IFAD yawasaidia vijana kupunguza unene, kupata ajira
- Ni vijana wa nchi ya Tonga waliopewa mafunzi ya ufundi stadi.
- Wamefunzwa kupiga makasia na kutengeneza mitumbwi.
- Shughuli hizo zitawaidia kupunguza unene na kupata kipato.
Dar es Salaam. Kila tatizo lina suluhu yake ambayo ni fursa kwa watu kujiajiri na kujipatia kipato.
Tonga, taifa la visiwa vidogo lililoko katika bahari ya Pasifiki, vijana wanafundishwa stadi ya utengenezaji mitumbwi ikiwa ni njia mojawapo ya kujipatia kipato, kulinda mazingira na kupunguza unene uliopitiliza (utipwatipwa).
Tonga ni taifa lenye visiwa vidogo 170 na chakula si mazao yalimwayo nchini humo bali wakazi wake hutumia zaidi vyakula vilivyosindikwa na hivyo kusababisha kuwa moja ya nchi yenye watu wengi wenye unene uliopitiliza duniani.
“Tonga inakabiliwa na viwango vya juu kabisa vya lishe duni na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama unene kupita kiasi na mengi ambayo yanahusiana na ukosefu wa lishe bora.
“Eneo la ardhi ni dogo na limeathiriwa na maji ya chumvi, mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la idadi ya watu na kwa hivyo ni muhimu watu hapa kupata nafasi ya kwenda baharini kuvua samaki,” amesema Tawfiq El-Zabri, Mkurugenzi Mkazi wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) nchini humo.
Ili kunusuru vijana wa Tonga, IFAD imeanzisha mradi kwa kushirikiana na serikali pamoja na taasisi ya Mordi Tonga ili kutoa mafunzo stadi ya kutengeneza mitumbwi, wakufunzi wakiwa ni wazee.
Kupitia mafunzo hayo, vijana wanapata nyenzo za uvuvi, pili stadi za kupiga makasia zitawaweka kwenye afya njema kwani ni mazoezi, na tatu samaki watakaovua baharini watawasaidia si tu kupata kipato bali lishe bora.
“Kwa sasa watu lazima walipe fedha ili waweze kwenda baharini kwa kutumia boti. Lakini ukiwa na mtumbwi, kisha ukapata kifungua kinywa kizuri, hapo kijana atapata nguvu ya kutosha kupiga makasia siku nzima,” amesema Alipate Sailosi, mkufunzi na kiongozi wa jamii ya Eua wakati akiwahojiwa na radio ya Umoja wa Mataifa.
Mradi huo pia unakusudia kuwa hakikisho la upatikanaji wa chakula na kuwa chanzo cha kipato cha ziada kwa familia za Tonga.
Latest
