Nishati jadidifu itakavyowainua kiuchumi wanawake Pwani

Rodgers George 0447Hrs   Agosti 23, 2021 Teknolojia
  • Ni wale wanaojihusisha na ufugaji kuku wa kisasa wilayani Mkuranga.
  • Washauriwa kutumia umemejua na biogesi wakati wakisubiri umeme wa gridi.
  • Nishati hiyo itawasaidia kuongeza uzalishaji na kupata faida.

Dar es Salaam. Ni asubuhi ya saa tano, mama huyu akichakarika na shughuli zake za ufugaji ambazo ni sehemu ya maisha yake ya kila siku.

Akiwa ameshamaliza kufagia uwanja wa kuku anaowafuga, mamia ya ndege hao wanazunguka huku na kule wengine midomo yao ikidonoa ardhini wakitafuta chakula huku wengine wakiwa kwenye madumu ya maji wakipoza kiu.

Ni Lucy Liukutu, mwana kikundi cha wanawake cha Muungano kilichopo kata ya Kimanzichana, Wilaya ya Mkuranga mkoani pwani, kinachojishughulisha na ufugaji wa kuku na biashara ya mayai.

Lucy ambaye ni katibu wa kikundi hicho anasema mradi wao una kuku wa kisasa zaidi ya 300 na umewasaidia kujipatia kipato cha kujikimu kimaisha.

Hata hivyo, wanashindwa kufaidika ipasavyo na mradi huo kutokana na kukosa nishati ya umeme kuendesha shughuli zao ikiwemo kutotolesha mayai. 

“Tuna mashine hii ya kutotoreshea mayai. Inatumia umeme. Mashine ya kusaga chakula cha kuku tunayo tayari  lakini haifanyi kazi kutokana na ukosefu wa nishati ya umeme inayoweza kuiendesha,” anasema Lucy.

Ili wapate umeme wa gridi zinatakiwa kusimikwa nguzo sita zinazotakiwa kufika katika eneo mradi wao.

Wasipopata umeme kwa wakati huenda mashine hizo na vifaa vingine vya ufugaji walivyosaidiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga na Kituo cha Mapadri cha Benedict cha Kanisa la Katoliki kilichopo wilayani humo zikaharibika na kuzorotesha juhudi zao za kujikwamua kiuchumi.

Mtandao wa umeme wa gridi bado hujafika katika eneo lao na hivyo kulazimika kufuga kuku hao kwa njia za kienyeji ambazo Lucy na wenzake wanaamini hazitawapa mafanikio wanayokusudiwa.

Licha ya kuwa tayari wana taa za umemejua lakini hawajaweza kuunganisha umeme huo na mashine zao kwa sababu hazina mfumo wa kutumia aina hiyo ya nishati.


Sehemu ya banda la kikundi cha Muungano ambalo hutumika kufuga kuku. Picha: Thabit Mikidadi/ Tangsen.

Gharama watakazoziepuka kwa kupata umeme

Mwenyekiti wa kikundi hicho, Halima Mandai ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa kila mwezi wanatumia Sh480,000 kwa ajili ya kununua chakula cha kuku, jambo ambalo mashine zingekuwa zinafanya wangeweza kutengeneza wenyewe na kupunguza gharama za uendeshaji mradi.

“Kwa siku (kuku) wanatumia chakula kilo 30. Huwa tunanunua viroba 10 vyenye gharama ya Sh420,000 kila baada ya wiki mbili,” anasema Halima.

Kwa sasa, kikundi hicho kinategemea biashara ya mayai tu kama chanzo cha kipato cha kuendeshea mradi wao ikiwemo kununua chakula na dawa kwa ajili ya mifugo yao.

“Kwa sasa tuna uwezo wa kukusanya trei mbili na nusu za mayai kila siku. Huwa tunauza trei moja kwa Sh10,000,” aanaema Halima na kuwawezesha kupata ya Sh60,000 kwa mwezi.

Katibu wa Kikundi cha Muungano, Lucy Liukutu (kulia) na Muweka Hazina wa kikundi hicho, Jamila kumbinga (kushoto) wamesema tayari wana shehena ya malighafi za kuzalisha chakula cha kuku, wanachosubiria ni umeme tu. Picha|Rodgers George.

Wadau wa maendeleo na nishati wanena

Wakati wanawake hao wakisubiri Serikali kuwapelekea umeme wa gridi, wanaweza kuangazia matumizi ya nishati mbadala ikiwemo ya biogesi na umemejua ambazo ni safi na salama.

Afisa Programu wa Mtandao wa Jinsia na Nishati Endelevu Tanzania (Tangsen), Thabit Mikidadi anawashauri kuwa wanunue mashine zenye  mifumo miwili itakayowawezesha kutumia umeme wa Tanesco na umeme mbadala ili kuwa na uhakika wa uzalishaji.

“Inaweza kutokea siku wameweka mayai yatotoleshwe halafu umeme ukakatika, watapata hasara,” anasema Mikidadi huku akiwahimiza kuwa na vyanzo mbadala vya nishati. 

Kwa mujibu wa kampuni ya kutengeneza mashine za kutotoresha vifaranga vya kuku ya Tai Incubators Tanzania ya Ubungo Dar es Salaam,, mashine zinazotumia umemejua zinauzwa kuanzia Sh1.4 milioni. 

Mashine hiyo ndogo inayoweza kubeba mayai 120, kwa wakati mmoja ina mfumo unaowezesha kutumia gesi.

“Ukinunua mashine unapata mitungi miwili  ya gesi ya kilogramu 15, paneli za sola na betri na kila kitu. Mashine inakuja ikiwa imekamilika,” anasema Mtoa huduma wa kampuni hiyo, Emmanuel Raphael.

Raphael amesema zipo mashine za mayai 180 kwa Sh1.6 milioni na za mayai 240 zinazouzwa kwa Sh1.8 milioni.

Msajili wa mashirika yasiyo ya kiserikali ambaye pia ni Afisa Maendeleo wa Wilaya ya Mkuranga, Timonty Kudra anasema ikiwa umeme na mashine hizo zitapatikana kwa wakati zitasaidia kuwainua kiuchumi wanawake hao.

“Wakipata umeme inamaanisha uzalishaji utakuwa na hata faida itapanda,” anasema Kudra.

Related Post