Gesi ya majumbani kuagizwa kwa pamoja

April 15, 2019 6:06 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Utaratibu wa kuagiza gesi inayotumika majumbani kwa pamoja utasaidia Taifa kutambua kiwango halisi cha gesi kinachohitajika na kinachoingizwa nchini. Picha|Mtandao.


  • Serikali imesema iko katika hatua za awali za kuandaa mpango wa uagizaji wa gesi ya mitungi (LPG) kwa pamoja kama ilivyo kwa bidhaa za mafuta ili kudhibiti usambazaji na bei elekezi ya gesi hiyo inayotumika majumbani.
  • Itaondoa changamoto ya kila muuzaji amekuwa akjiamulia bei na sehemu anayotaka kupeleka gesi,
  • Itakuwa rahisi kufahamu takwimu halisi za mahitaji na uagizaji wa nishati hiyo.

Dar es Salaam. Serikali imesema iko katika hatua za awali za kuandaa mpango wa uagizaji wa gesi ya mitungi (LPG) kwa pamoja kama ilivyo kwa bidhaa za mafuta ili kudhibiti usambazaji na bei elekezi ya gesi hiyo inayotumika zaidi katika shughuli za nyumbani. 

Kwa sasa kila muuzaji amekuwa akjiamulia bei na sehemu anayotaka kupeleka gesi, hali inayofanya baadhi ya maeneo nchini kukosa kabisa nishati hiyo.

Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani aliyekuwa  akizungumza wakati wa semina kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini iliyofanyika jijini Dodoma, amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha wananchi katika maeneo yote nchini wanafikiwa na huduma hiyo ambapo inaandaa mpango wa kuratibu usambazaji wa gesi hiyo. 

“Serikali ikitangaza bei elekezi kulingana na soko, itawafanya wauzaji wafuate bei hiyo badala ya wao kujipangia, hii itasaidia wananchi kuuziwa gesi kwa gharama inayofanana katika maeneo mbalimbali ambapo gesi hiyo itauzwa,” amesema Dk Kalemani.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Nishati, utaratibu wa kuagiza gesi inayotumika majumbani kwa pamoja utasaidia Taifa kutambua kiwango halisi cha gesi kinachohitajika na kinachoingizwa nchini ambapo itaongeza tija kwa wanawanchi na upatikanaji wa mapato ya Serikali.


Zinazohusiana: 


Awali, akitoa taarifa kwa Wajumbe wa Kamati hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Erasto Simon amesema Wakala huo unafanya tathmini ya namna bora ya kuanza uagizaji wa pamoja wa gesi ya mitungi  kwa kuzingatia maoni kutoka kwa wadau mbalimbali.

Akizungumzia faida mbalimbali zinazotokana na uagizaji wa mafuta wa pamoja, Simon amesema kuwa ni kuweka mazingira sawa ya kibiashara kwani gharama za uagizaji wa mafuta ziko sawa kwa makampuni yote na kuondoa mianya ya rushwa katika uagizaji kwa sababu ufunguzi wa zabuni hufanyika kwa uwazi na washiriki wote huridhika na matokeo ya zabuni.

Pia  Taifa kuwa na uhakika wa usalama wa upatikanaji wa mafuta kwa muda wote na kuwezesha Serikali kuwa na takwimu sahihi za mafuta zinazosaidia katika ukusanyaji wa mapato na kupanga bei elekezi ya mafuta.

Ameabainisha kuwa mfumo wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja umewezesha nchi kudhibiti ubora wa mafuta yanayoingia nchini na pia kuongezeka kwa sehemu za kupokelea mafuta kama bandari ya Tanga na Mtwara, tofauti na ilivyokuwa awali kwani bandari ya Dar es Salaam ndiyo ilikuwa ikitumika kwa shughuli hizo.

Kama utaratibu wa kuagiza mafuta kwa pamoja utatumika pia kwenye gesi utasaidia kuwepo kwa ushindani ulio sawa na ukuaji wa biashara hiyo nchini ambayo inalenga moja kwa moja shughuli za uzalishaji za wananchi katika maeneo yao.

Enable Notifications OK No thanks