Mambo yatakayosaidia uraghbishi kustawi Tanzania
- Wananchi kuwa mstari wa mbele ili kujiletea maendeleo yao.
- Wanasiasa kutoelewa shughuli za uraghibishi kunakwamisha jitihada za maendeleo.
- Vyombo vya habari vyatakiwa kuwasaidia wananchi kupaza sauti.
Dar es Salaam. Wanasema siri ya mtungi aijuaye ni maji si kata tena na hivyo ndivyo waraghbishi hutumia sehemu ya muda wao kutambua na kutatua kiini cha changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo wanayofanyia kazi nchini.
Uraghbishi ni mtindo wa maisha wenye falsafa, mtazamo na namna ya kuwachochea wananchi washiriki kwa pamoja katika kujiletea maendeleo yao kwa kuwafundisha wanajamii kuibua changamoto walizonazo.
Japo wengi hufanya uraghbishi bila kutambua, shirika la Twaweza linashirikiana na mashirika ya kijamii na asasi za kiraia kuiboresha dhana hii kwa kuongeza ushiriki wa wananchi, kuboresha uwezo wa serikali za mitaa na kuimarisha upatikanaji wa huduma za jamii.
Hivi sasa ni Wilaya tano za Kigoma-Ujiji, Lindi, Maswa, Mbogwe na Pangani ambazo jitihada za uraghbishi zinaonekana kuzaa matunda kwa kuimarisha upatikanaji wa huduma za kijamii na kuamka kwa ari ya jamii kuchukua hatua za pamoja kutatua kero zinazowakabili.
“Wote tunafahamu kuwa kuna mpango wa fursa na vikwazo kwa ajili ya wananchi kuweza kuibua, ile mipango na malengo ni mizuri, lakini utekelezaji wake una changamoto kwenye uhalisia.
“Mambo mengi yanaukumba ule mchakato kama vipaumbele vya kiwilaya, kitaifa, kichama vina influence (shawishi) ule mchakato kiasi kwamba vipaumbele ambavyo vijiji vinaibua vinaakisi vipaumbele vya kitaifa ambavyo labda siyo vipaumbele vya wananchi,” anaeleza Richard Temu, Afisa Programu Mwandamizi wa Utafiti wa Twaweza.
Temu ameeleza hayo leo Oktoba 7, 2022 jijini Dar es Salaam katika mkutano uliowakutanisha waraghbishi zaidi ya 100 kutoka wilaya nane kujadili changamoto za kazi hiyo na namna ya kufanya kwa ufanisi.

Waraghabishi wakiwa kwenye mkutano uliowakutanisha kutoka maeneo mbalimbali nchini katika ukumbi wa APC Hotel& Conference Center wakijadili changamoto na mbinu na kuzitatua kwa pamoja.
Kibarua kilichopo mbele yao
Licha ya umuhimu wa waraghbishi, bado wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikitishia kazi zao.
Changamoto hizo ni pamoja na msukumo wa kisiasa na usalama, uhaba wa waraghbishi, uelewa mdogo kwa baadhi ya wanakamati za wananchi, uhaba wa vyombo vya usafiri na uelewa mdogo wa elimu ya uraghbishi kwa baadhi ya viongozi wa kata na vijiji.
Japo shughuli za uraghbishi zinafanywa na wanajamii kwa ajili ya wanajamii changamoto inayoonekana kukwamisha zaidi jitihada zao ni kukosa ushirikiano wa moja kwa moja kutoka kwa wanasiasa wanaoona kama waraghbishi huingilia majukumu yao kwa kujaribu kutatua kero za jamii.
“Nina mfano, mwaka huu tumefanya uraghbishi Maswa na tukawa tumealika madiwani, watu kutoka kijijini na waraghbishi, madiwani wakasema hiki kikao hatukitambui na katika maeneo yetu hatutaki kabisa kukisikia, wakapinga kabisa na wakawa wakali,” anasema Temu.
Mgongano wa kimaslahi kati ya wanasiasa na waraghbishi umefafanuliwa zaidi na Amisa Sahani anayetokea Wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu aliyeezea kuwa, “kwa kweli siasa na uraghbishi ni vitu viwili tofauti, vinagongana inatubidi tutumie mbinu, sisi kwanza tusiwe wanasiasa, pili inatakiwa kuwatongoza wanasiasa na kuwajenga kiakili waelewe kwamba sisi sio adui zao bali tunawasaidia katika kazi zao za kisiasa.”

Waraghibishi wakiwa kwenye majadiliano na Wanahabari kuhusiana na changamoto zinazowakabili
Mraghbishi kutoka Wilaya ya Maswa, Daniel Peter amesema uwezo wa kujenga urafiki, ushirikiano na ukaribu wake na viongozi wa kijiji na kata unamsaidia kutimiza wajibu wake.
“Tunagemea kiongozi apaze sauti kutoka kwa wananchi, lakini kwa sababu tumefika sehemu ambayo kiongozi anaona kama yeye ni mfalme ndiyo tunapokuja na waraghbishi na ataona ni watu ambao hawatakiwi,” amesema Peter.
Amesema lengo kubwa la uraghbishi ni kuirudisha uongozi wa vijiji kwa wananchi ili kuwawezesha kuamua kwa uwazi kuhusu maendeleo ya maeneo yao huku wakiongozwa na kiongozi anayewasikiliza.
Waraghbishi hao wamesema wao wana nia ya dhati ya kuona maeneo yao yanapata maendeleo kwa kuwaleta wananchi pamoja kuibua na kutatua kero zao bila kuisubiri Serikali.
Ili kutimiza jukumu hilo, wanashauri viongozi wa Serikali kuwapata ushirikiano ili kuhakikisha kunakuwa na uwajibikaji na uwazi katika matumizi ya rasilimali za nchi.
“Kuna umuhimu mkubwa wa vyombo vya habari kufahamu uraghbishi na shughuli za wananchi…wananchi wanapambana kujiletea maendeleo wenyewe. Wanafanya ufuatiliaji wa bajeti za maeneo yao na kuwajibisha watendaji, sauti zao zapaswa kusikilizwa,” amesema Annagrace Rwehumbiza, Mratibu wa Programu kutoka shirika la Tamasha.
Latest
