Jeshi la Polisi la Tanzania latangaza nafasi za ajira kwa vijana

March 21, 2025 10:37 am · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link

  • Ajira hizo ni kwa ajili ya waombaji wenye elimu ya kidato cha nne, kidato cha sita, na wahitimu wa shahada, stashahada na astashahada katika taaluma mbalimbali.

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi la Tanzania limetangaza nafasi za ajira kwa vijana wa Kitanzania wenye sifa stahiki, likiwataka kutuma maombi yao kupitia mfumo wa ajira wa jeshi hilo kabla ya tarehe 04 Aprili, 2025.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Inspekta Jenerali (IGP) Camillus Wambura Machi 20, 2025 nafasi hizo zinahusisha waombaji wenye elimu ya kidato cha nne, kidato cha sita na wahitimu wa shahada, stashahada na astashahada katika taaluma mbalimbali.

Miongoni mwa vigezo vilivyotajwa kwa waombaji ni kuwa na uraia wa Tanzania kwa kuzaliwa, afya njema kimwili na kiakili iliyothibitishwa na daktari, kutokuwa na kumbukumbu za uhalifu, kutokuwa na alama za kuchorwa mwilini (tatoo), na kutowahi kutumia madawa ya kulevya ya aina yeyote. 

Kwa mwombaji mwenye elimu ya sekondari anatakiwa awe amehitimu kidato cha nne au sita kuanzia mwaka 2019 hadi 2024. Huku wakitakiwa kuwa na umri kuanzia miaka 18 hadi 25 pamoja na wale wa Astashahada . 

Kwa mwombaji wa kidato cha nne anatakiwa kuwa na ufaulu wa daraja la kwanza mpaka la nne huku mwaombaji mwenye ufaulu wa daraja la nne akitakiwa kuwa na ufaulu wa alama 26 hadi 28.

Kwa mwombaji wa kidato cha sita anatakiwa awe na ufaulu wa daraja la kwanza mpaka la tatu huku wahitimu wa Shahada na Stashahada wakitakiwa kuwa na  umri kuanzia miaka 18 hadi 30.

Waombaji wote wanatakiwa kuwa na urefu usiopungua futi tano na inchi nane kwa upande wa wanaume, na futi tano inchi nne kwa wanawake. Pia awe na uwezo wa kuongea lugha ya Kiswahili na Kingereza kwa ufasaha. 

Mwombaji anatakiwa we hajaajiriwa au kuwai kuajiriwa na taasisi yoyote ya Serikali. Pia awe tayari kufanya kazi za Polisi mahali popote Tanzania. Awe tayari kujigharamia kifedha katika hatua zote za usaili endapo ataitwa.

Kwa upande wa wahitimu wa shahada, nafasi za ajira zinazopatokana ni kwa taaluma kama uhandisi bahari, Tehama, sheria, uchumi, na uhandisi wa Ndege.

Wahitimu wa stashahada taaluma zinazohitajika ni muziki, uuguzi, Tehama, afya ya wanyama, upigaji rangi wa magari, usanifu wa magari pamoja na useremala vikihitajika.

Utaratibu wa kutuma Maombi

Waombaji wote wanatakiwa waandike barua za maombi yao kwa mkono bila kusahau namba za simu na watumie anuani ya Mkuu wa Jeshi la Polisi S.L.P 961 DODOMA. Barua hiyo inatakiwa kuambatanishwa kwenye maombi ikiwa kwenye mfumo wa ‘pdf.

Waombaji wote wanatakiwa wafanye maombi yao kupitia kwenye mfumo wa Ajira wa Polisi kwa njia ya mtandao kupitia tovuti ya www.ajira.tpf.go.tz huku nyaraka muhimu kama barua ya maombi, nakala za vyeti vilivyothibitishwa, cheti cha kuzaliwa, na kitambulisho cha utaifa (NIDA) zikiambatanishwa.

Jeshi hilo limeonya kuwa maombi yatakayowasilishwa kwa barua pepe, posta au kwa mkono hayatapokelewa, huku hatua za kisheria zikitarajiwa kuchukuliwa kwa wale watakaowasilisha nyaraka za kughushi au taarifa za uongo.

Hata hivyo, jeshi hilo halijabainisha idadi ya nafasi za ajira zilizotolewa kwa ajili ya vijana Wakitanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks