Jinsi ya kutatua matatizo unayokutana nayo hotelini
- Yapo matatizo ya kawaida ambayo utakutana nayo ukiwa hotelini ikiwemo kukosa maji ya moto, mapokezi mabovu na hata kelele za majirani zako.
- Unatakiwa kuelewa aina ya tatizo kabla ya kulitatua ili usiharibu safari yako.
Wale wanaosafiri mara kwa mara na kukaa katika hoteli tofauti tofauti, lazima watakuwa wamekutana baadhi ya matatizo katika vyumba vya hoteli wanavyofikia.
Licha ya kuwa matatizo hayo yanatofautiana lakini yapo baadhi yanayofanana karibu kwa watu wote wanaotumia hoteli za ndani au nje ya nchi hususan nyingi zilizopo karibu na makazi ya watu.
Haya ni baadhi ya matatizo kama siyo changamoto na jinsi unavyoweza kuzikabili na kuzitatua ili kuhakikisha safari yako inakuwa ya mafanikio kama ulivyopanga.
Kelele za vyumba vya majirani
Moja tatizo ambalo utakutana nalo hotelini ni kelele za mtu ambaye umepakana naye chumba. Kelele hizi hutofautiana kutoka zile za kukoroma hadi za wanywaji pombe na wanaochelewa kurudi hotelini usiku.
Hii hutokea zaidi kama chumba chako kiko juu au madirisha yametazamana na chumba cha mwingine.
Hapa unaweza ukaongea na uongozi wa hoteli wakuhamishie kwenye vyumba vyenye utulivu kama havijachukuliwa na watu wengine. Lakini unaweza kutumia vifaa maalum (noise-canceling headphones or earplugs) vya kuzuia kelele ukiwa umelala.
Hotelini nyingi zinajitahidi kuweka mazingira tulivu katika vyumba lakini ufahamu kuwa kuna wakati huwa tofauti. Jiandae kukabiliana na kelele ambazo huenda zikatokea.
Kelele zinaweza kukukosesha usingizi. Unahitaji utulivu ukiwa hotelini ili kupata usingizi wa uhakika. Picha|Matandao.
Uchafu wa chumba
Pia uchafu kwenye vyumba vya hoteli ni changamoto nyingine hasa kwenye vyumba ambavyo havijatumika muda mrefu. Unaweza kukutana na wadudu kama mende na hata uvundo kwenye kitanda hasa kama cumba hakijatumika muda mrefu.
Unaweza kutoa malalamiko yako kwa uongozi wa hoteli na ukahamishiwa kwenye chumba kingine. Kwa sababu hoteli zinatofautina hadhi ni vema kabla ya kutafuta hoteli angalie ile inayokufaa ili kuepuka matatizo yasiyo ya lazima.
Ni muhimu kufahamu hiyo haitokei mara kwa mara, kwa sababu hoteli nyingi zinazingatia sana viwango vya usafi ili kuvutia wageni kufurahia huduma zao. Ikitokea ujulishe uongozi ili wachukue hatua stahiki.
Soma zaidi:
- Waziri Kanyasu ataka tathmini ifanyike ajira hoteli za kitalii Tanzania
- Hizi ndizo sababu kwanini hoteli zinatumia mashuka meupe
- Kwanini ukague chumba cha hoteli kabla hujaanza kutumia?
Upungufu wa vyumba
Kuna wakati mwingine hoteli hupokea idadi kubwa ya watu kuliko uwezo wake na kusababisha usumbufu kwa wageni hasa kama ratiba ya kuingia na kutoka hoteli haijazingatiwa.
Hili linaweza kukuta kwa hoteli ambazo hazina mfumo wa kielektroniki wa ‘booking. Muhimu unatakiwa uwe mtulivu, ongea na uongozi wa hoteli ili wafanye mpango wa kukutafutia hoteli nyingine. Kama itashindakana itakubidi kuingia gharama za ziada kujisitiri sehemu nyingine.
Kutokuwepo kwa maji ya moto
Kuwepo kwa maji moto hotelini kunaweza kusiwe hoja kubwa kwako kama unataka kuupoza mwili kwa maji ya kawaida, lakini kwa wengine ni tatizo kwao kwa sababu hawajazoea kuoga maji ya baridi.
Kutokana na changamoto za mifumo ya machemsho ya maji, unaweza kujikuta chumba chako hakina maji ya moto. Katika hali hii ufanye nini kama unayahitaji maji ya moto kwa ajili ya kuosha mwili?
Wakati mwingine inaweza isiwe tatizo la kupatikana kwa maji ya moto, bali ni kutokujua jinsi ya mifumo ya machemsho ya maji kwenye chumba chako. Omba msaada kwa wahudumu wa hoteli na kama hamna kabisa maji ya moto wanaweza kukutafutia namna nyingine ya kuyapata.
Maji ni huduma muhimu ya kijamii inayotakiwa kuwepo wakati wote ili kukidhi mahitaji ya watumiaji. Picha|Mtandao.
Lugha na mapokezi mabaya ya wahudumu
Baadhi ya wahudumu wa hoteli kutokana na changamoto mbalimbali katika kazi wanaweza kukutolea lugha ya kuudhi au wasikupokee vile unavyotaka. Hii inaweza kukuharibia siku yako na usijisikie vizuri wakati wa safari yako.
Ni vema usibishane nao, walipoti kwa uongozi wa hoteli kwamba hujapendezewa na huduma walizokupa ili kuangalia chanzo cha tatizo na jinsi ya kulimaza.
Safari yako itakuwa na mafanikio kama utatambua kuwa changano zipo na unapaswa kuzikabili kwa busara na hekima ili kuepusha matatizo zaidi wakati ukitimiza majukumu yako kule unakokwenda.
Latest
