Huyu ndiye mrithi wa DPP Biswalo

May 15, 2021 12:23 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni Sylvester Mwakitalu ambaye ameteuliwa na Rais Samia kuwa DPP.
  • Anachukua nafasi ya Biswalo Mganga aliyeteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu.
  • Pia Rais amefanya teuzi za viongozi wengine wa taasisi za Serikali.

Dar es Salaam. Kitendawili kilichokuwa kinasubiriwa nani atarithi nafasi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Biswalo Mganga iliyoachwa wazi baada ya kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu kimeteguliwa leo na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua Sylvester Mwakitalu  kushika nafasi hiyo. 

Biswalo aliteuliwa kuwa Jaji Mei 11 mwaka huu baada ya kudumu katika nafasi ya DPP tangu mwaka 2014 alipoteuliwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete.

Kabla ya uteuzi huo, Mwakitalu ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi katika Ofisi ya Msajili wa Hazina na sasa atafanya kazi na Joseph Pande ambaye Rais Samia amemteua kuwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka (DDPP).

Pande anachukua nafasi ya Edson Makallo ambaye atapangiwa majukumu mengine.

Mbali na uteuzi huo wa DPP, Rais  amemteua Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Salum Hamduni kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) akichukua nafasi ya Brigedia Jenerali John Mbungo ambaye atapangiwa kazi nyingine.

Kabla ya uteuzi huo, Hamduni alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha.

“Aidha, Rais Samia amempandisha cheo ACP Hamduni kuwa Kamishna wa Polisi (CP),” imeeleza sehemu ya Taarifa iliyotolewa leo Mei 15, 2021 na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu.

Hamduni atafanya kazi kwa karibu na Neema Mwakalyelye ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru. 

Rais Samia katika taarifa hiyo ya uteuzi wa wakuu hao wa taasisi pamoja na wakuu wa mikoa, viongozi hao wataapishwa Mei 18, 2021 Ikulu, jijini Dar es Salaam.


Zinazohusiana


Pia ememteua Dk Edwin  Mhede kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) kuchukua  nafasi ya Ronald Lwakatale ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Dk Mhede aliwahi kuwa Kamishana Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kabla kuondolewa katika nafasi hiyo mara baada ya Rais Samia kuingia madarakani Machi mwaka huu. 

Aidha, Taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa inaeleza kuwa Nenelwa Mwihambi ameteuliwa kuwa Katibu wa Bunge  kuchukua nafasi ya Dk Stephen Kagaigai ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu  wa Mkoa wa Kilimanjaro.

“Amemteua Balozi Joseph Sokoine kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuchukua nafasi ya Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,” imeeleza taarifa hiyo.

Enable Notifications OK No thanks