inDrive yawanoa wanafunzi wa Tanzania katika Tehama
Washiriki wa mafunzo maalum ya Tehama yaliyoandaliwa na BeginIT, mradi wa kimataifa wa elimu ulioanzishwa na kampuni ya inDrive wakifanya majaribio ya teknolojia ya usafirishaji. Mafunzo hayo yamefanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam kama njia ya kuchochea ari ya watoto kupenda masomo ya sayansi. Picha | BeginIT.
- Mafunzo hayo ni hatua ya kuwawezesha kupata suluhu za matatizo ya sekta ya usafirishaji.
- Yametolewa na BeginIT, mradi wa kimataifa wa elimu ulioanzishwa na inDrive.
- Tanzania ni miongoni mwa nchi 15 zilizopata mafunzo hayo ya aina yake.
Dar es Salaam. Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi chache ambazo wanafunzi wake wa shule za msingi na sekondari wamefaidika na ujuzi na maarifa ya Tehama yaliyotolewa na kampuni ya teknolojia na usafirishaji ya inDrive ili kuwajengea uwezo wa kubuni njia bora za kutatua changamoto za usafirishaji nchini.
Mafunzo hayo ya siku moja yalitolewa kwa watoto wa makundi maalum na BeginIT, mradi wa kimataifa wa elimu ulioanzishwa na inDrive mwaka 2012 ili kuamsha shauku ya watoto kujifunza, ukuaji binafsi na kushawishi uchaguzi wa mzuri wa taaluma ya baadaye.
Wanafunzi 39 kutoka shule tatu za msingi za Kinondoni, Msisiri na Mkuti na Shule moja ya Sekondari ya Debribant waliletwa pamoja katika Shule Kuu ya Habari na Teknolojia ya Mawasiliano ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM) kujifunza namna wanavyoweza kuitumia na kufaidika na mstakabali wa teknolojia ya mjongeo duniani (the future of mobility).
Pia mafunzo hayo yaliyokuwa yakitolewa na wataalam wa Tehama yalilenga kuwaandaa wanafunzi hao na mstakabali wao na kuwapa ushauri wa kitaalam kuhusu teknolojia mpya katika sekta ya elimu ambazo zinaweza kuboresha maisha yao na jamii inayowazunguka.
Tanzania miongoni mwa nchi chache duniani
Ndani ya mwaka 2022, mradi huo ulilenga kuvifaidisha kimaarifa vituo 127 vya watoto yatima, makazi, na shule za vijijini katika chini 15 za Urusi, Kazakhstan, Brazili, Mexico, Colombia, Ecuador, Afrika Kusini, Tanzania, Kenya, Nigeria, Peru, Chile, Indonesia, India na Pakistan.
Wakati wa mafunzo hayo, wanafunzi walipata fursa ya kujadili, kuwasilisha mawazo na kazi zao bunifu zinazotoa suluhu za kiteknolojia kukidhi mahitaji ya jamii katika sekta ya usafirishaji.
Kaimu Mkuu wa Idara ya Tehama ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Mhandishi Eliud Kataraihya aliwaeleza wanafunzi hao kuwa zamani watu walilazimika kusubiri au kutafuta taxi mitaani ili kuwapeleka wanakotaka lakini kwa sasa kila kitu kinafanywa kutumia simu yako.
“Ukiwa na inDrive unaamua au mnaafikiana nauli, kipengele hiki ni cha kipekee kwenye soko. Unapoona vitu vinabadilika kwa uzuri, hii ina maana kuwa kuna watu wako nyuma wanaofanya kazi kwa bidii kuleta suluhu,” amesema Mhandisi Kataraihya.
Soma zaidi:
- WhatsApp inavyowabeba wajasiriamali Tanzania
- ‘Apps’ zinazoweza kuwasaidia wazazi katika malezi ya watoto
- App ya Tap2Eat yarahisisha upatikanaji wa chakula kwa wanafunzi shuleni
Watakiwa kutumia maarifa hayo kila siku
Amewataka wanafunzi hao kutumia maarifa hayo katika maisha yao ya kila siku kwa kuwa wabunifu na kuona kwa upana changamoto zilizopo kwenye jamii na namna wanavyoweza kutoa suluhu ili kuboresha maisha ya watu wanaowazunguka hasa katika sekta ya usafiri.
Wanafunzi hao 39 pia watatembelea kituo cha ufuatiliaji wa magari ya usafiri wa umma na kujionea jinsi LATRA inavyofuatilia mabasi ya mikoani yakiwa katika safari barabarani jambo linalolenga kuwahamasisha kuwa wabunifu zaidi na kutafuta suluhu ya matatizo yanayoizunguka jamii.
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa kampuni ya SwahiliSoft Technologies Limited, Khamis Pembe aliyekuwa mmoja wa wawezeshaji wa mafunzo hayo, ameishukuru BeginIT kwa kutekeleza programu hiyo inayowaandaa watoto wa Tanzania kuwa wabunifu hasa kutatua changamoto katika jamii zao bila kusubiri teknolojia za nje.
Wanafunzi 39 wakiwa pamoja na viongozi wa LATRA na kampuni ya SwahiliSoft Technologies Limited katika picha ya pamoja mara baada ya kuhitimisha mafunzo. Wanafunzi hao wamesisitizwa kuwa wabunifu na kubobea katika kutafuta suluhu zitakazosaidia kuboresha maisha ya watu kwenye jamii. Picha | BeginIT.
Ni mafunzo adimu kwa watoto
“Mpango wetu wa warsha umeendelezwa vizuri sana, shukrani nyingi kwa BeginIT kwa mpango huu unaolenga kukuza ukuaji wa kibinafsi wa watoto, kufanya teknolojia ya kusisimua na kupatikana kwa kila mtu bila kujali hali ya kijamii na kifedha, kuongoza na kushawishi uchaguzi wa kazi za baadaye,” amesema Pembe.
Pia shule ambazo wanafunzi wake wameshiriki katika mradi huo zitapata usaidizi wa kifedha kwa ajili ya kununua vifaa vya kiufundi vya madarasa ya kompyuta, kozi za programu na mafunzo ya ziada.
“Tunaamini kwamba BeginIT itasaidia sana kuleta hatma njema kwa washiriki na kati yao watatokea watayarishaji wapya wa programu wenye vipaji, wabunifu, wajasiriamali wa Tehama, wanasayansi na wawakilishi wengine wa uchumi mpya,” ameeleza Arsen Tomsky, Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa inDrive katika tovuti ya BeginIT.
Latest
