Ripoti: Uhalifu makosa ya jinai waongezeka Tanzania
- Makosa ya maadili yaripotiwa zaidi
- Kujichukulia sheria mkononi, wivu wa mapenzi vyatajwa kama sababu
Dar es Salaam. Tanzania imeripoti ongezeko la matukio ya uhalifu wa jinai mwaka 2022 huku elimu kuhusu umuhimu wa kutoa taarifa pindi matukio ya uhalifu yanapotokea ikitajwa kama sababu ya ongezeko hilo.
Kosa la jinai ni tendo lolote ambalo limekatazwa kwa sheria, ambapo mtu yeyote akilitenda anakuwa ameikosea Jamhuri.
Katika makosa ya jinai, mlalamikaji anakuwa ni Jamhuri (Serikali), ikiwakilishwa na mwendesha mashitaka wa Serikali.
Taarifa ya Hali ya Uchumi ya mwaka 2022 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imebainisha kuwa makosa ya kijinai yaliyotolewa taarifa mwaka 2022 ni 54,123 ambayo yameongezeka kutoka 50,412 ya mwaka 2021.
Kwa mujibu wa NBS ongezeko hilo la asilimia 7 kwa makosa ya jinai yaliyoripotiwa, limechangiwa na ushirikishwaji wa wananchi kupitia vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na elimu kuhusu umuhimu wa kutoa taarifa pindi matukio ya kihalifu yanapotokea.
Hata hivyo, Wakili Maduhu William ambaye ni Afisa Programu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ameiambia Nukta Habari kuwa jamii na Serikali inapaswa kujikita kufikiri namna ya kuzuia matukio ya kihalifu kutokea zaidi ya kuripoti pekee.
“Kutoa taarifa ni matokeo ya tukio la uhalifu, jamii iwekeze kwenye kutoa elimu juu ya madhara ya kufanya vitendo vya uvunjifu wa sheria, na Serikali itengeneze mazingira wezeshi kuepusha watu kushawishika kufanya vitendo vya kihalifu, amesema William.
Mwaka 2022 ulishuhudia kiwango kikubwa cha makosa ya uhalifu, ikiwemo unyang’anyi wa kutumia silaha uliofanywa na kikundi cha uhalifu cha panya road jijini Dar es Salaam pamoja na baadhi ya maeneo ya mkoa wa Pwani.
Makosa ya maadili ya jamii yaongoza
Takwimu zinaonesha makosa ya maadili ndio yaliyoripotiwa zaidi katika kundi la makosa ya jinai, ambapo jumla ya makosa 21,238 yaliripotiwa.
Kwa mujibu wa William baadhi ya makosa yanayotafsirika kama ya jinai yaliyo katika kundi la maadili ya jamii ni pamoja na ubakaji, ulawiti pamoja na vitendo vya ngono kwa watu ambao ni ndugu wa damu.
Makosa mengine yaliyoripotiwa kwa kiwango kikubwa ni yale ya kuwania mali ambayo ni 20, 960 yakifuatiwa na makosa 11,118 dhidi ya binadamu na makosa ya uhalifu wa fedha ni 807.
Soma zaidi
-
“Panya Road” walivyoacha maumivu kwa wakazi wa Dar mwaka 2022
-
Samia ‘alipa makavu’ Jeshi la Polisi, alitaka kufanya mageuzi makubwa
Kwa upande mwingine, makosa madogo yaliyotolewa taarifa nayo yameongezeka kutoka makosa 493,850 mwaka 2021 hadi makosa 520,758 mwaka 2022.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Hamad Masauni alipokuwa akisoma Hotuba ya Bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2023/24 aliwaambia wabunge kuwa miongoni mwa sababu ya ongezeko la makosa makubwa ni watu kujichukulia sheria mkononi.
Sababu nyingine ni pamoja na wivu wa mapenzi, imani za kishirikina, migogoro ya ardhi na mirathi, mmomonyoko wa maadili na tamaa ya mapenzi.
Makosa ya ajali yapungua
Kwa mujibu wa ripoti hiyo matukio ya ajali yaliyotolewa taarifa yamepungua na kufikia 1,732 kutoka ajali 1876 zilizotokea mwaka 2021.
Ajali za barabarani ndio zimeripotiwa zaidi zikiwa na matukio 1,720 zikifuatiwa na matukio 11 ya ajali za majini na ajali moja ya angani ambapo watu 19 walipoteza maisha baada ya ndege ya Precision Air kuanguka Ziwa Victoria.
Serikali yajipanga kudhibiti uhalifu
Hata hivyo kwa mujibu wa Masauni Serikali inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu kuzingatia sheria, kuhamasisha jamii kutoa taarifa za makosa hayo kwa wakati kwa kushirikisha viongozi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, pamoja na na kushirikisha viongozi wa dini katika kutoa elimu ya maadili mema kwa jamii.
Latest