Ifahamu mikoa 5 yenye majengo mengi yasiyo na anwani za makazi

May 18, 2023 8:18 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na Dodoma, Dar es Salaam na Mwanza.
  • Migogoro ya ardhi yachangia baadhi ya majengo kukosa anwani hizo.
  • Serikali yasema zoezi la anwani za makazi ni endelevu, kila jengo litafikiwa.

Dar es Salaam. Huenda baadhi ya wakazi nchini wakashindwa au wakachelewa kupata huduma za kijamii, kiuchumi ikiwemo vifurushi kutokana na maeneo wanayoishi kukosa anwani za makazi.

Mwaka 2022 Serikali ya Tanzania ilianza rasmi zoezi la  uwekajii  wa anwani za makazi katika mikoa na wilaya zote nchini ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya Posta ya mwaka 2003.

Sera hiyo inaelekeza kuwepo kwa anwani za kitaifa zitakazowezesha ufikishaji wa barua, nyaraka, vifurushi na vipeto majumbani na katika ofisi mbalimbali.

Licha ya maelekezo ya sera hiyo, baadhi ya maeneo nchini bado hayajafikiwa na huduma hiyo. 

Ripoti ya matokeo ya mwanzo ya Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 iliyozinduliwa Aprili 15, 2023 inaeleza kuwa  Tanzania ina jumla ya majengo (makazi) milioni 14.3, kati ya hayo, majengo milioni 10.4 ndio yenye anwani za makazi.

Hiyo ni sawa na kusema majengo saba kati ya 10 nchini yana anwani za makazi. 

Ripoti hiyo imeeleza kuwa mpaka mwishoni mwa mwaka 2022, majengo milioni 3.5 yalikuwa hayana anwani za makazi, jambo ambalo linaweza kuwakosesha huduma muhimu wakazi katika majengo hayo.

Dodoma ndio mkoa ambao umetajwa kuwa na majengo mengi yasiyo na anwani za makazi nchini.

Ripoti hiyo iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaeleza kuwa Dodoma ambayo ndio makao makuu ya nchi ina makazi 305,837 yasiyo na anwani na makazi.

Majengo hayo yasiyo na anwani za makazi ni sawa na asilimia 36.5 ya majengo 836,909 yaliopo mkoani humo na asilimia 8.5 ya makazi yasiyo na anwani nchini.

Hii ni sawa na kusema zaidi ya theluthi moja ya makazi ya Dodoma hayana anuani za makazi. 

Anwani za makazi  zinaongeza kasi ya kupambana na uhalifu, kuimarisha shughuli za uhamiaji, utalii, ulinzi na usalama.Picha|Dar 24.

Dodoma inafuatiwa na Dar es Salaam kwa kuwa na majengo mengi ambayo hayajawekewa anwani za makazi.

Dar es Salaam ambalo ni jiji la kibiashara na viwanda lilikuwa na makazi 275,034 yasiyo na anwani hizo zinazorahishisha shughuli na kijamii na kibiashara.

Majengo hayo yasiyo na makazi jijini Dar es Salaam ni sawa na asilimia  30.1 ya makazi yote katika jiji hilo. Hiyo ni sawa kusema kwa kila majengo 10, majengo 3 hayana anwani za makazi.

Mikoa mingine yenye majengo mengi yasiyokuwa na anwani za makazi ni pamoja na Mwanza majengo 231,199, Morogoro (226,359) na Tabora yenye majengo 198,070. 

Wakati mikoa hiyo ikiwa na idadi kubwa ya majengo yasiyo na anwani za makazi, kwa baadhi ya mikoa watafaidi zaidi faida za anwani hizo kutokana na kuwa na majengo mengi yenye anwani.

Mikoa hiyo ni pamoja na kaskazini Pemba yenye majengo 57,058 yenye anwani za makazi sawa na asilimia 89.9, Mtwara (451,095) na Njombe 244,920.

Mingine ni Kusini Pemba yenye majengo 50,939, Kagera  yenye  majengo 598,332 yenye anwani hizo.


Soma zaidi


Kwanini mikoa hiyo ina anwani za makazi chache?

Afisa Mipango Miji wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Emanuel Richard akizungumza na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) anasema baadhi ya nyumba zimekosa anwani za makazi kutokana  na changamoto mbalimbali ikiwemo migogoro ya ardhi.

“Wakati ule zoezi hili linafanyika kuna baadhi ya  nyumba zilikuwa kwenye migogoro ya ardhi au kwenye maeneo hatarishi hivyo hazikupewa postcode (anwani za makazi),” anasema Richard.

Kwa kuwa anwani za makazi ni utambulisho wa kudumu afisa huyo anawashauri wakazi wa maeneo yenye migogoro ambayo hayakupata anwani hizo awali kuwasiliana na viongozi wao wa Serikali za mitaa baada ya migogro kuisha.

Zoezi la anwani za makazi ni endelevu

Serikali inasema zoezi la kugawa anwani za makazi ni endelevu, hivyo maeneo ambayo hayajafikiwa yatafikiwa na wananchi wanatakiwa kutoa ushirikiano. 

“Zoezi la postcode (anwani za makazi) mpaka leo bado linaendelea…Watendaji wa mitaa walipewa mafunzo kuzichambua nyumba ambazo hazina anwani hizo  na kuziingiza kwenye mfumo.

“Kwa Wananchi ambao hawakupata postcode (anwani za makazi) waende kwenye ofisi ya serikali za mitaa na nyumba zao zitapewa namba na kuingizwa kwenye mfumo wa anwani za makazi (NAPA),” anasema Richard.

Waziri wa Habari, Mawasiliano,Teknolojia ya Habari Nape Nnauye aliyekuwa akiwasilisha Bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2022/23 alisema Serikali imetenga Sh40 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi nchini. 

Pia Waziri huyo alisema Serikali itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu anuani za makazi ili zirahisishe utoaji wa huduma na kuharakisha maendeleo.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
PART 2: Yafahamu magari 10 yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta.

PART 2: Yafahamu magari 10 yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta.

Nukta TV

🔴LIVE: LIVE:WABUNGE WAKIWACHAPA MASWALI MAWAZIRI | Bunge la 13 | Kikao cha 28

🔴LIVE: LIVE:WABUNGE WAKIWACHAPA MASWALI MAWAZIRI | Bunge la 13 | Kikao cha 28

Nukta TV

PART 1: Yafahamu magari 10 yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta

PART 1: Yafahamu magari 10 yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta

Nukta TV