Fahamu fursa zilizojificha kwenye sekta ya uvuvi

July 10, 2023 7:44 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na ufugaji wa samaki na uchakataji wake.
  • Fursa hizo zinaweza kuwa chanzo cha ajira na kipato.

Dar es Salaam.Watu wengi wanaamini kuwa ili kutoboa kwenye masuala ya uvuvi ni lazima uingie ziwani au baharini kuvua au kuuza sokoni, la hasha. 

Sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa Taifa na pato la mtu mmoja mmoja ina fursa kibao ambazo baadhi hawazifahamu kiasi cha vijana kuipiga teke. 

Kwa mujibu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Tanzania Bara ina fursa nyingi katika ufugaji wa samaki ambazo bado hazijatumika kikamilifu. 

Fursa hizo zinachangiwa na uwepo wa maji (maji baridi na bahari), ardhi, mfumo wa kisheria unaounga mkono ufugaji wa samaki na hali ya hewa inayofaa.

 Jovina Kyaruzi ambaye ni mtaalamu wa uvuvi kutoka kampuni ya Nasha Acqua Fish iliyopo Mkuranga Mkoani Pwani ameiambia Nukta Habari kuwa mbali na kuvua samaki kuna fursa nyingine ikiwemo kutengeneza vifungashio na ukaushaji wa samaki.

“Kama si mpenzi wa ufugaji unaweza ukawekeza kwa namna nyingine, mfano unaweza kuanza na uchakataji ukasubiri wenzako wamefuga ukazichakata zile samaki, ukauza,”amesema mtaalamu huyo.

Katika uchakataji wa samaki ipo fursa ya kutengeneza vifungashio vya samaki, ukaushaji wa samaki, pamoja na ukaangaji na ugandishaji wa samaki kwenye majokofu kwa ajili ya matumizi ya baadae.

Mbali na fursa hiyo unaweza kuwekeza katika usafirishaji na usambazaji wa samaki ili kuwafikia wateja na walaji ndani na nje ya nchi. 


Soma zaidi


Ni chanzo cha ajira

Katika kipindi hiki ambacho katika nchi nyingi duniani kuna tatizo la ukosefu wa ajira, sekta ya uvuvi inaweza kuwa njia mbadala ya kujiajiri na kujipatia kipato.

Wizara ya Mifugo na Uvuvi, inabainisha kuwa mwaka 2020/2021, sekta hiyo imetoa ajira za moja kwa moja kwa wavuvi 194,804 na wakuzaji viumbe maji 31, 998.

Sambamba na hayo zaidi ya Watanzania milioni 4.5 wanapata mahitaji yao ya kila siku kutokana na shughuli zinazofanyika katika sekta hiyo ikiwemo kuunda na kutengeneza boti, kushona nyavu, biashara ya samaki na mazao ya uvuvi pamoja na Baba na Mama lishe. 

Kutokana na faida hizo Jovina anasema kampuni yao iliyoanzishwa mwaka 2017  imejikita kutoa mafunzo kwa vitendo zaidi ili kutoa fursa kwa vijana kupata maarifa yatakayowawezesha kujipatia kipato kupitia fursa hizo.

“Tunafundisha si kwa maneno tu bali hata kwa vitendo, tuna mabwawa kule mkuranga utajifunza na kujionea mambo yanaendaje,”ameongeza Jovina.

Kwanini uwekeze katika sekta ya uvuvi

Kuna sababu nyingi za kuwekeza katika sekta ya uvuvi ikiwemo uchache wa watu wanaofanya shughuli hiyo, kupungua kwa uzalishaji wa samaki  na kuongezeka kwa mahitaji ya kitoweo hicho.

Ripoti ya Sensa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya Mwaka wa Kilimo 2019/ 2020 inaonyesha kuwa  kaya zinazojishughulisha na shughuli hizo nchini Tanzania ni chini ya asilimia moja.

Hiyo ni sawa na kusema kati ya kaya zaidi ya milioni 12 zilizopo Tanzania ni kaya  120,078 au pungufu zaidi ya hizo zinayojishugulisha na uvuvi.

Aidha, kwa mujibu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi uzalishaji wa samaki nchini hususani samaki wanaofugwa ni mdogo.

Mwaka 2020/21 tani 18,717 za samaki wa kufugwa zilizalishwa, kiwango hicho ni chini ya asilimia nne ya jumla ya uzalishaji wa samaki.

Hivyo, juhudi za pamoja zinahitajika ili kuendeleza ufugaji wa samaki kwa kiwango kinachohitajika ili kuziba pengo kati ya mahitaji na usambazaji,” imesema taarifa ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Kwa upande wake Jovina mtaalamu wa uvuvi anasema kwa sasa kuna mahitaji mengi ya samaki ndani ya nchi na nje ya nchi hususani nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (Kongo DRC)

“Kwa uzoefu wangu nimeona zaidi samaki kama kambale aliyekaushwa ambaye nchi kama Uganda na Kongo wanahitajika sana na bei yake ni nzuri.

Kwa soko la ndani sato ana soko sana, kuna wakati tulikuwa tunaletewa samaki kutoka nchi za nje kutokana na uzalishaji wetu ulikuwa haujajitosheleza,” anasema Jovina.

/
No matches found for this filter
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
5 Jun, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
5 Jun, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Wabunge waliokwenda Morocco bila kibali kikaangoni , utoro ukiibuliwa bungeni

Wabunge waliokwenda Morocco bila kibali kikaangoni , utoro ukiibuliwa bungeni

Nukta TV

Mfahamu Leonard Mususa Alama ya Ungozi iliyoacha majonzi kwa 'MACEOs' Tanzania

Mfahamu Leonard Mususa Alama ya Ungozi iliyoacha majonzi kwa 'MACEOs' Tanzania

Nukta TV

Bei za mafuta mwezi Juni hizi hapa, dizeli ikipaa kwa Sh85

Bei za mafuta mwezi Juni hizi hapa, dizeli ikipaa kwa Sh85

Nukta TV