App ya Tap2Eat yarahisisha upatikanaji wa chakula kwa wanafunzi shuleni

November 12, 2019 5:37 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Huko nchini Kenya, taasisi ya Food For Education au mlo kwa ajili ya elimu imebuni programu tumishi ya simu (App) ya Tap2Eat na kuleta  mapinduzi makubwa katika kuwezesha wanafunzi kupata chakula wakiwa shuleni. Picha| Tap2Eat.


  • Tap2Eat ni app ambayo inatumia teknolojia ya juu kuwezesha wanafunzi wa shule za msingi kupata lishe bora.
  • Wanafunzi huvalishwa bangili ya rangi ya chungwa ambapo kabla ya kula simu ya mkononi inaelekezwa kwenye bangili hiyo inasoma data na mtoto anapatiwa chakula.
  • Naibu Katibu Mkuu wa UN amesema teknolojia hiyo ni muhimu kuinua kiwango cha elimu Afrika. 

Dar es Salaam. Wakati wadau wa elimu nchini Tanzania wakiendelea kutafuta suluhisho la kuwapatia wanafunzi chakula shuleni, matumizi ya programu za simu yanaweza kusaidia kufikia azma hiyo. 

Huko nchini Kenya, taasisi ya Food For Education au mlo kwa ajili ya elimu imebuni programu tumishi ya simu (App) ya Tap2Eat na kuleta  mapinduzi makubwa katika kuwezesha wanafunzi kupata chakula wakiwa shuleni.

Tap2Eat ni app ambayo inatumia teknolojia ya juu kuwezesha wanafunzi wa shule za msingi kupata lishe bora.

Kupitia apu hiyo, wazazi wanalipa Sh15 za Kenya sawa na Sh337 za Tanzania kwa mlo ili kuwapatia watoto chakula wakiwa shuleni, jambo linalowasaidia kusoma vizuri na kupata maarifa yaliyokusudiwa. 

Juhudi kama hizo za kuwapatia watoto chakula shuleni zinaendelea nchini, lakini kama teknolojia ikitumiwa vizuri inaweza kurahisisha mchakato wa kuwapatia chakula wanafunzi wengi kwa wakati mmoja. 

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Amina Mohammed amesema, Wawira Njiru, ambaye ni muasisi wa shirika hilo la Food For Education pamoja na apu hiyo ya Tap2Eat na wadau wao ni mfano wa  jinsi  ya kuwapa watoto kipaumbele katika elimu.

Kwa mujibu wa taarifa ya UN, Mohammed jana alitembelea shule  ya msingi ya Ruiru iliyoko jijini Nairobi nchini Kenya na kushiriki katika tukio la kuwagawia wanafunzi mlo wa mchana.

Lengo la ziara hiyo pamoja na kuwagawia wanafunzi chakula, ilikuwa pia kushuhudia jinsi taasisi hiyo ilivyobuni app ya Tap2Eat na kuleta  mapinduzi makumbwa katika kuwezesha wanafunzi kupata mlo wakiwa shuleni.

“Tunafahamu kuwa pindi watoto wana njaa, hawawezi kusoma. Kudumaa na kudhoofu kwa mwili kunaathiri zaidi ya watoto milioni 200 kote duniani na hivyo kufanya vigumu sana kwa mtoto kuishi na kumakinika shuleni. Kubadili mwelekeo huu si jambo rahisi, tunahitaji hatua za kipekee zaidi,” amesema Mohammed.


Soma zaidi: 


Amesema Tap2Eat imeleta ujuzi wa kipekee kutoka sekta mbalimbali kwa muktadha wa malengo ya maendeleo endelevu (SDG’s) na mpango wa utekelezaji utokanao na mkutano wa kimataifa wa watu na maendeleo, (ICPD).

Mohammed ambaye ni raia wa Kenya amesema wadau hao kwa pamoja wanatekeleza malengo ya SDG’s, namba moja kuhusu kutokomeza umaskini, namba 2 la kutokomeza njaa, namba 3 la afya bora na namba 4 la elimu bora.

Watoto wanaonufaika na mpango huo wanakuwa wamevalishwa bangili ya rangi ya chungwa ambapo kabla ya kula simu ya mkononi inaelekezwa kwenye bangili hiyo inasoma data na mtoto anapatiwa chakula.

“Hivi sasa watoto 10,000 kila siku nchini Kenya wanapatiwa chakula, na kwa kupatia bangili hiyo siyo tu wao wananufaika bali pia wakulima wa eneo jirani ambako mazao yao ndio yanapikwa kuwa chakula na pia wapishi wa jirani ndio wanapikia watoto,” amesema Mohammed.

Amekumbusha kuwa anayepata mlo leo atamkwamua mtu mwingine kutoka kwenye njaa kesho yake na pia kusaidia kubadilisha dunia.

Kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa, kudumaa miongoni mwa watoto hugharimu bara la Afrika dola za Marekani bilioni 25 (takriban Sh57.6 trilioni) kila mwaka.

Enable Notifications OK No thanks