Uzalishaji wa chakula cha samaki bado bado Tanzania

December 4, 2024 11:41 am · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Wafugaji wa samaki wanategemea kiasi kikubwa cha chakula kutoka nje ya nchi licha ya mahitaji kuongezeka kuongezeka.
  • Wengine wataja ukosefu kama sababu inayochangia sekta hiyo isikue.

Dar es Salaam. Alipokuwa anaingia katika biashara ya uzalishaji wa vifaranga vya samaki alikuwa na mategemeo ya kuwa mfanyabiashara mkubwa wa bidhaa hiyo ndani ya muda mfupi.

Jambo ambalo hakufahamu ni kuwa katika biashara kuna changamoto ambazo zinaweza kuchelewesha mafanikio yako. 

Huyu ni mmiliki wa kampuni ya uzalishaji wa vifaranga vya samaki aina ya Tilapia (Sato) ya Aquaeco Hatcheries, Mbonea Mdoe ambaye anasema upatikanaji wa chakula cha samaki kwa wakati ni changamoto kubwa inayoendelea kumkabili. 

“Ni upatikanaji ndani ya muda, unaweza ukawa unahitaji chakula fulani ukaambiwa kila wakala hana, kuna wakati inaweza kukuchukua mpaka mwezi kukipata tena hususan kwetu ambao tunazalisha vifaranga, inatulazimu wakati mwingine kutengeneza wenyewe japo ni changamoto kwa sababu hatuna viungo vinavyotakiwa na fomula sahihi,” anasema Mdoe. 

Changamoto inayompata Mdoe inafanana na wazalishaji wengine wa vifaranga vya samaki ambao wamewekeza fedha zao katika biashara hiyo lakini wana safari ndefu ambayo isipotatuliwa kwa wakati inaweza kuchelewesha mafanikio yao na Taifa. 

Kutokana na ongezeko la mahitaji ya chakula cha samaki, wafugaji na wazalishaji wa vifaranga vya samaki hulazimika kuagiza nje ya nchi. 

Mdoe ambaye anafanyia shughuli zake mkoani Mwanza anadai vyakula vya ndani bei yake iko chini ukilinganisha na wanavyoagiza nje ya nchini lakini wazalishaji wa ndani hawajawekeza katika  tafiti za kutoa bidhaa zinazoaminika kushindana na vyakula vya nje.

“Mimi nimejaribu chakula kinachotengezwa nchini na kinachoingizwa kwa sababu nazalisha mbegu kwa ajili ya wafugaji wengine hivyo nazingatia ubora, vinavyoingizwa vinafanya vizuri zaidi,” anasema mdau huyo wa sekta ya uvuvi Tanzania. 

Hali halisi ya upatikanaji wa vyakula vya samaki

Kitabu Cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2023 kilichotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), inaeleza kuwa mwaka 2023,  tani 4,337.9 za chakula cha samaki zilitumika nchini Tanzania ikilinganishwa na tani 2,156.1 za 2022

Kati ya tani hizo, 4,337.9 zilizotumika mwaka jana, tani 3,012.7 ambazo ni takribani robo tatu au asilimia 70 ziliagizwa kutoka nje ya nchi.

Hali hii inayoonesha utegemezi mkubwa wa chakula cha samaki kutoka masoko ya kimataifa licha ya kuwa kuna uwezekano wa chakula hicho kuzalishwa nchini. 

Kwa mujibu wa kitabu hicho, ongezeko la mahitaji ya chakula cha samaki linachangiwa na kuongezeka kwa uzalishaji wa vifaranga vya samaki.

Mathalani, mwaka 2023 vifaranga vya samaki 35,967,180 vilizalishwa sawa na ongezeko la asilimia 22.8 ikilinganishwa na mwaka 2022.

Mfugaji wa samaki akiwarushia chakula samaki aina ya sato kwenye bwawa. Picha | FAO.

Mitaji ni changamoto

Meneja Masoko na Mauzo kutoka kampuni ya utengenezaji wa vyakula vya samaki ya NovFeed, Miraji Joseph, anasema changamoto kubwa inayowakabili wazalishaji wa ndani wa vifaranga vya samaki na kusababisha uzalishaji kuendelea kuwa mdogo ukilinganisha na mahitaji ya soko ni kukosa mitaji na teknolojia ndogo.

“Gharama za uwekezaji ni kubwa kufungua kiwanda ambacho kinazalisha tani nyingi zaidi, ukiangalia mashine nyingi ambazo tunazo hapa Bongo (Tanzania) ni za gharama ya chini, lakini zinazouzwa nje bei ni ghali. Sisi Watanzania inakua ngumu kuzitumia kwa sababu ndiyo tunaanza tunatumia mashine hizi za kawaida, jambo kubwa hapa ni pesa”

Miraji ameongoza kuwa wateja kutokuwa na imani na bidhaa zinazozalishwa nchini ni changamoto inayowakabili wanapofikiria kuongeza uzalishaji wa chakula cha samaki.

“Jambo kubwa linalofanya tujifikirie mara mbili ni namna wafugaji wanavyoonesha wasiwasi wao, wengi bado wanaile fikra kwamba chakula kinachotoka nje ya nchi ni bora zaidi, mteja anaweza akakupigia simu akakuuliza chakula chenu kinatoka nchi gani, ukimwambia ni Tanzania anaingia mitini,” ameongeza Miraji.

Kwa mujibu wa ripoti ya Fursa za Uwekezaji katika Sekta Ndogo ya Uvuvi na Ufugaji wa Samaki, Tanzania ya mwaka 2019 iliyotolewa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Serikali inasaidia usambazaji wa chakula cha samaki kwa bei nafuu kwa kutoa ruzuku ya asilimia 85 ya bei ya kuuza kwa wafugaji wa samaki. 

Viwanda vidogo vya kusaga chakula cha samaki vinatumia malighafi zinazopatikana ndani ya nchi kama vile unga wa dagaa, soya, mafuta ya alizeti, unga wa mhogo, pumba za ngano na mahindi. 

Mdoe ambae ameishauri Serikali kuboresha mazingira yatakayovutia uwekezaji wakubwa wa kuzalisha chakula kwasababu tayari umefanyika kwa ufugaji kama misamaha ya kodi za mashine na pembejeo zinazohitajika. Pia kuwasaidia wazalishaji wa ndani wanaojitokeza kupata mitaji katika benki za uwekezaji sambamba na kufanya tafiti.

Kwa Mujibu wa bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya 2024/25, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kutoa vibali 44 vya kuingiza chakula cha samaki kutoka nje ya nchi kwa kampuni 15.

Pia imezipa kampuni hizo misamaha ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT) na ushuru wa forodha kama moja ya juhudi za kukabiliana na changamoto ya hali duni ya uzalishaji wa chakula cha samaki.

Enable Notifications OK No thanks