Jinsi ya kuchagua soketi nzuri ya umeme
- Kifaa hicho ni daraja kati ya umeme na vifaa vya kielektroniki na umeme vinavyotumia kwa shughuli mbalimbali.
- Unaponunua kifaa hicho hakikisha unazingatia matumizi na eneo utakapoenda kukiweka.
- Zingatia umaarufu na ubora wa kifaa hicho wakati wa manunuzi.
Dar es Salaam. Unawezaje kutumia friji yako bila kuwa na soketi nyumbani? Au kusaga juisi yako kama haujachomeka waya wake kwenye soketi?
Kifaa hicho kwa mujibu wa wataalamu walioongea na Nukta ni daraja kati ya umeme na vifaa vya kielektroniki na umeme vinavyotumia kwa shughuli mbalimbali.
Soketi huja kwa miundo mbalimbali zingine zikiwa na sehemu moja ya kuchomekea na zingine zikiwa na sehemu zaidi ya moja.
Hata hivyo, unahitaji kuzingatia baadhi ya mambo wakati unajipanga kununua bidhaa hiyo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba yako.
Nunua kifaa kipya
Fundi umeme, Damas Sambonanga ambaye anafanya shughuli zake Jijini Dar es Salaam anasema soketi bora ni ipya kwani iliyotumika huwezi kujua imetumika kwa muda gani.
Fundi huyo amesema vifaa hivyo vinapatikana kuanzia Sh5,000 na vinakuja na majina ya makampuni tofauti tofauti.
“Soketi za Tronic zinaanzia Sh6,500 hadi Sh7,000 kwa ambazo zina sehemu mbili za kuchomekea kifaa. Hauna sababu ya kununua kitu kilichotumika” ameeleza Sambonanga.
Zipo soketi ambazo zina sehemu ya kuchomekea waya wa simu na zipo za kawaida, ni wewe kuchagua kulingana na matumizi yako. Picha| Freepik.
Zingatia jina na umaarufu
Fundi Sambonanga amesema hakuna kinachovuma kwa bahati mbaya.
Kinachosababisha kitu kufahamika na kuongelewa na kila mtu ni ubora wake au ubaya wake. Hivyo kama kitukinasifika kwa uzuri ni muhimu kutokupuuza.
Hivyo ni muhimu kuhakikisha kuwa pale unapoenda kununua kifaa, hakikisha unaangalia kitu kinachofahamika na kusifika kwa uzuri endapo hauna ujuzi wa kifundi zaidi.
Mahitaji yako
Soketi zinakuja na muundo tofauti. Zipo ambazo zina hadi sehemu ya kuchomekea waya wa kuchajia simu huku zingine zikiwa na mifumo ambatanishi (zinaweza kuingia aina yeyote ya kichomekeo cha waya)
Kama unanunua soketi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, ni rahisi kutabiri vifaa vitakavyorandana na vifaa vya umeme unavyotumia nyumbani.
“Zipo soketi ambazo zina sehemu ya kuchomekea waya wa simu na zipo za kawaida, ni wewe kuchagua kulingana na matumizi yako,” amesema Sambonanga.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, uzuri wa bidhaa hizi ni kuwa haziharibiki kirahisi.
Zinazohusiana
- Zingatia haya unaponunua taa za nyumbani
- Unayoweza kufanya kudhibiti matumizi makubwa ya umeme nyumbani
- Usifanye makosa haya wakati wa kununua “blender”
Hata hivyo, inapotokea kifaa chako kimeharibika au kuungua baada ya kukichomeka kwenye soketi, usikimbilie kulaumu soketi kwani haiwezi kuunguza kifaa chako.
“Mara nyingi huwa ni kuzidi kwa umeme kutoka kwa mtoa huduma au kifaa chake unachokitumia kufanya kazi kwa muda mrefu bila kupumzika,” amesema mtaalam huyo na kubainisha kuwa vifaa vinavyotumia umeme mwingi kama mashine za kuchomelea ndiyo vinaweza kuharibu soketi endapo vitatumika kwa muda mrefu.
Yapo mengi ya kujifunza kutokana na vifaa vya umeme. Wiki ijayo, utajifunza mambo mengi kuhusu faida za mashine za maji ya kunywa almaarufu kama “water dispensor”.
Latest
