Hatma ya Lissu Novemba 6, Jamhuri ikisema akitiwa hatiani si lazima kifo

September 29, 2026 8:24 pm · Method Allen
Share
Tweet
Copy Link

  • Hukumu hiyo kutoka kwa jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu itaamua iwapo kiongozi huyo wa upinzani ana hatia au la.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania imepanga kutoa hukumu ya kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu Novemba 6, 2026, huku upande wa mashtaka ukieleza kuwa iwapo atakutwa na hatia ya uhaini si lazima ahukumiwe adhabu ya kifo. 

Hatua hiyo inafuata baada ya kukamilika kwa ushahidi na utoaji mawasilisho ya mwisho kutoka pande zote mbili katika kesi hiyo inayofuatiliwa kwa kina ndani na nje ya nchi. 

Lissu, kiongozi wa juu wa chama kikuu cha upinzani nchini, imekuwa mahabusu kwa zaidi ya siku 538 baada ya kukamatwa Aprili 9, 2026 mkoani Ruvuma na kisha kusafirishwa hadi Dar es salaam alipofunguliwa mashtaka hayo ya uhaini siku moja baadaye. 

Kesi yake ilianza kusikilizwa Mahakama Kuu masjala ndogo ya Dar es Salaam Septemba 2025 baada ya kumalizika kwa taratibu za awali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa kuwa mahakama hiyo ya chini haikuwa na uwezo wa kusikiliza shauri hilo.

Baada ya kukamilika kwa majumuisho ya mwisho yaliyotolewa na upande wa Jamhuri leo Septemba 29, Kiongozi wa jopo la majaji watatu wanaosikiliza kesi hiyo Jaji Dastani Ndunguru amesema kutokana na unyeti wa shauri hilo mahakama inahitaji muda wa kutafakari ushahidi huo neno kwa neno na mstari kwa mstari kabla ya kutoa hukumu Novemba 6, 2026. 

Akiwasilisha hoja za mwisho mahakamani leo, Wakili Mkuu wa Serikali Nassoro Katuga amesema ushahidi uliotolewa na mashahidi 17 wa Jamhuri, ukichangiwa na maelezo ya mshitakiwa mwenyewe, unaonyesha wazi kuwa kauli za “kukinukisha”, “kuhamasisha uasi” na “kuzuia uchaguzi” zililenga kuitishia Serikali na kuvuruga amani ya nchi.

Katuga ameiambia mahakama kuwa hakuna utata kwamba Lissu aliyatamka maneno hayo mnamo Aprili 3, 2025, kwani hata ushahidi wa mashahidi watano wa utetezi na maelezo ya mshitakiwa mwenyewe yamethibitisha kutolewa kwa kauli hizo. Lissu alihitimisha majumuisho yake ya mwisho Septemba 28, 2026 baada ya yeye na mashahidi wake wanne kukamilisha ushahidi. 

Katuga ameiambia mahakama kuwa mshitakiwa mwenyewe alitoa ushahidi bora zaidi dhidi yake pale aliposema “kwani tukikinukisha wataniua, si kwamba watanikamata na kunifungulia kesi ya uhaini”.

“Mshitakiwa alifanya hivyo akiamini anachokifanya kinaweza kumletea mashitaka ya uhaini. Hii ni nia ya dhati kabisa (pure reasonable intention). Ni kitu gani tena kitakachoizuia mahakama kutambua nia ya uhaini aliyonayo mtuhumiwa?” amedai Katuga.

‘Akikutwa na hatia si lazima ahukumiwe adhabu ya kifo‘

Licha ya kuwa jamhuri ndiyo inayomshtaki Lissu, Katuga amesema iwapo Mahakama itamkuta mshtakiwa na hatia katika shtaka la uhaini, adhabu inayotolewa haimaanishi moja kwa moja kuwa ni adhabu ya kifo, akisisitiza kuwa Mahakama ina mamlaka ya kutumia busara yake katika kuamua adhabu kulingana na mazingira ya kosa.

Katuga amesema adhabu katika shtaka hilo inaanzia kiwango cha chini hadi kiwango cha juu kinachoruhusiwa na sheria, huku adhabu ya kifo ikiwa ndiyo kiwango cha juu (maximum penalty).

Katuga ameiambia mahakama kuwa hakuna utata kwamba Lissu aliyatamka maneno hayo mnamo Aprili 3, 2025, kwani hata ushahidi wa mashahidi watano wa utetezi na maelezo ya mshitakiwa mwenyewe yamethibitisha kutolewa kwa kauli hizo. Lissu alihitimisha majumuisho yake ya mwisho Septemba 28, 2026 | Picha Method Allen.

“Mahakama yenu ina utashi wake wa kuamua adhabu, endapo mshtakiwa atatiwa hatiani, si lazima iwe adhabu ya kifo. Inategemea na aina ya kitendo ulichokitenda,” amesema. 

Ikumbukwe kuwa kesi ya uhaini namba 19605/2025 inayomkabili Tundu Lissu ni ya tatu katika historia ya Tanzania, huku ikiwa ni ya kwanza kwa kusimamiwa na sheria na Kanuni za adhabu kifungu cha 39 (2) (d).

Lissu, ambaye ni mkosoaji mkubwa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, anashtakiwa kwa kosa la uhaini kinyume na Sheria ya Kanuni ya Adhabu iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2023 linalotokana na tuhuma za matamshi aliyoyatoa Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam ya kutoshiriki na kuzuia Uchaguzi Mkuu 2025. 

Chadema na baadhi ya wanaharakati wemekuwa wakiikosoa kesi hiyo wakidai ni ya kisiasa na miongoni mwa mbinu za kupunguza nguvu wapinzani katika kudai mabadiliko ya kidemokrasia. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
29 Sep, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
29 Sep, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
29 Sep, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Fidia yakwamisha wakazi 27 Kigogo kuhama mabondeni, ‘El Nino’ ikikaribia

Fidia yakwamisha wakazi 27 Kigogo kuhama mabondeni, ‘El Nino’ ikikaribia

Nukta TV

Haya ndio maeneo ghali zaidi kuishi Dar es Salaam

Haya ndio maeneo ghali zaidi kuishi Dar es Salaam

Nukta TV

Fahamu athari za matumizi ya feni, kiyoyozi kiafya.

Fahamu athari za matumizi ya feni, kiyoyozi kiafya.

Nukta TV