Unavyoweza kukabiliana na kichefuchefu ukiwa safarini
- Unaweza kupata kichefuchefu na hata kutapika pale unapotumia usafiri wa ndege, meli na gari.
- Inasababishwa na kupishana kwa mawasiliano kati ya macho, masikio na ubongo.
- Unaweza kuepuka hali hiyo kwa kupumzika kabla ya safari na kusikiliza muziki.
Dar es Salaam. Ilikuwa ni takriban dakika 45 tangu nanga ya meli niliyokuwa nimepanda kutoka Zanzibar kwenda Dar es Salaam ing’olewe. Kwa tulipokuwa, meli ilikuwa imezungukwa na maji tu huku kukiwa hamna dalili ya ardhi yoyote inayoonekana.
Hata hivyo, ushwari uliokuwepo ulipotea ghafla na anga likaanza kuwa na mawingu meusi. Ni kama wahudumu walifahamu kinachoenda kutokea kwani walianza kugawa bahasha kwa ajili ya kutapikia na punde si punde bahasha zilianza kutumika.
Wakati nikiwaza kwa nini mimi bahasha yangu iko tupu na hakuna mabadiliko yoyote mwilini mwangu, kuna mama mmoja ambaye alikuwa umbali wa siti tano kushoto kwangu alikuwa tayari ametumia bahasha mbili.
Nikiwa nimekaa nilikuwa nahisi meli inapaa kidogo na kutua kwenye maji kwa kishindo. Kwa hali ilivyokuwa inaendelea, sikuhitaji kuambiwa nifunge mkanda kwani kilo zangu nazijua mwenyewe na kama nisingeshtuka huenda ningejikuta nimerushwa juu na kuacha siti yangu.
Mama yule sasa alikuwa ameshamaliza bahasha nne na aliendelea kuomba zingine. Nilimuonea huruma lakini alikuwa mbali kiasi cha kushindwa kumpa pole yangu. Hakuwa mjamzito, walau kwa muonekano.
Usipokuwa makini, badala ya kufurahia safari yako inaweza kuwa safari isiyosahaulika. Picha| Berkshire Hathaway.
Hali hiyo inasababishwa na nini?
Kwa mujibu wa tovuti ya masuala ya afya, Everyday Health hali hiyo kwa kitaalamu inaitwa “Motion sickness” ambayo hutokea pale mawasiliano kati ya macho, masikio na akili yanapotofautiana.
Kwa uelewa zaidi, Mkurugenzi wa masuala ya tiba kutoka kampuni ya Carnival Cruise Lines inayojishughulisha na usafiri wa majini, Dk John Bradberry ameelezea kuwa, unapokuwa kwenye meli, macho hayaoni mwendo hivyo yanaiambia akili kuwa haupo kwenye mwendo.
Hata hivyo, masikio yanahisi mwendo na yanapowasilisha ripoti hiyo kwa ubongo, unabaki njiapanda na hivyo wengine kuumwa kichwa, kuhisi kichefuchefu na dalili zingine za motion sickness.
Mbali na gari, treni na ndege, leo tutaangazia hali hii kwenye usafiri wa meli na boti.
Yafuatayo ni maujanja ya kukusadia kuepukana na hali hiyo:
Pata muda mwingi wa kupumzika kabla ya safari
Pale unapokuwa haujapumzika vya kutosha, unakuwa kwenye hatari zaidi ya kuhisi kichefuchefu na hata kutapika uwapo safarini. Kwa mujibu wa Daktari kutoka Kituo cha Afya cha Ahmadiyya kilichopo Mkoani Morogoro, Dk Joshua Sultan, kuwa na uchovu mwingi kabla ya safari inakuweka kwenye asilimia kubwa za hupatwa na kichefuchefu.
kupata siti ya dirisani uwapo kwenye boti inaweza kukusaidia kuepuka kichefuchefu kwakua unaweza kutama nje. Picha| Live and Lets fly.
Yaondolee macho yako udanganyifu
Awali nimekwambia kuwa macho yako yanaweza kudanganya akili yako kuwa haupo kwenye mwendo. Hivyo endapo unaruhusiwa kwenda kwenye kivaranda cha meli, unaweza kwenda huko na kuangalia mbele ili macho yajue kuwa unatembea na yapeleke ujumbe sahihi kwenye akili.
Pia inashauriwa kutokutazama skrini za simu na televisheni na hata kusoma vitabu kwani ni vyanzo vya macho kuona kuwa haupo kwenye mwendo.
“Badala ya kusoma kitabu kwa karibu au kuangalia filamu, unaweza kusikiliza muziki kwa kutumia earphones na kufumba macho, itakuepusha na kichefuchefu,” amesema Dk Sultan.
Mtaalamu huyo pia ameshauri usikilize kwa sauti ya chini ili linapotolewa tangazo ndani ya boti au meli usikie.
Epuka vichochezi vya kichefuchefu uwapo safarini
Kila mtu ana vichochezi vyake vya kichefuchefu. Wapo wanaopata vichefuchefu kwa harufu na wengine kuona vitu vitakavyowapatia kinyaa.
Hivyo ni muhimu pia kuchagua chombo kizuri cha usafiri ambacho hakina vichochezi vyako ikiwemo harufu za samaki na kadhalika.
Dk Sultan pia anashauri kutokuongelea kuhusu kutapika wala kuwaza kuhusu kutapika kwani na wewe unaweza kujikuta unaunga tela la wanaotapika.
“Pata siti ya dirishani ili usipate vishawishi vya kuangalia wenzio ambao wanaweza kuwa kwenye hali mbaya (kutapika),” ameshauri Dk Sultan.
Unapopanga safari kwenda sehemuutakayovuka maji, ni vyema kujiandaa. Picha| helen in Wonderlust.
Tafuta cha kutafuna
Kuacha tumbo lako tupu wakati wa safari sio kitu kizuri, inaweza kuwa sababu ya wewe kuhisi kichefuchefu.
Dk Sultan amesema unaweza kupata kitu cha kutafuna kulingana na kile unachomudu. Wapo wanaotafuna jojo, wengine humung’unya pipi huku wengine biskuti au vinywaji vikiwa suluhu.
“Kabla ya safari unaweza kunywa chai ya tangawizi. Imesaidia baadhi kuepuka kichefuchefu wakati wa safari,” ameshauri mtaalamu wa afya, Dk Sultan.
Fahamu
Motion Sickness sio ugonjwa ni changamoto tu ya mwili na haiwezi kuambukizwa. Mara nyingi huwapata wanawake wajawazito na watoto lakini mtu yeyote anaweza kufikiwa nayo.
Natumaini siku ukifungasha kwenda Zanzibar, Ukerewe, Mwanza na hata ughaibuni kwa meli una pa kuanzia.
Latest
