Serikali yapanga kutumia Sh47.4 trilioni mwaka wa fedha 2024 – 25

November 6, 2023 9:13 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni ongezeko la Sh3.1 trilioni kutoka ile ya 2023/24.
  • Zaidi ya nusu ya bajeti kutumika kwenye matumizi ya kawaida.


Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania inakusudia kukusanya na kutumia jumla ya Sh47.4 trilioni katika mwaka wa fedha 2024/25 ikiwa ni ongezeko la Sh3.1 trilioni kutoka bajeti ya sasa ambayo ukomo wake unaishia Juni mwaka ujao. 

Ikiwa bajeti hiyo itapitishwa mwakani basi, itakuwa imeongezeka kwa asilimia sita ikilinganisha na ya sasa ya 2023/24.

Mwaka 2023/24 Serikali ilipitisha kukusanya na kutumia Sh44.4 trilioni ambapo mapato ya ndani ni Sh31.4 trilioni huku kiasi kilichobaki kikitarajiwa kutoka kwenye mikopo nafuu, mikopo ya kibiashara na misaada ya wahisani.

Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba aliyekuwa akiwasilisha bungeni mpango wa bajeti wa mwaka 2024/25 leo Oktoba 11, 2023 amewaambia Wabunge kuwa kati ya fedha hizo Sh34.43 ni mapato ya ndani.

“Mapato ya ndani yanakadiriwa kuwa Sh34.43 sawa na asilimia 72 ya bajeti yote, aidha washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh4.29 sawa na asilimia 9 ya bajeti na Serikali inatarajia kukopa Sh6.14 kutoka soko la ndani na Sh2.55 kutoka soko la nje,” amesema Dk Nchemba jijini Dodoma.


Mwigulu ameongeza kuwa maoteo ya bajetiya 2024/25 yamezingatia mwenendo wa ukusanyaji wa mapato, matarajio ya ukuaji wa uchumi, hali ya uchumi wa dunia pamoja na mikakati ya Serikali ya kuongeza mapato ya ndani.

Zaidi ya nusu ya bajeti kutumika kwa matumizi ya kawaida

Kama bajeti nyingine zilizopita, huenda zaidi ya nusu ya bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/25 ikatumika kwenye matumizi ya kawaida ikiwemo kulipa deni la Serikali pamoja na mishahara.

Kwa mujibu wa Mwigulu, Sh12.1 trilioni zitatumika kwa ajili ya kugharamia deni la Serikali, Sh11.77 trilioni kulipa mishahara ya wafanyakazi, Sh8.22 trilioni kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za Serikali ambapo programu za maendeleo zinatarajiwa kutumia Sh15.32 trilioni.

“Makadirio haya yamezingatia mahitaji ya kugharamia deni la Serikali, mishahara ya watumishi wa umma, uendeshaji wa miradi iliyokamilika, ugharamiaji wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa na maandalizi ya uchaguzi kwa mwaka 2025,” ameongeza Nchemba.

Enable Notifications OK No thanks