Vodacom, ACP kuziunganisha shule za Serikali kidijitali

February 9, 2022 8:55 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Wamezindua mradi wa kugawa kompyuta, tableti katika shule za vijijini.
  • Shule hizo pia zitapewa intaneti ya mwaka mzima.
  • Ni juhudi za kuipeleka Tanzania katika uchumi wa dunia.

Dar es Salaam. Taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation kwa kushirikiana na Taasisi ya African Child Projects (ACP) zimezindua upanuzi wa mradi wa uunganishwaji wa shule kidijitali katika shule ya Sekondari ya Mawenzi iliyopo Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Mradi huo unaolenga kuboresha elimu ya Tehama mashuleni, unatarajia kuunganisha shule 50 za uma zilizopo kwenye mikoa 10 nchini kwenye mtandao wa intaneti.

Shule hizo zitapokea jumla ya kompyuta 186, tableti 246 pamoja na vifurushi vya intaneti vya GB50 kila mwezi kwa mwaka mmoja.

Mradi huo ni juhudi za muendelezo wa Tanzania kuingia katika uchumi wa dunia hivyo kutekeleza mradi huo kwa kizazi kijacho ni njia sahihi.

“Tusikubali vijana wetu kukosa faida zinazotokana na mafunzo yanayotolewa kidijitali,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Sitholizwe Mdlalose anayeamini kuwa, elimu bora ni msingi wa kujenga jamii ya kidijitali.

Shule hizo zitapokea jumla ya kompyuta 186, tableti 246 pamoja na vifurushi vya intaneti vya GB50 kutoka vodacom kila mwezi kwa mwaka mmoja. Picha| Vodacom.

Juhudi hizo ni muendelezo wa shughuli za Vodacom katika kuboresha elimu kwa njia ya mtandao nchini. 

Mathalan, mfumo wa E-Fahamu ulioanzishwa na kampuni hiyo wenye gharama ya Sh1.7 bilioni hadi mwaka jana, umewezesha wanafunzi 81,500 nchini kupata mafunzo kwa kutumia intaneti.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema ni muhimu pale watu wanapowajibika katika utekelezaji wa sera za elimu, utafiti, huduma za maktaba, sayansi, teknolojia, ubunifu na uendelezaji wa mafunzo ya ufundi, wawe makini ili maendeleo yazifikie jamii za Watanzania zilizo mbali.

“Tunahitajika kila siku kuwa makini katika kuona na kutambua njia bora za kutoa na kufikisha huduma hii muhimu kwa jamii zetu, haswa kwa wale walio maeneo ya mbali vijijini,” amesema Prof Mkenda.


Soma zaidi


Pia, kwa kushirikiana na wadau wengine ukiwemo Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Vodacom imechangia kompyuta 1,400 na vifaa vya intaneti pamoja na kuunganisha shule za msingi na sekondari zilizoko kwenye maeneo ambayo yangeweza kusahaulika kwenye mtandao wa intaneti. 

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya ACP Catherine Kimambo amesema ahadi yake ni kuhakikisha mradi huo unatimizwa kwa ubora mkubwa kwani sababu ya kufanya hivyo ni imani ya kuwa “elimu ni msingi ambao vijana tunaweza kujenga kutimiza ndoto zetu za maisha.”

Aidha, mradi huo utachangia kutimiza malengo ya maendeleo endelevu (SDG’s) hasa lengo namba tisa linalolenga ‘kuongeza kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma za Tehama kwa gharama nafuu kwa nchi zinazoendelea’ na lengo la nne ambalo ni, ‘kuhakikisha usawa katika ubora na upatikanaji wa elimu ili kujenga mazingira endelevu ya kujifunza kwa wote.’

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...