Mila, desturi zilizopitwa wakati, sababu ongezeko la VVU Mwanza

December 1, 2023 12:25 pm · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Zatajwa kuwa chanzo cha Mkoa wa Mwanza kuwa na maambukizi mengi
  • Waviu waonywa kutoacha kunywa dawa za kufubaza makali.
  • Utoaji elimu na uwazi kwa wanandoa wasisitizwa.

Mwanza. Mila na desturi zilizopitwa na wakati ikiwemo wanaume kutotahiriwa  zimetajwa kuwa sababu zinazochangia ongezeko la maambukizi ya virusi vya ukimwi hususani jijini Mwanza.

Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Seny’i Nganga aliyekuwa akisoma taarifa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla kwenye maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani leo Disemba mosi 2023, amebainisha kuwa mila hizo ni miongoni mwa sababu zinazochangia Mkoa wa Mwanza kuwa na maambukizi ya juu nchini.

Kwa mujibu wa Nganga takwimu za mwaka 2016/17 zinaonyesha Mkoa wa Mwanza umerekodi maambukizi ya mapya kwa asilimia 7.2 ambayo yako juu kuliko ya kitaifa ambayo ni asilimia 4.2

“Asilimia kubwa ya waviu ni wanawake na hii ni kutokana na maumbile yao lakini pia mila na tamaduni ambapo wanaume wengi hawajatahiriwa hali inayosababisha kupata na kusambaza maambukizi hayo kwa haraka,”amesema Nganga.


Soma zaidi : Hatari inayowakabili wauzaji, watumiaji mafuta ya vibaba Mwanza


Ngaga ameongeza kuwa licha ya kuwa bado jamii imeng’ang’ania mila za kizamani baadhi ya wanaume wameendelea kupuuzia matumizi ya kinga (kondomu) wakati wa tendo la ndoa jambo ambalo ni hatari kwa kuwa husababisha kuenea kwa maambukizi ya magonjwa ikiwemo ya zinaa.

Takwimu rasmi zinabainisha kuwa jumla ya watu 378,399 walipima Virusi vya Ukimwi jijini Mwanza katika kipindi cha Januari hadi Novemba 2023, ambapo watu 11,763 walibainika kuwa na VVU.

” Katika takwimu hizo wanawake 7,478 walibainikakuwa na virusi vya ukimwi,” amesema Nganga.

Mbali na ongezeko hilo, changamoto nyingine iliyobainika ni kwa ni wagonjwa wa Ukimwi kuacha kutumia dawa za kufubaza VVU hasa katika wilaya ya Sengerema na Ukerewe.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa, kiwango cha kufubaza VVU kinaendelea kukua ambapo kwa sasa ni wastani asilimia 78% ikilinganishwa na asilimia 52% iliyokuwepo kulingana na utafiti wa mwaka 2016/17.


Soma zaidi : Faida, hatari za uzazi njia ya upasuaji kwa wanawake Tanzania


Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, kuacha kutumia dawa za kufubaza makali ya VVU kunaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo, kupungukiwa kinga kwa kasi, kupata magonjwa yaambukizwayo kwa haraka ikiwemo kifua kikuu na wakati mwingine kifo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa watu wanaoishi na Ukimwi jijini Mwanza, Daudi Fabian amesema elimu ya kujitambua inapaswa kuendelea kutolewa ili waathirika wasijifiche pale wanapobainika na waanze kutumia dawa mara moja.

Aidha, Elisha Fabian ambaye ni mmoja wa Waviu wilayani Sengerema amewashauri wanandoa kutoficha siri iwapo kati yao atabainika na ugonjwa huo hali itakayosaidia kupunguza maambukizi mapya lakini kupeana ushauri na kukumbushana muda wa kumeza dawa.

Enable Notifications OK No thanks