Fahamu madhara ya usugu wa dawa (Uvida)

November 24, 2025 6:08 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kuchangia vifo milioni 5 bkila mwaka duniani.
  • Wizara ya Afya imeitaka jamii kufuata maagizo ya wataalamu wa afya kila wanapoandikiwa dawa. 

Dar es Salaam. Kila siku mamia ya watu duniani hupoteza maisha kutokana na maambukizi ambayo miaka ya nyuma  yalikuwa yakitibika kwa urahisi kupitia dawa zinazotoolewa na wahudumu wa afya.

Sababu kuu ya vifo hivyo ni matumizi holela ya dawa yanayosababishwa na usugu wa vimelea dhidi ya dawa (Uvida) changamoto inayofanya maradhi ya kawaida kuwa hatari kubwa inayotishia maisha, kimya kimya.

Kwa mujibu wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (Africa CDC), Uvida hutokea pale dawa zinazotumika kuua vimelea vya ugonjwa zinaposhindwa kufanya kazi kutokana na vimelea kuwa sugu dhidi ya nguvu ya dawa hizo. 

Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa Uvida unasababisha vifo vya moja kwa moja zaidi ya milioni 1.3 duniani huku ikichangia vifo milioni 5 kila mwaka.

Mbali na athari za kiafya, tatizo hili linatishia pia uchumi wa dunia ambapo inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2030, gharama za tatizo hili kimataifa zinatarajiwa kufikia hadi Dola  za Marekani trilioni 3.4 (sawa na takriban Sh9,860 trilioni).

Uvida hutokea kadri muda unavyopita pale vijidudu kama vile bakteria, virusi na vimelea vinapojibadilisha na kuzoea uwepo wa dawa zilizobuniwa ili kupambana na hali hiyo. Picha /BioMérieux. 

Madhara ya Uvida kwa afya ya binadamu

Katika mahojiano na Nukta Habari, Mfamasia kutoka Sudan Kusini anayehudumu nchini India, Dk Akolk Manyuat Anei Akoldit, anabainisha kuwa athari za Uvida ni nyingi na nzito.

Akoldit amebainisha kuwa miongoni mwa madhara ya Uvida ni pamoja na kushindwa kwa matibabu hasa kwa maambukizi ya magonjwa kama vile nimonia, maambukizi ya njia ya mkojo (UTI), kifua kikuu na kisonono yanakuwa magumu au hata kutotibika.

“Dawa za mwanzo za matumizi (first-line drugs) hushindwa kufanya kazi, na mgonjwa huhitaji dawa kali zaidi, zenye sumu zaidi au zenye gharama kubwa,” ameelza Dk Akoldit.

Madhara mengine ni kuongezeka kwa ukali wa magonjwa na hatari ya vifo, pamoja na hatari kubwa wakati wa upasuaji au taratibu nyingine za kitabibu ikiwemo kupandikiza viungo, tiba ya mionzi (chemotherapy) na upasuaji wa kujifungua.

Naye, mtaalamu wa magonjwa ya binadamu kutoka Dar es Salaam, Dk Dinnah Nyirenda anaeleza kuwa usugu wa vimelea dhidi ya dawa unaweza ukaongeza wingi wa siku za mtu kukaa hospitali na usambaji wa magonjwa na kuongeza hatari zaidi ya kupata matatizo makubwa na mwisho kusababisha vifo. 

Aidha, Usugu huo unaweza pia kuongeza muda wa kuugua na kutibiwa, ugonjwa kusambaa sehemu nyingine zaidi ya ile ambayo mgonjwa alianza kuumwa. 

Nyirenda amesisitiza kuwa usugu wa vimelea vya magonjwa unaweza ukasababisha utasa na maambukizi ya magonjwa hatarishi ikiwemo ukimwi.

Wiki ya uhamasishaji kuhusu Uvida

Wiki ya kuongeza uelewa kuhusu usugu wa vimelea duniani huadhimishwa kila mwaka kuanzia Novemba 18 hadi 24, ikiwa na lengo la kuelimisha jamii kuhusu matumizi sahihi ya dawa tangu kugunduliwa kwa antibiotiki karibu karne moja iliyopita.

Katika kuhitimisha maadhimisho hayo, Wizara ya Afya imeitaka jamii kufuata maagizo ya wataalamu wa afya kila wanapoandikiwa dawa. 

Wamekumbusha kuwa mgonjwa hapaswi kusitisha kutumia dawa kabla ya muda uliopangwa, hata kama anajisikia nafuu, kwa kuwa kufanya hivyo kunachochea kuzalishwa kwa vimelea sugu. 

“Antibiotiki hazitibu maambukizi yanayosababishwa na virusi kama vile mafua,” imeeleza sehemu ya taarifa ya Wizara ya Afya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks