Faida, hasara za kupungua kwa wakulima Tanzania

November 6, 2023 2:21 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Wanawake wapungua kwa asilimia 48 na wanaume asilimia 38. 
  • Mabadiliko ya teknolojia, fursa mpya za kiuchumi vyatajwa kama sababu.

Dar es Salaam. Huenda sekta ya kilimo nchini Tanzania ikakabiliwa na upungufu mkubwa wa watu jambo litakaloathiri mwenendo wa sekta hiyo muhimu ikiwemo uzalishaji na upatikanaji wa chakula mara baada ya kuripotiwa kupungua kwa idadi ya watu wanaojishughulisha na kilimo mwaka hadi mwaka.

Ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania ya mwaka 2022  (THDS-MIS) imebainisha kuwa idadi ya wanawake wanaojishughulisha na kilimo imepungua kwa asilimia 48 huku wanaume wakipungua kwa asilimia 39 ndani ya kipindi cha miaka tisa.

Hiyo ni sawa na kusema wanaume na wanawake 4 kati ya 10 waliohojiwa katika utafiti huo waliachana na kilimo na kuhamia katika shughuli nyingine ikiwemo kazi za kitaaluma, mauzo, kazi zenye ujuzi pamoja na kazi za nyumbani.

Ripoti ya utafiti huo iliyotolewa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) inafafanua kuwa, hadi mwaka 2022 ni asilimia 30 ya wanawake na asilimia 32 ya wanaume nchini Tanzania ndiyo wanaojishughulisha na kilimo ukilinganisha na asilimia 78 ya wanawake na asilimia 71 ya wanaume iliyokuwepo mwaka 2004-2005.

Kati ya idadi hiyo ya wakulima, sita kati ya kati ya 10 wanaishi vijijini na wanne  wanaishi mijini, huku miongoni mwao wakikabiliwa na ukosefu wa elimu.

“Wanawake wengi ambao hawana elimu wanafanya kazi katika kilimo asilimia 46, ikilinganishwa na asilimia 14 ya wale walio na elimu ya sekondari au ya juu…

… Wanaume wengi ambao hawana elimu pia wanafanya kazi katika kilimo (asilimia 48), ikilinganishwa na asilimia 17 ya wale walio na elimu ya sekondari au ya juu,” imesema ripoti hiyo.

Hata hivyo, si wote wanaojishughulisha na kilimo wanaweza kupata kipato cha kutosha cha kuendesha maisha yao, ripoti hiyo inaonyesha zaidi ya nusu ya wanawake wanaojishughulisha na kilimo hawalipwi huku wengine wakilima mashamba ya familia.

“Karibu nusu ya wanawake wanaofanya kazi katika kilimo hawalipwi, asilimia 68 wakifanyia kazi mashamba ya familia asu kujiajiri asilimia 17,” imeeelza ripoti hiyo.

Aidha, Ripoti ya  Finscope ya mwaka 2023 inaonesha kuporomoka kwa idadi ya watu wanaojishughulisha na kilimo na uvuvi ambapo miaka kadhaa iliyopita zilikuwa miongoni mwa shughuli zinazotajwa kuchangia upatikanaji wa fedha kwa watu wengi.

“Kumekuwa na mabadiliko katika chanzo cha msingi cha mapato kutoka kilimo na uvuvi kuelekea kazi ya kawaida na utegemezi,” imesema ripoti hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo wakulima na wavuvi nchini Tanzania wamepungua kwa asilimia 13 kutoka asilimia 41 iliyokuwepo mwaka 2017 hadi asilimia 28 mwaka huu.

Wataalamu wa kilimo waeleza sababu

Josephat Masanja, mratibu wa Taasisi ya Africa Youth Pastoralist inayojishughulisha na masuala ya kilimo ameiambia Nukta Habari kuwa, kupungua kwa idadi ya wakulima nchini kunaweza kusababishwa na kuongezeka kwa mabadiliko ya teknolojia pamoja na kupungua kwa ardhi ya kilimo.

“Kadri bunifu za kiteknolojia zinavyongezeka ndivyo matumizi ya ya watu yanavyopungua hususani katika shughuli zinazotumia nguvu kama kilimo..

…Utaona wakulima wengi sasa hivi wananunua trekta inayoweza kulima zaidi ya hekari 200 ndani ya siku mbili ilihali angetumika binadamu ingekuwa ni mamia ya watu,”

Aidha, Masanja amesema mbali na ongezeko la teknolojia, shughuli za kilimo nchini Tanzania zinaathiriwa na ongezeko la watu na shughuli nyingine za kijamii na kiuchumi ikiwemo ujenzi wa viwanda na upanuzi wa miji.

“Tunaambiwa ifiikapo mwaka 2050 huenda tukawa watu milioni 90, kwahiyo uwezo wa ardhi tuliyonayo utazidi kupungua kwa sababu ya makazi na shughuli nyingine za kiuchumi kwa hiyo sekta ya kilimo itakuwa na watu wachache kama nchi nyingine zilizoendelea,” amesema Masanja.


Soma zaidi:Serikali yapanga kutumia Sh47.4 trilioni mwaka wa fedha 2024 – 25


Hata hivyo, Masanja amewataka watanzania kutumia fursa ya kupungua kwa wakulima nchini kuanzisha kilimo cha mashamba makubwa ambacho kitawawezesha kupata faida zaidi na kuliwezesha taifa kuwa na usalama wa chakula.

“Tunahitaji wakulima wakubwa ambao watalima eneo kubwa watazalisha kwa ajili ya watu wengine…ni namna gani tunaweza kuwapata wakulima wakubwa ni kuwapa mitaji, pamoja na teknolojia ya kutosha,” ameongeza Masanja.

Kwa upande wake mtaalamu wa kilimo (Agronomist) ambaye hakutaka jina lake litajwe ameiambia Nukta Habari kuwa utafiti huo umejikita zaidi katika kuangazia kilimo kama shughuli ya kiuchumi na siyo kama sekta ya kiuchumi.

Mtaalamu huyo amenukuu sensa ya mwisho ya kilimo iliyofanyika mwaka 2019/2020 inayoonesha kuongezeka kwa idadi ya kaya zinazojishughulisha na kilimo pekee kwa asilimia 45.4.

Mwaka 2007/08 sensa hiyo ilionesha kulikuwa na kaya milioni 3.5 zinazojishughulisha na kilimo pekee ambazo  ziliongezeka hadi kufikia milioni 5.1 mwaka 2019/20.

Kwa mujibu wa takimu hizo idadi ya kaya zinazojishughulisha na kilimo zinaongezeka kinyume na utafiti wa THDS-MIS unaoonesha kupungua kwa idadi ya wakulima kwa asilimia 39 kwa wanawake na asilimia 40 kwa wanaume mwaka 2022.


Zinazohusiana:Tanzania kutumia teknolojia kuwavuta vijana kwenye kilimo


Wasomi waongezeka

Wakati idadi ya wakulima nchini ikiporomoka, idadi ya wasomi inaongezeka kwa kasi huku jambo linalohisiwa kuchangia kupunguza idadi ya wakulima nchini.

Ripoti hiyo inaweka wazi kuwa asilimia 80 ya wanawake na asilimia 87 ya wanaume ni wasomi wenye kazi mbalimbali za taaluma au zenye ujuzi.

Hata hivyo, bado sekta ya kilimo nchini Tanzania inaendelea kuwa miongoni mwa mihimili muhimu ya maendeleo ya nchi.

Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo mwaka 2022 sekta ya kilimo ilichangia asilimia 26.1 katika pato la taifa, kutoa ajira kwa wananchi kwa wastani wa asilimia 65.6 na kuchangia asilimia 65 ya malighafi za viwanda.

Enable Notifications OK No thanks