Tanzania kutumia teknolojia kuwavuta vijana kwenye kilimo

Husna Miraj 1124Hrs   Septemba 07, 2023 Teknolojia
  • Ni kupitia kuwekeza kwenye tafiti na kutoa vifaa vya kisasa.
  • Rais Samia asema itabadili fikra za vijana kuwa kilimo ni kazi ngumu.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania inatarajia kutumia teknolojia kuongeza idadi ya vijana wanaojihusisha na shughuli za kilimo ili kuchochea uzalishaji wa mazao na kupunguza wimbi la ukosefu wa ajira kwa vijana.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), mwaka 2021 asilimia 9 ya vijana nchini Tanzania hawakuwa na ajira huku ikikadiriwa idadi hiyo inaweza kuongezeka na kufikia asilimia 9.4 mwaka 2023.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliyekuwa akishiriki mkutano wa Jukwaa la Mfumo wa Chakula Afrika (AGRF) leo Septemba 7, 2023, amewaambia washiriki kuwa matumizi ya sayansi na teknolojia ya kisasa yatasaidia kubadili fikra za vijana wa Kitanzania kuwa kilimo ni kazi ngumu.

“Tumewekeza kwenye tafiti, katika maeneo yote, kilimo, ufugaji na uvuvi, kwa kutumia teknolojia tunaendele kufanya usajili wa wakulima, aina ya kilimo wanachofanya, eneo alilonalo na mambo mengine yanayomhusu mkulima,” amesema Rais Samia jijini Dar es Salaam.

Rais Samia ameongeza kuwa, ili kuhakikisha matumizi ya mbolea sahihi na mbegu sahihi, Serikali imewawezesha maafisa ugani nchi nzima kuwa na vifaa vya kupima udongo ili kuepusha gharama zinazotokana na matumizi ya pembejeo zisizo sahihi na kuongeza uzalishaji wa mazao.

Kwa mujibu wa Rais Samia kupitia teknolojia Serikali inaendelea kuhakikisha uzalishaji wa mbegu za kisasa unafanyika nchini ili kupunguza gharama za kuagiza kutoka nje hatua ambayo itafanikisha upatikanaji wa mbegu hizo kwa wakulima kwa bei nafuu.

“Tunategemea mpaka 2025 robo tatu ya mbegu zinazotumika zizalishwe hapa nchini, na ni mbegu ambazo zimethibitishwa, zinazohimili mabadiliko ya hali ya hewa na hali ya udongo,” ameongeza Rais Samia.

Takwimu za Wizara ya Kilimo zinaonesha kuwa mwaka 2022  Tanzania ilitumia jumla ya tani 64,152 za mbegu bora za mazao mbalimbali ikiwemo za mazao ya chakula na biashara ambapo tani 44,344 zilizalishwa nchini.


Maeneo mengine yatakayotumia teknolojia na kuwavuta vijana katika kilimo ni katika utunzaji wa mazao za umwagiliaji ambako Serikali imepanga kufunga mifumo ya kisasa itakayoendana na zao husika pamoja na kiwango cha maji hitajika.

Itakumbukwa kuwa Serikali imekusudia kuendeleza  miradi 69 ya umwagiliaji kwenye eneo lenye ukubwa wa hekta 95,005 ili kuongeza mtandao  wa umwagiliaji kutoka hekta 727,280 mwaka 2022 hadi kufikia hekta 822,285 mwaka 2023.



Related Post