduma za ufadhili wa masomo ya nje.

Mshindi wa pili ilikuwa kampuni ya Visual Identity kutoka Afrika Kusini na watatu ni Wallet (Nigeria). Washindi wote watatu watapata nafasi ya kufanya mafunzo kwa vitendo ya miezi sita kutoka benki ya Ecobank ili kuwajengea uwezo wa kuendesha shughuli zao.

Benjamin Fernandes (aliyeva bendera ya Tanzania) akipokea hundi ya pesa za Dola za Marekani 10,000 kama zawadi ya mshindi wa kwanza kwenye tuzo za Ecobank Fintech Challenge za ubunifu wa huduma bora za kifedha barani Afrika kwa mwaka 2018 zilizofanyika jijini Lome, Togo.

Wadau mbalimbali wa masuala ya vijana na ujasiriamali wamesema ushindi wa NALA uwe chachu kwa vijana ambao wana ndoto za kutatua changamoto za jamii na kutafuta suluhisho la ukosefu wa ajira.

“Hicho ni kitu cha kujifunza kwetu vijana wa kitanzania, tusiwe na imani kwamba kampuni kubwa za teknolojia ziwe zinatokea kutoka ‘Silicon Valley’, ni muda wetu sasa,” ameandika Marra Matta katika mtandao wa Instagram. 

Kwa upande wake, Mwanzilishi wa taasisi ya Nyumbani Street Icon, Olary Tomito katika ukurasa wake wa Instagram, amewashauri vijana kujenga ushirikiano katika utendaji wa shughuli zao za kila siku, “Nawapa hongera sana kwa timu yote ya NALA money kwa ushindi huu.” 

Enable Notifications OK No thanks