Fahamu faida za kusafisha ‘AC’ mara kwa mara
- Kutakuepusha na magonjwa ya mfumo wa hewa pamoja na kufanya AC yako idumu zaidi
- Inashauriwa kusafisha kila baada ya miezi mitatu au mitano
Dar es Salaam. Kiyoyozi au ‘AC’ (Air Conditioner) kama wengi wanavyopenda kukiita ni kifaa cha kisasa kinachotumia umeme kupooza hewa, na mara nyingi hutumika maeneo yenye joto.
Kwa mikoa kama Dar es Salaam kifaa hicho huwawezesha watumiaji kupata hewa ya baridi licha ya jua kali na joto linalokuwepo hususan nyakati za mchana na wakati mwingine usiku.
Licha ya faida hizo, watu wengi hupuuza umuhimu wa kusafisha kifaa hicho hali inayopelekea vifaa hivyo kuharibika na kusababisha matatizo ya afya.
Kwa mujibu wa tovuti ya Alfold Mechanical AC isiyosafishwa mara kwa mara inaweza kusababisha magonjwa ya mfumo wa hewa, magonjwa ya ngozi na mzio unaoweza kuhatarisha afya za watumiaji.
Ili kuepukana na madhara hayo ni lazima kusafisha AC mara kwa mara
Ibrahim Mwela, fundi viyoyozi jijini Dar es Salaam ameiambia Nukta Habari kuwa kifaa hicho kinatakiwa kusafishwa kila baada ya miezi mitatu kwa watumiaji waliopo maeneo yenye vumbi au moshi kwa wingi.
“Baadhi ya dalili zinazoonesha AC kuwa chafu ni kama kupungua kwa kiwango cha ubaridi uliozoeleka na pia kifaa hicho kutoa kiasi kikubwa cha maji isivyo kawaida,” amesema Mwela.
Aidha Mwela amefafanua kuwa kwa watumiaji waliopo maeneo tulivu yasiyo na vumbi wanatakiwa kusafisha AC kila baada ya miezi mitano.

Baadhi ya dalili kuwa AC yako imejaa uchafu ni pamoja na kutoa maji mengi kuliko kawaida na kupungua kwa kiwango cha ubaridi uliozoeleka.PichalClimate Care
Huboresha ufanisi
Kwa mujibu wa Idara ya Nishati ya Marekani, moja ya faida ya kusafisha kiyoyozi ni kuepusha kuziba kwa vichungi vya hewa yaani ‘air filters’ kunakozuia mzunguko wa kawaida wa hewa kwa sababu ya uchafu na kusababisha ‘AC’ kufanya kazi kubwa zaidi kuliko inavyopaswa.
Hali hii husababisha kupungua kwa ufanisi na kuongeza matumizi ya nishati hivyo kupaa kwa bili za umeme.
Hivyo wataalamu kutoka Idara ya Nishati ya Marekani wanashauri kubadilisha kichujio kichafu au kilichoziba na kuweka kisafi kunaweza kupunguza matumizi ya nishati ya ziada kwa asilimia 5 hadi 15 ya kiyoyozi chako.
Soma zaidi
-
Upungufu wa walimu shule za msingi unavyoathiri elimu Tanzania
-
Veronica Sarungi: TO anayeishi ndoto, taaluma ya ualimu
-
Miongozo mipya elimu maalum kuongeza ujumuishi Tanzania
Kudumu kwa kiyoyozi
Usafishaji wa mara kwa mara husaidia kuongeza muda unaoweza kuendelea kutumia kiyoyozi chako.
Ni muhimu kuelewa kuwa uchafu na vumbi vinaweza kujikusanya kwenye koili za kuchuja na kupoozea hewa na hali hii hupunguza mzunguko wa hewa na kudhoofisha uwezo wa koili hizo kufyonza joto ipasavyo.
Licha ya kukiongezea kiyoyozi mzigo mkubwa wa kufanya kazi ya ziada, uchafu husababisha kuongezeka kwa kasi ya uchakavu wa vifaa vilivyomo ndani ya kiyoyozi.
Kwa mujibu wa Mwela kutosafisha AC kwa wakati inaweza kusababisha ongezeko la gharama za matengezo ikiwemo kupungua kwa gesi zinazotumika ndani ya kifaa hicho yaani CFCs.
“Ikiziba ‘evaporator’ huduma haitofanyika kifaa kilipofungwa, inabidi kishushwe, na utakapo ‘pump’ lazima gesi nyingine itamwagika inamaana itataka ‘service’ kubwa ambayo tunaita kuflashi,” amesema fundi Mwela.
Mwela amebainisha kuwa wakati wa kusafisha AC ni muhimu kuzingatia sakiti au mota ya feni haiingii maji aidha kwa kuifunika na karatasi au kuifungua.

Kusafisha kiyoyozi mara kwa mara kutakuepusha na magonjwa ya mfumo wa hewa kama mafua na nimonia.PichalEsau Ng’umbi/Nukta
Ubora wa hewa
Kulingana na Wakala wa Usalama wa Mazingira Marekani (EPA) viwango vya uchafuzi wa hewa ya ndani vinaweza kuwa mara mbili au tano zaidi ya viwango vya nje kutokana na vumbi, moshi wa sigara, ukungu, na mba kutoka kwa wanyama.
kusafisha kiyoyozi mara kwa mara unaweza kusaidia kuhakikisha kuwa hewa inayozunguka nyumbani kwako ni safi na imechunjwa vizuri iwezekanavyo.
Kuepuka gharama kubwa za marekebisho
Kiyoyozi kinapofanya kazi katika hali ya uchafu kwa muda mrefu, hatimaye kinaweza kukumbwa na hitilafu kubwa au hata kushindwa kabisa kufanya kazi.
Kwa mujibu wa Voltora Industries kifaa kinapokusanya vumbi na uchafu kwa kiasi kikubwa inakuwa vigumu zaidi kukisafisha na kuongeza gharama kubwa za shughuli hiyo au hata hitaji la vifaa vipya.
Kupunguza uwezekano wa magonjwa
Kwa mujibu wa Sanitair, kampuni ya usafishaji viyoyozi na mazingira ya australia, mfumo wa viyoyozi unaweza kuwa eneo la kuzaliana kwa bakteria na vimelea vingine vya hatari ambavyo vinaweza kusababisha matatizo katika mfumo wa upumuaji wa binadamu.
Dk.Kelvin Lotti kutoka Zahanati ya Arafa iliyopo Tabata jijini Dar es Salaam, amebainisha kuwa kutokusafisha AC mara kwa mara kunaweza kusababisha magonjwa ya njia ya hewa yakiwemo pumu, nimonia, mafua na kushindwa kupumua vizuri.
“Magonjwa unayoweza kupata ni yale yanayohusiana na mfumo wa upumuaji, kama pumu na mafua kutokana na mzio wa vumbi, au nimonia kutokana na kuvuta pumzi iliyochanganyika na vumbi ambayo huathiri mapafu,” amesema Dk Kelvin.
Aidha, Dk. Kelvin amewatahadharisha watu wenye mzio na hewa itokanayo na AC hususani wenye historia ya pumu au mafua ya mara kutotumia AC mara kwa mara kwani inaweza kuwasababishia athari za kiafya.
Latest