HESLB: Wanafunzi vyuo vikuu kupata mikopo kabla ya Juni Mosi
- Helsb wameanza kupanga mikopo na wanafunzi watapata kabla ya kurudi vyuoni.
- Rais Magufuli aagiza vyuo vifunguliwe Juni mosi mwaka huu.
- Vilifungwa Machi, 2020 kuepuka maambikizi ya virusi vya Corona.
Dar es Salaam. Bodi ya mikopo ya elimu ya juu Tanzania (HESLB) imesema wanafunzi wa vyuo vikuu wataingiziwa mikopo yao ikiwemo fedha za malazi na chakula kabla ya vyuo kufunguliwa tena Juni mosi mwaka huu.
Hatua hiyo ya Heslb inakuja muda mfupi baada ya Rais John Magufuli kuagiza leo kuwa vyuo vyote vilivyofungwa Machi vifunguliwe Juni 1, 2020 kwa sababu maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya Corona yamepungua kwa kiasi kikubwa.
Dk Magufuli amezitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Wizara ya Fedha na Mipango kujiandaa vema ikiwemo kuwapatia wanafunzi mikopo kwa wakati na kutatua kwa haraka changamoto zote kabla ya vyuo havijafunguliwa.
Mkurugenzi wa Elimu na Mawasiliano wa bodi hiyo, Omega Ngole ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa wameanza kufanyia kazi maelekezo ya Rais Magufuli na wizara ya elimu.
“Tumeanza kuandaa malipo na wanafunzi watapata fedha zao kabla ya Juni 1 ambapo vyuo vitakuwa vinafunguliwa,” amesema Ngole.
Amesema timu ya Heslb imeanza kufanya malipo yenye thamani ya Sh63.7 bilioni za chakula na malazi kwa ajili ya robo ya tatu ya mwaka 2019/2020 huku Sh59.1 bilion ni kwa ajili ya ada za wanafunzi wanufaika ambazo zitalipwa kwa taasisi zaidi ya 70 za elimu ya juu zilizopo nchini.
Zinazohusiana
- Waombaji 10,452 Heslb wapewa siku nne kurekebisha kasoro
- Heslb yaanika kozi zitakazopewa kipaumbele mikopo elimu ya juu 2019-2020
- TCU yaanika sifa za wanafunzi kujiunga vyuo vikuu Tanzania
Mikopo hiyo kwa mujibu wa Ngole inajumuisha fedha za malazi na chakula kwa ajili ya wanafunzi kujikimu wakiwa vyuoni ambazo hulipwa kwa awamu nne kila baada ya siku 60.
“Wanafunzi waliingia vyuoni Novemba mwaka jana na walifunga Machi mwaka huu (kwa sababu ya Corona), tayari tuliwalipa fedha za awamu mbili na sasa watapata za awamu ya tatu,” amesema Ngole.
Katika mwaka wa fedha wa 2019/2020, Serikali imetenga Sh450 bilioni kwa ajili ya wanafunzi 132,119 wa elimu ya juu, ikiwa imeongezeka kutoka Sh427 bilioni zilizotengwa mwaka uliopita.
Wakati vyuo vikifunguliwa Juni mosi, Rais Magufuli ameagiza wanafunzi kuendelea kuchukua tahadhari zinazopendekezwa na wataalamu wa afya kwa sababu Corona bado ipo.
“Lengo la malipo haya ni kuziwezesha taasisi za elimu kumudu gharama za uendeshaji na hivyo kutoa elimu inayokusudiwa kwa wanafunzi wanaosoma katika taasisi zao,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru leo jijini Dar es Salaam.
Latest
