Hifadhi ya Taifa ya Gombe: Eneo ambalo Sokwe mtu amefanyiwa utafiti zaidi ya miaka 40

September 22, 2018 12:57 pm · Daniel
Share
Tweet
Copy Link
  • Ina ukubwa wa kilometa za mraba 52 tu ikiwa ni Hifadhi ya Taifa ya pili kwa udogo  hapa nchini.
  • Umaarufu wake ni uwepo wa wanyama jamii ya Sokwe mtu.

Dar es salaam. Ina ukubwa wa kilometa za mraba 52 tu ikiwa ni Hifadhi ya Taifa ya pili kwa udogo  hapa nchini lakini imekuwa kivutio kikubwa duniani kwa sababu ya  kuwa na idadi kubwa ya wanyama jamii ya Sokwe.

Inapatikana Magharibi mwa mkoa wa Kigoma ikiwa ni umbali wa kilometa 16 kutoka mji wa Kigoma Ujiji.

Thamani ya Gombe ilianza kuonekana mwaka 1940 pale ilipoanza kama Pori la Akiba la wanyama pori. Hifadhi hii ulianzishwa mwaka wa 1968, na shughuli za kitalii zilianza mwaka 1978.

Lakini huwezi kuzungumzia Hifadhi za Taifa za Gombe, pamoja na ile ya Milima ya Mahale, bila kutaja jina la Dk. Jane Goodall, ambaye ametumia miaka zaidi ya 40 katika kutafiti maisha na tabia za sokwe ambao wanapatikana katika Hifadhi hizo.

Alifika Tanzania wakati huo ikijulikana kama Tanganyika Julai 1960, ikiwa na umri wa miaka 26. Alisafiri kutoka Uingereza mpaka hifadhi ya Gombe, eneo ambalo leo linajulikana kama nyumbani kwa sokwe mtu. Tangu wakati huo amewekeza muda wake mwingi katika kutafiti maisha ya Sokwe.

Katika kutambua jitihada zake, Serikali ilimpatia tuzo Dk. Jane Goodall, kutokana na mchango mkubwa alioutoa katika kuthamini, kulinda na kuendeleza vizazi vya Sokwe. 

Gombe iko katika ukanda mwembamba wa misitu, milima na miteremko mikali inayoingia katika mwambao wa Mashariki wa Ziwa Tanganyika.  


Zinazohusiana:


Gombe ni miongoni mwa makazi machache yaliyosalia ya sokwe duniani. Sokwe hao ni wale wa jamii ya Kasakela, ambao taarifa zake zinapatikana katika vitabu na hati kadhaa, huishi katika Hifadhi ya Taifa ya Gombe.

Wanyama wengine wanaopatikana katika hifadhi hiyo ni pamoja na kima wenye mikia myekundu na kima wa bluu, pongo, nguruwe pori, fungo, tembo na pundamilia. Lakini wanyama jamii ya paka kama chui na simba hawapo katika hifadhi hii na hivyo kuifanya kuwa salama kwa safari za miguu.

Ukiachilia wanyama na vivutio vingine, hifadhi hiyo ni makazi ya ndege zaidi ya aina 200 sambamba na maporomoko ya maji ya Kakombe na Mkenke .

Wakati mzuri wa kutembelea hifadhi hii ni wakati wa kiangazi, Julai hadi Oktoba kwa sababu sokwe hawapendi kutembea nyakati za mvua.  

Inafikika kwa njia mbalimbali kulingana na bajeti yako ikiwemo ndege kutoka Dar es salaam au Arusha, pia kwa njia ya treni kutoka Dar es salaam mpaka Kigoma na kwa njia ya maji kutoka ziwa Tanganyika kutokea Burundi na Zambia.

Hifadhi ya Taifa ya Gombe imekuwa ni nyumbani kwa Sokwe watu ambao idadi yao inapungua kila mwaka. Picha| Azaniapost

Enable Notifications OK No thanks