Ilala kinara uhalifu wa kifedha Tanzania

November 14, 2022 3:53 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Matukio mawili kati ya 10 ya uhalifu yanatokea katika mkoa huo wa kipolisi.
  • Ukisefu wa maadili, ajira wachangia uhalifu wa kifedha kushamili nchini.

Dar es Salaam. Licha ya makosa ya uhalifu wa kifedha kupungua Tanzania katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Mkoa wa kipolisi wa Ilala ndiyo kinara wa makosa hayo hasa yanayohusisha kughushi nyaraka ili kujipatia fedha isivyo halali.

Uhalifu wa kifedha unahusisha makosa mbalimbali ya kijipatia fedha kwa njia isiyo halali ikiwemo ya kugushi, noti bandia, wizi katika mabenki, mashirika ya umma, Serikali kuu/mitaa na vyama vya siasa. 

Baadhi ya makosa hayo yanashughulikiwa na Sheria ya Makosa ya Mtandaoni ya mwaka 2015. 

Kwa mujibu wa ripoti ya Takwimu za Uhalifu na Matukio ya Usalama Barabarani ya Januari hadi Desemba 2020, iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Jeshi la Polisi inaonyesha kuwa makosa  ya uhalifu wa kifedha yamepungua hadi 905 mwaka 2020 kutoka makosa 1,218  mwaka 2019.

Hiyo ni sawa na kusema makosa hayo yamepungua kwa asilimia 25.7 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

Licha ya makosa hayo ya kifedha kupungua, makosa  ya kughushi nyaraka bado yameendelea kuwa ya kiwango cha juu kuliko matukio mengine.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa mwaka 2020, makosa ya kughushi yalikuwa 744 sawa na asilimia 82.2 ya makosa yote ya kifedha au sawa na kusema matukio nane kati ya 10 ya kifedha yalikuwa ya kughushi.

Uhalifu wa kughushi unafuatiwa kwa mbali na noti bandia na wizi katika mashirika ya umma. 

Ripoti hiyo inayopatikana katika tovuti ya NBS inaeleza kuwa sababu ya kuwepo kwa makosa ya uhalifu wa kifedha ni watu kukabiliwa na hali duni ya kiuchumi, kukosa maadili, ukuaji wa miji na utandawazi.

“Umaskini, tofauti kubwa ya hali ya maisha kati ya walionacho na wasionacho, ukosefu wa ajira kwa vijana na tamaa ya mali,” inaeleza ripoti hiyo kuwa ni sababu zinazochangia hali hiyo.

Hata hivyo, ripoti hiyo haijaeleza kiasi cha fedha kilichohusishwa au kupotea katika makosa hayo 905 ya uhalifu wa kifedha.

Ilala kinara uhalifu wa kifedha

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Mkoa wa Kipolisi wa Ilala jijini Dar es Salaam ndiyo unaongoza kwa matukio ya kiwango cha juu cha uhalifu wa kifedha Tanzania.

Mwaka 2020, Ilala iliripoti makosa 163 sawa asilimia 18 ya makosa yote  yaliyoripotiwa nchini.

Mkoa wa kipolisi wa Tarime-Rorya mkoani Mara ndiyo mkoa ambao haukuripoti tukio hata moja la uhalifu wa kifedha.

Uhalifu wa kifedha siyo tu unasababisha hasara kwa watu na taasisi, lakini huwasababishia watu ulemavu, majeraha na hata vifo, jambo linalopinguza nguvu kazi ya Taifa na kuongeza utegemezi katika familia.

Hata hivyo, NBS imeeleza kuwa tangu mwaka 2016 idadi ya makosa ya uhalifu wa kifedha imekuwa ikipungua mfululizo, jambo linaloweza kuashiria kuwa kuna kazi kubwa ya wadau wa usalama wa raia na mali zao inafanyika kudhibiti makosa hayo.

Mathalan, mwaka 2016 kulikuwa na makosa 1,990 lakini mwaka uliofuata yakapungua hadi 1,640 kabla hayapungua zaidi hadi 1,303 mwaka 2018. Hali hiyo iliendelea hata katika miaka miwili iliyofuata ya 2019 na 2020.

Ikiwa mwenendo wa makosa ya uhalifu wa kifedha utaendelea katika mtitiriko huo, huenda katika miaka ijayo, Tanzania ikaweka historia ya kutokuwa na makosa hayo kabisa. 

Wakati uhalifu wa makosa ya kifedha ukipungua Tanzania, Idara ya Uchumi na Masuala ya Kijamii ya Umoja wa Mataifa (UN) imeeleza kuwa uhalifu wa kifedha hasa utakatishaji fedha bado unaitesa dunia, hivyo hatua zaidi zinatakiwa zichukuliwe ili kuunusuru uchumi wa mtu mmoja mmoja na Serikali. 


Soma zaidi: 


Nini kifanyike kupunguza uhalifu wa kifedha

Jeshi la Polisi na NBS wanasema ili kupunguza au kutokomeza kabisa matukio ya uhalifu wa kifedha, jamii hasa vijana wahamasishwe na kushirikishwa katika shughuli za ujasiriamali ili kujipatia kipato halali kuendesha maisha yao.

“Kuzishawishi taasisi za fedha kupunguza urasimu wa upatikanaji wa mikopo na kupunguza riba kubwa zinazotozwa kwa mikopo hiyo na kuwepo na mipango ya utoaji elimu kwa jamii hasa ya elimu ya ujasiriamali,” imependekeza ripoti hiyo.

Taasisi za umma na binafsi hasa zinazohusika na malezi ya watoto kuongeza kasi ya kusimamia maadili ya jamii na kuendelea kutoa elimu kwa wafanyakazi kufuata maadili ya kazi, kanuni, taratibu na sheria kwa kuzingatia viapo vyao.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni katika hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2022/23 amesema amani, utulivu na usalama ni muhimu katika maendeleo ya nchi kiuchumi, kijamii na kisiasa, hivyo lazima ulinzi wa raia na mali zao uendelee kuimarishwa. 

Amesema Jeshi la Polisi litaeendelea kuchukua hatua kubaini, kuzuia na kudhibiti uhalifu wa aina zote ukiwemo wa kifedha ili kuwawezesha wananchi kuendelea kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kijamii katika hali ya amani na utulivu.

“Katika mwaka 2022/2023 Jeshi la Polisi litaendelea kuwapatia mafunzo ya kuwajengea uwezo kiutendaji watumishi wake. Mafunzo hayo yatawawezesha kukabiliana na uhalifu wa aina zote,” amesema Mhandisi Masauni katika hotuba yake akiwa Bungeni jijini Dodoma.  

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...