Filamu zinavyotumika kuelimisha, kupinga ukeketaji Tanzania
- Filamu hufikisha ujumbe kwa haraka kwa jamii.
- Hutumika pia mashuleni kuwafundishia wanafunzi.
- Wadau wataka ulinzi zaidi kwa wanawake.
Dar es Salaam. Huenda ukawa ni mpenzi wa sanaa zikiwemo filamu na maigizo ambazo mara nyingi hutoa burudani na mafunzo mbalimbali yenye uhalisia katika maisha.
Fahamu kuwa filamu hutumika kutoa elimu ya masuala ya jinsia Tanzania ili kuwafikia watu kwa haraka na urahisi.
Katika siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia nchini Tanzania, Ubalozi wa Ufaransa kwa kushirikiana Shirika la Hope for Girls and Women wameonesha filamu ijulikanayo “In The Name Of Your Daughter” ambayo inasimulia mabinti shupavu waliokimbia kutoka majumbani kwao ili wasikeketweAkizungumza wakati wa mdahalo uliokwenda sambamba na filamu hiyo Disemba 5, 2022 jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women Rhobi Samwelly amesema moja ya mbinu ambazo huzitumia katika kupinga na kuelimisha juu ya ukeketaji ni kuonyesha filamu hiyo sehemu mbalimbali za umma.
“Dhumuni la kuonyesha filamu hii ni kuwasaidia mabinti wa kike ambao wamefanyiwa au wanaotaka kufanyiwa, tunapaza sauti zao ili kupinga kitendo hiki cha ukatili,” amesema Samwelly.
Aidha ameongeza kuwa katika siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia wameamua kuonyesha filamu hiyo ili wadau mbalimbali wajionee mambo yanayotendeka na kuweza kuchukua hatua za haraka kutokomeza kitendo hicho.

Wachangiaji walioshiriki mdahalo uliokwenda sambamba na filamu ya In The Name Of Your Daughter Disemba 5, 2022 jijini Dar es Salaam. Picha | David Mselewa.
Maonyesho ya filamu hupelekwa mpaka mashuleni
Emmanuel Goodluck ambaye ni Afisa Mwelimishaji Jamii katika shirika hilo linalopinga masuala ya ukeketaji amesema wamekuwa pia wakionesha filamu hiyo mashuleni kwa sababu husaidia kufikisha ujumbe kwa haraka kwa wanafunzi ili waweze kujua iwapo wapo kwenye hatari ya kufanyiwa kitendo hicho.
“Huwa tunaonyesha filamu hii mashuleni kwa ajili ya kuwapa elimu wanafunzi hasa mabinti ili waweze kujua iwapo wapo hatarini kufanyiwa ukeketaji na namna gani wanaweza kuepuka wasifanyiwe ukatili huu,” amesema Goodluck.
Mmoja wa wanufaika wa shirika hilo Amina Ramadhani, ambaye kwa sasa amejiunga na masomo ya chuo kikuu amesema yeye ni miongoni mwa mabinti waliokuwa hatarini kukeketwa wakati yupo darasa la saba.
“Nilipata elimu kutoka wa waelimishaji (Hope for Girls and Women) juu ya madhara ya ukeketaji hivyo ikanibidi nikimbie kwenda Nyumba Salama ambapo ni sehemu yenye usalama kwa mabinti wote ambao wapo hatarini kufanyiwa ukeketaji,” amesema Amina wakati wa mdahalo huo.
Soma zaidi
-
Mambo ya kujifunza baada ya mgao wa maji kupungua Dar
-
Tanzania yazidi kujiimarisha mapambano dhidi ya ujangili
Hali ya ukeketaji Tanzania
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), mmoja kati ya wanawake 10 nchini Tanzania (wenye umri wa miaka 15-49) amewahi kufanyiwa ukeketaji.
Kati yao, asilimia 35 wamekeketwa kabla ya kufikia umri wa mwaka mmoja.
Ukeketaji umeenea zaidi katika mikoa ya Manyara, Dodoma na Arusha kwa asilimia 58, asilimia 47 na asilimia 41 kwa takwimu za mwaka 2018 za UNFPA . Ukeketaji umeenea maradufu katika maeneo ya vijijini (asilimia 13) kuliko maeneo ya mijini (asilimia 5).
(UNFPA) inaeleza kuwa ongezeko la idadi ya watu linahatarisha maendeleo na juhudi zilizofikiwa mpaka sasa kwa kuwa idadi halisi ya wasichana walio katika hatari ya kukeketwa inaongezeka.
Tafiti mbalimbali zinaeleza kuwa ukeketaji umejikita kwenye kanuni na taratibu za kijamii, imani za kiutamaduni na vichocheo vya kiuchumi.
Ukeketaji unaonekana kutumika kama njia ya kudhibiti ashki ya kujamiiana kwa wanawake, na katika jamii nyingi, inachukuliwa kama jambo la muhimu katika shughuli za jando na unyago.
Simulizi potofu kuhusu ukeketaji zimekuwa zikirudiwa mara nyingi kiasi cha kusadikiwa kuwa ni kweli nazo huchangia tatizo hilo kuendelea kujihishirishja kwenye jamii.
Madhara ya ukeketaji
Ukeketaji unakwamisha utendaji kazi wa asili wa mwili wa mwanamke na una madhara makubwa kwa afya ya wanawake na wasichana, ikiwa ni pamoja na afya yao kisaikolojia, kimahusiano na afya ya uzazi.
Madhara mengine ni kifo kutokana na kutoka damu nyingi na maumivu makali, uharibifu mkubwa wa mfumo wa nje wa viungo vya uzazi na maambukizi.
Madhara ya muda mrefu yanaweza kuwa maumivu makali, maambukizi ikiwemo maambukizi ya mara kwa mara ya njia ya mkojo na kupungua kwa raha ya kujamiiana.
Madhara ya kisaikolojia, kama vile msongo wa mawazo utokanao na maumivu, kuongezeka kwa hatari za kujifungua kwa njia ya upasuaji na kuongezeka kwa hatari za vifo vya watoto wachanga.
Kongezeka kwa hatari ya watoto kuzaliwa kabla ya muda, kutoka damu nyingi wakati na baada ya kujifungua na watoto kuzaliwa na uzito mdogo (njiti).
Tangazo:

Mkakati wa kitaifa kutokomeza ukeketaji
Mpango wa Taifa wa Utekelezaji wa kukomesha Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (NPA-VAWC) 2017/18- 2021/22) umeeleza kwa ufasaha kwamba ukeketaji ni mila inayoathiri wanawake na watoto.
Tanzania imedhamiria kukomesha kabisa ukatili wa aina zote dhidi ya wanawake na watoto, ikiwemo ukeketaji, kama sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya Maendeleo Endelevu ya 2030.
Mwitikio wa jumla wa sekta mbalimbali ni muhimu katika kukomesha ukeketaji.
“Watendaji katika sekta ya kisheria lazima wafundishwe kuhakikisha kuwa sheria inayozuia ukeketaji inatekelezwa; jamii isisitiziwe kutumia njia mbadala kwenye sherehe za jando na unyango,” imeeleza UNFPA na kusisitiza kuwa
“Programu hizo lazima zizingatie makundi mbalimbali yanayojihusisha na ukeketaji wakiwemo mangariba ambao hupata kipato chao kutokana na shughuli hii na sherehe zinazohusiana na jando na unyago.”
Maeneo salama yanapaswa kuanzishwa kwa ajili ya wasichana waliopo katika hatari na mipango ya sekta ya afya inapaswa kujumuisha mikakati ya kuzuia na kutokomeza ukeketaji.
Latest