Gharama zinavyokwamisha matumizi ya nishati safi ya kupikia shuleni

March 19, 2022 10:22 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Kuunganisha mifumo ya nishati safi mashuleni inahitaji mamilioni.
  • Kwa kuwa kuni zipo karibu na ni bure, shule zinaamua kuendelea nazo.
  • Wadau washauri matumizi ya teknolojia banifu kuokoa misitu wilayani humo.

Pwani. Licha ya nishati jadidifu ikiwemo umemejua kuwa suluhu ya uharibifu wa mazingira, gharama za upatikanaji wa nishati hiyo imezifanya baadhi ya taasisi za elimu katika Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani kuendelea kutumia kuni na mkaa. 

Matumizi ya kuni na mkaa yanatajwa na wadau wa mazingira kuwa yanachochea ukataji wa miti na hivyo kuzidisha athari za mabadiliko ya tabianchi na afya za watu.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Kilangalanga iliyopo Kibaha, Albert Mabiki amesema, licha ya walimu na wadau wengine wa elimu kujua madhara ya matumizi ya kuni shuleni, hawana namna kwa sababu nishati hizo zinapatikana kwa urahisi. 

Mkuu huyo wa shule ameiambia Nukta Habari (nukta.co.tz) kuwa, aliwahi kufanya upembuzi yakinifu pamoja na kampuni moja ili kuunganishwa na nishati ya gesi lakini gharama zilikuwa juu ambapo zilikuwa Sh31 milioni.

“Tuliangalia tukaona kwa kweli fedha hiyo hatuna. Gesi tunaipenda lakini hatuwezi kuimudu walau kwa gharama za mwanzo,” amesema Mwalimu Mabiki.

Licha ya shule nyingi za wilaya hiyo kuunganishwa na umeme wa gridi hazitumii umeme huo kwa shughuli za kupikia ili kupunguza gharama za nishati hiyo ambayo inatajwa kuwa safi na salama. 

Viongozi na wajasiriamali wa Kibaha wakionyeshwa baadhi ya teknolojia rafiki za kupikia katika taasisi. Picha| Rodgers George.

Wadau waliokutana kwenye Kongamano la Nishati lililoandaliwa na Mtandao wa Jinsia na Nishati tanzania (Tangsen) wilayani humo wamesema umeme wa gridi hautabiriki na shule nyingi zipo vijijini ambako wasambazaji wa gesi hawafiki.

Jambo hilo linawachelewesha kuhamia katika matumizi ya nishati jadidifu na kuacha mbadala mmoja tu, matumizi ya kuni.

Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Kibaha mkoa wa Pwani, Grace Mhagama amesema wilaya hiyo ina shule 63 za sekondari na msingi. Kati ya hizo, ni shule 38 tu ndiyo zimefikiwa na nishati ya umeme sawa na asilimia 60 ya taasisi hizo.

Ili shule hizo zisizo na umeme zipate nishati ya kupikia zinatakiwa ziwekeza pesa za kutosha katika nishati jadidifu ambayo ina mchango mkubwa katika utunzaji wa mazingira hasa kupunguza ukataji wa miti.

Mhandisi wa umeme kutoka Tanesco, Joseph Mbunju amesema kukatika kwa umeme kunasababishwa na sababu mbalimbali ikiwemo kuingiliwa kwa miundombinu ya Tanesco kunakofanywa na shughuli za binadamu au mazingira.

Mambo kama ajali za barababrani, miti kuanguka na shughuli za kibinadamu ni vigumu kupambana nayo na hivyo uhakika wa umeme bila kukatika unakuwa mdogo.

“Tunakarabati miundombinu yetu ikiwemo kwa kuweka nguzo za zege ili kukabiliana na changamoto ya nguzo kuanguka,” amesema Mhandisi huyo.


Soma zaidi


Ruzuku habado hazijafika jikoni

Wadau wa elimu waliohudhuria kongamano hilo wamesema licha ya uwepo wa ruzuku kwa ajili ya kuboresha miundombinu shuleni, ruzuku hiyo haijazingatia kuboresha miundombinu ya kupikia chakula.

Afisa Elimu vifaa na Takwimu kwa shule za sekondari wa Kibaha, Mukiza Kato amesema pesa kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule inatolewa lakini katika fedha hiyo, hakuna maainisho ya kiasi gani kichangie katika kuboresha miundombinu ya jikoni.

“Tunapewa pesa ya ruzuku kwa ajili ya madarasa, maktaba na miundombinu mingine ya shule lakini hakuna fedha inayoingia kwa ajili ya kuboresha miundombonu ya jikoni ikiwemo kutumia nishati safi,” amesema Kato.

Mdau huyo wa elimu amesehauri, maboresho ya shule yanaweza kwenda sambamba na maboresho ya nishati inayotumika kuandaa chakula cha wanafunzi shuleni kwani itasaidia kuongeza ufanisi katika upishi lakini pia kuokoa mazingira.

Wataalamu wa nishati ya umemejua wakitoa elimu kwa wananchi na viongozi wa Kibaha. Picha| Rodgers George.

Suluhu hii hapa

Baadhi ya wadau waliohudhuria kongamano hilo, wamesema safari ya kuinusuru misitu ya wilayani humo inaweza kuanza na kuelimisha wananchi kutumia nishati mbadala kama umeme jua, biogesi na vifaa banifu vinavyopunguza matumizi ya kuni na mkaa.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Envotech, Sylvester Mwambije amesema zipo baadhi ya teknolojia rahisi zilizoboreshwa ili kuminya matumizi makubwa ya kuni na mkaa.

Mtaalamu  huyo amesema, yapo majiko yanayofaa taasisi, migahawa na hata kwa matumizi ya familia ambayo yanauzwa kwa bei nafuu.

“Kama kutumia gesi ni gharama, tunaweza anza kuiokoa misitu yetu kwa kupunguza kiwango cha kuni zinazotumika. Kuna majiko yanaweza kupika chakula kwa kiasi kidogo sana cha kuni,” amesema Mwambije.

Kongamano la nishati Wilaya ya Kibaha ni mwendelezo wa jitihada za kupunguza matumizi ya kuni na nishati isiyofaa na kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala pamoja na umeme katika shughuli za uzalishaji na nyumbani.

Meneja Miradi kutoka Tangsen, Thabit Mikidadi amesema kuwa juhudi za elimu ziende sambamba na kufundisha kwa mifano ili watu waelewe na kuzifahamu nishati jadidifu.

“Wadau wanaotoa huduma hizi wapo na halmashauri zinatoa mikopo ambayo inaweza kuwasaidia wananchi kuingia kwenye matumizi ya nishati jadidifu. Cha msingi ni Watanzania wazione na wafikiwe na hizo teknolojia,” amesema Mikidadi.

Mdau huyo wa jinsia na nishati ametoa wito kwa kampuni zinazoshughulika na nishati mbadala kuzifikia taasisi za elimu na kuonyesha bidhaa zao kwani wapo wenye nia wanaoweza kununua, kukopa na hata kuchanga ili kuzipata ziwainue katika maendeleo yao.

Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Kibaha, Grace Mhagama amesema kwa sasa matumizi ya nishati muhimu katika utunzaji wa mazingira na Serikali imekuwa ikichagiza hasa katika maeneo ambayo hayajafikiwa na gridi ya Taifa.

“Kwa sehemu ambazo bado hazijafikiwa na umeme wa gridi, wadau wa nishati mbadala ndio hawa hapa, wanaweza kutusaidia kufikisha nishati hizo kwa Wananchi wakati serikali ikifanya juhudi ya kufikisha umeme wa gridi,” amesema Mhagama.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW