Huduma za ziada zinazochochea ongezeko la wateja mgahawani, baa

August 10, 2018 4:35 pm · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Intaneti ya bure inavutia na kuwaweka wateja wako kwa muda mrefu katika eneo lako la biashara.
  • Usisahau kusajili eneo lako la biashara katika Google Maps ili usaidie watu kulifikia kwa haraka.
  • Vipi kuhusu kuchaji simu? Usisahau kuweka angalau soketi moja kila meza kunusuru wateja kuishiwa chaji.

Kwa wasanifu wazoefu wa majengo na sehemu za biashara za chakula, burudani na starehe ni kawaida kuzingatia mambo muhimu yanayotakiwa kitaalamu kama nafasi ya kutosha kwa wateja, usalama na mandhari ya kuvutia.
Hata hivyo, kadri mabadiliko ya teknolojia yanavyokua kwa kasi mahitaji ya maeneo ya biashara yanahitaji zaidi ya usanifu wa kuvutia kwa macho.
Katika ulimwengu wa dijitali ambao watu wengi wanatumia simu janja kuwasiliana na kusafu mtandaoni wakati mwingi hata wakiwa baa au mgahawani kuna huduma za msingi ambazo kwa sasa hutakiwi kuziacha katika usanifu wa eneo lako la biashara.

Intaneti ya bure na ya uhakika

Maeneo yenye intaneti ya bure yamekuwa kivutio cha watu wengi hususan vijana kwenda kupata huduma. Baadhi ya wamiliki wa migahawa, baa na hoteli wanaweka intaneti ya bure kupitia Wi-fi kama kivutio na huduma ya ziada kwa wateja wao. Intaneti inafanya wateja watumie muda mrefu kupata huduma kwako huku wakinunua zaidi vinywaji au chakula.

Utafiti wa faida za intaneti katika maeneo ya biashara uliofanywa na kampuni ya Device Scape ya Marekani katika biashara ndogondogo 400 ulibaini kuwa asilimia 62 au wafanyabiashara sita kwa kila 10 waliohojiwa waliripoti kuwa wateja walitumia muda mwingi katika maduka yao tangu walipoanza kutoa huduma ya bure ya intaneti.

Mbali na kutumia muda zaidi, utafiti huo uliofanywa mwaka 2014 unaeleza kuwa takriban nusu ya wafanyabiahara (asilimia 50) waliohojiwa walisema kuwa wateja wao walitumia fedha nyingi zaidi baada ya kuanza kutumia intaneti ya bure. 

Kwa sasa kuna modem za Wi-Fi ambazo zinaweza kuwaunganisha watu hadi zaidi ya 10. Jambo la msingi ni kuangalia kiwango cha kifurushi unachotakiwa kujiunga kila siku na iwapo inakulipa kufanya hivyo. Ni vyema ukatumia vifurushi vya bei rahisi kupitia promosheni na mtandao wenye kasi zaidi ili kuhakikisha huduma haikwami.

Katika kutoa huduma hiyo, usisahau kuweka nywila ili kuhakikisha wanaounganishwa ni wale tu wanaopata huduma katika biashara yako. Pia, hakikisha unaweka udhibiti wa kiasi cha kupakua mafaili mtandaoni ili baadhi ya wateja wako wasiishie kupakua movie nzima kupitia Wi-fi.

Hata Bajaj zina Wi-Fi siku hizi, jiongeze. Mmoja wa madereva wa Bajaj zenye intaneti ya bure jijini Dar es Salaam. Picha|AyoTV.


Zinazohusiana: Mbinu zinazoweza kuwasaidia wajasiriamali kunufaika na fursa zinazowazunguka

                          StraightBook: Mwokozi wa wajasiriamali asiyefahamika


Eneo la kuchajia simu

Watu wanaotumia zaidi simu janja katika kupiga soga au kufanya kazi kupitia intaneti hawakawii pia kuishiwa chaji kwa haraka katika simu zao. Kwa mantiki hiyo huduma ya intaneti yapaswa kwenda sanjari na uwepo wa soketi za kuchajia simu.

Ubunifu uliopo katika maeneo mengi ya biashara kwa sasa, ni kuweka chini ya meza angalau soketi mbili au katika ukuta uliopo karibu kwa kila meza. Hii inafanya watu wazichaji simu zao wakiwa katika meza wanazopata chakula au kinywaji bila ya hofu ya usalama wa vifaa vyao vya kielektroniki.

Kama ilivyo katika udhibiti wa matumizi ya intaneti, katika huduma ya kuchaji simu hakikisha pia anayechaji ni miongoni mwa watu waliohudumiwa. Wahudumu wanapaswa kuwa makini kwa kuwa baadhi ya watu watageuza  eneo lako la biashara kuwa kijiwe na kuishia kukuingiza hasara ya kununua Luku.
Simu zikichajiwa katika stesheni maalum ya kuchajia katika mgahawa. Upatikanaji wa huduma ya uhakika ya kuchaji simu unaongeza wateja katika biashara yako. Picha|DHgate.com.

Hakikisha umejisajili kwenye ramani

Kwa sasa watu wengi wanatafuta huduma kupitia mtandao hususan katika program za ramani kama Google Maps ambayo hutoa uelekeo husika, gharama za huduma na muda wa utoaji huduma.

Watumiaji wa huduma za usafiri kama Uber na Taxify nao hutumia maeneo yaliyopo kwenye ramani ili wafike vyema waendako. Kwa mantiki hiyo, ukiisajili biashara yako katika Google Maps unaongeza wigo mkubwa wa kupata wateja kutokana na urahisi wa kufikika.  Uwepo wa biashara yako kwenye ramani hiyo unasaidia wateja kuitafuta katika mtandao na hata kuwasaidia kufika bila kupotea.

Katika ulimwengu wa teknolojia, wateja wengi wanahitaji ufanisi na uharaka wa upatikanaji wa huduma husika. Huduma za intaneti na kuchaji simu zinazidi kuwa huduma muhimu kwa sasa nchini na wafanyabiashara hawana budi kuziingiza kama vivutio mojawapo kwa wateja wao. Siyo lazima tu kwenye migahawa na baa, huduma hizi zinaweza pia kuwekwa hadi katika Bajaji, mabasi na taxi.

Nuzulack Dausen ni Mhariri Mkuu wa Nukta aliyekita zaidi katika habari za Biashara, Uchumi, Teknolojia, na takwimu. Mtumie ujumbe kupitia ndausen@nukta.co.tz au kupitia Twitter: @nuzulack 

Enable Notifications OK No thanks