Mambo ya kuzingatia kabla ya kuoa/kuolewa

January 28, 2026 8:42 am · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni muhimu kuzingatia tabia na mwenendo wa mtu bila kusahau vipaumbele vyako.
  • Pia jiulize kama huyo mtu uliyemchagaua unampenda au laa.

Dar es Salaam. Kufunga ndoa ni miongoni mwa maamuzi makubwa na nyeti zaidi katika maisha ya mwanadamu yanayohusisha upendo, uaminifu, majukumu, na mshikamano wa kifamilia.

Wengi huingia kwenye ndoa wakiwa na matumaini makubwa ya furaha, lakini bila maandalizi ya kutosha, hujikuta wakikumbana na majuto na vilio visivyo na mwisho au kuangukia kwenye talaka.

Kwa mujibu wa Takwimu muhimu zilizotolewa na Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (Rita) Juni 2024, idadi ya talaka zilizosajiliwa iliongezeka kutoka 447 ya mwaka 2022 hadi 711 mwaka 2023.

Takwimu hizo ni sawa na kusema zaidi ya nusu ya ndoa zilizofungwa mwaka 2023 (asilimia 59) zilivunjika kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kukosa maandalizi kwa ajili ya safari hiyo muhimu maishani.

Hivyo, kabla ya kusema ‘ndiyo’ mbele ya familia, jamaa na jamii, na mwisho wa siku kuishia kutengana ni muhiimu kufanya maandalizi muhimu na kujiuliza maswali ya msingi ikiwemo suala la dini.

Dini hujenga misingi ya maadili, uaminifu na hofu ya Mungu ndani ya ndoa hivyo, tofauti za kidini zisipojadiliwa mapema, huweza kuleta migogoro mikubwa kifamilia. Picha/Canva.

Ndiyo, ili uweze kufunga ndoa nchini Tanzania ni lazima iwe ya kidini, ya kiserikali au ya kimila hivyo suala la kujua kuwa mwenzi wako wa maisha anaamini dini gani ni muhimu kama anavyoeleza Ustadhi Athuman Othman kutoka mkoani Tanga.

“Hakikisha mwenzi wako ana dini, hofu ya Mungu na maadili mema. Dini ndiyo nguzo kuu ya subira, uaminifu na uadilifu katika ndoa,” anasisitiza Ustadhi Othuman.

Tofauti za kidini zikipuuzwa zinaweza kusababisha migongano ya kifamilia, malezi ya watoto, na hata uhusiano wa kijamii katika maisha ya ndoa.

Kumfahamu mtu unayemuoa/kuolewa naye

Askofu Mathias Anthony, kutoka Kanisa la Mwanakondoo jijini Dar es Salaam ameiambia Nukta habari kuwa ni jambo la msingi kwa mtu kumfahamu kwa kina mwenza wake kabla ya kuchukua uamuzi wa kufunga ndoa. 

Ameeleza kuwa kufahamiana kunapaswa kuanzia katika historia ya maisha, tamaduni, malezi pamoja na maoni ya jamii anayotoka mwenza huyo.

“Kutokumfahamu mwenza wako vyema kunaweza kusababisha migongano ya mara kwa mara ndani ya ndoa, hasa pale tofauti za tamaduni na mitazamo zinapojitokeza bila maandalizi ya awali, anasema Askofu Anthony.

Akikazia hoja hii, mtaalamu wa saikolojia kutoka mkoani Tanga Tatu Mbuguni , anasema kabla ya kuoa au kuolewa ni muhimu mtu kuorodhesha vipaumbele vyake na kupata muda wa kutosha wa kufahamiana na mwenza wake ili kujenga uelewa wa kina kuhusu tabia na misimamo ya kila mmoja.

Fedha ni nyenzo muhimu katika kupanga na kutimiza mahitaji ya familia. Picha/ Further Africa.

Malengo ya maisha na uwezo wa kifedha

Ukubali ukatae fedha ina umuhimu mkubwa katika maisha ya ndoa ikiwawezesha wanandoa kumudu gharama za maisha na kupanga malengo katika siku za usoni.

Ustadhi Othuman anabainisha kuwa, tofauti kubwa za malengo na uwezo wa kifedha huleta migogoro isiyoisha, kwani kila mmoja hujaribu kuvuta ndoa upande wake.

Hata hivyo, mwanasaikolojia Chris Mauki anasema licha ya fedha kuwa muhimu sio msingi wa kila kitu katika ndoa akifafanua kuwa zinaweza kuchangia ndoa kuvunjika.

“Wengi wameumizwa na wengine kuvunjwa moyo kutokana na changamoto zihusuzo pesa kwenye mahusiano na ndoa… nikwambie tu ndoa inaweza kufanikiwa hata kama kukiwa na pesa ya kawaida,” anasema Mauki katika moja ya semina alizofanya jijini Dar es Salam mwaka 2024.

Unampenda

Askofu Anthony anafafanua kuwa aina ya upendo itakayokuingiza katika ndoa haitakiwi kuwa ile ya kuvutiwa na muonekano wa nje pekee, bali ni kukubali na kuvumilia hata madhaifu yake.

Kuna aina nyingi za upendo, lakini upendo unaohitajika kuanzisha familia ni ule wa wa kudumu, unaoambatana na uvumilivu na mshikamano.

“Kumpenda mtu ni kukubali madhaifu yake. Je, utayapenda hayo madhaifu? Kupenda si sura, bali ni kujali, kumlinda na kumtetea. Mtu asivutiwe na mambo ya nje, avutiwe na mambo ya ndani,” amesisitiza Askofu Anthony.

Kumfahamu mwenzi wako kwa undani kunasaidia kuelewa tabia, malezi na tamaduni zake. Picha/ Adobe stock.

Usawa wa kielimu

Akigusia suala la elimu, Askofu Anthony amesema kuwa usawa wa kielimu ni jambo muhimu katika kudumisha amani ya ndoa.

 Amefafanua kuwa tofauti kubwa za elimu kati ya wanandoa zinaweza kuleta changamoto katika mawasiliano, maamuzi na uelewa wa masuala ya kifamilia.

“Mfano mtu mwenye elimu ya darasa la nne anapooa au kuolewa na mtu mwenye elimu ya chuo kikuu, mara nyingi usawa wa fikra unakosekana, na migogoro huwa ya kudumu kwa sababu kiwango cha uelewa na mtazamo wa maisha hutofautiana sana,” amesema Askofu Anthony.

Pamoja na masuala hayo, kabla ya kukubali kuingia katika ndoa wataalamu wa saikolojia wanaeleza kuwa ni lazima uzingatie masuala ya afya ya akili pamoja na pamoja na afya ya mwili ili kuweza kuwa na ndoa yenye furaha na amani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks