Hatari inayowakabili wanaotumia vilainishi kama mbadala wa kondomu Tanzania
- Wataalamu wa afya wasema matumizi ya vilainishi yanaweza kusababisha magonjwa sugu ikiwemo UTI na fangasi kwa mwanamke.
Arusha. Kondomu ni miongoni mwa nyenzo muhimu zinazotumika kuwakinga watumiaji na mimba zisizotarajiwa na magonjwa ikiwemo ya ngono.
Tangu kuanza kwa matumizi ya nyenzo hiyo mamilioni ya watumiaji wamekuwa wakikingwa na hatari mbalimbali za kiafya na kuwafanya waendelee kuwa na afya njema.
Licha ya umuhimu wa nyenzo hiyo, takwimu za Wizara ya Afya zilizotolewa hivi karibuni zimebaini kupungua kwa matumizi yeke suala linalowaweka watumiaji hao katika hatari ya kupata magonjwa mbalimbali ikiwemo Virusi vya Ukimwi (VVU).
Dk Boniface Silvan aliyekuwa akimuwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali katika maadhimisho ya siku ya kondomu duniani yaliyofanyika jijini Dodoma Februari 14, 2025 alisema idadi ya matumizi hayo imeshuka nchini na kufikia milioni 73.
“Katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2025, jumla ya kondomu za kiume 72,875,900 zenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 6.93 zilisambazwa bila malipo, pamoja na kondomu za kike 180,500 zenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 284. “amesema Dk Silvan.

Mafuta ya kupaka mwili/kupikia yana kemikali zinazoweza kuharibu bakteria wazuri katika via vya uzaizi vya mwanamke na kusababisha magonjwa.Picha/Healthline.
Wakati matumizi ya kondomu au ‘zana’ kama zinazofahamika kwa vijana wengi yakiendelea kushuka nchini, baadhi ya watumiaji wamehamia katika matumizi ya vilainishi ikiwemo mafuta ya kupaka mwilini kama mbadala wa kutumia kondomu.
Dk Lameck Swax kutoka Sumbawanga ameiambia Nukta habari kuwa sababu kubwa ya kuongezeka kwa matumizi ya vilainishi hivyo ni kupungua kwa hofu ya Ugonjwa wa Ukimwi na uwepo wa dawa za kufubaza virusi vya ugonjwa huo kwa wingi.
“Watu wamechukulia kawaida ugonjwa wa ukimwi, sababu ya kupatikana kwa dawa za kuimarisha kinga za mwili na dawa nyingine mbadala kwa mfano PrEP (dawa ya kujikinga na maambukizi ya VVU kabla ya kuambukizwa),” amesema Dk Swax.

Kondomu pia inaweza kutumika kama njia ya uzazi wa mpango,Picha\ Healthline.
Ni hatari illiyojificha
Dk Joseph Clemence kutoka Hospitali ya Mtumba mkoani Dodoma ameiambia Nukta habari kuwa vilainishi haviwezi kuwa mbadala wa kondomu kwa sababu kondomu imetengezwa na kemikali maalum inayozuia magonjwa
“Kondomu imetengenezwa na latex material ambayo yanasaidia kuzuia maambukizi yoyote ya ngono, mafuta yana kemikali ambazo zinaua bakteria kinga wanaopatikana kwenye via vya uzazi husuani vya wanawake,” amebainisha Dk Clemence,
DK Clemence amebainisha kuwa mafuta yanapotumika ukeni yanasababisha mwanamke kutoka maji mengi ambayo yanaongeza msuguano unaoweza kuwa chanzo cha VVU na mengineyo yakiwaathiri wanawake na wanaume kwa pamoja.
“Kemikali nyingi zinakuja kuharibu mfumo wa misuli kwenye uume, kwa mwanamke ajiandae kuua bakteria wazuri wanaoishi ukeni ajiandae kupata magonjwa nyemelezi hasa fangasi na UTI sugu,” amefafanua Dk Clemence.
Latest