Unavyoweza kuzalisha pesa Facebook kupitia maudhui Tanzania
- Ni kupitia matangazo yanayowekwa kwenye maudhui, zawadi za watazamaji na usajili maalumu.
- Ubora wa maudhui unaweza kuongeza watazamaji na mapato.
- Waandaji wanashauriwa kuwa na njia mbadala za kuingiza pesa.
Dar es Salaam. Hivi karibuni kampuni ya Meta ilitangaza kuwa itaanza kuwalipa wazalishaji wa maudhui ya mtandaoni waliopo nchini Tanzania hatua inayotarajia kutoa ahueni ya kiuchumi kwa kuwa itatumika kama chanzo kipya cha mapato.
Meta, kampuni kubwa ya teknolojia nchini Marekani, ina miliki mitandao ya Facebook, Instagram na WhatsApp yenye wafuasi wengi duniani inaungana na kampuni kama YouTube na X zamani Twitter ambao walishaanza utaratibu wa kuwalipa wazalisha maudhui wake.
Ili kuongeza uelewa wa namna ya kujiingizia kipato kupitia uzalishaji wa maudhui kwenye mitandao hiyo Meta kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) na wadau wengine wa kidijiti wamebainisha mbinu zinazoweza kutumika ili kupata pesa katika mtandao wa Facebook.
Kwa mujibu wa Desmond Mushi, Meneja wa Sera Meta, muandaaji wa maudhui halipwi kwa kua mtandaoni pekee bali ni kwa namna ambavyo maudhui yake yatakuwa yakitumika kwa njia tofauti zaidi ya nne ikiwemo matangazo kwenye maudhui, ushirika wa kibiashara, kupata zawadi kwa wafuasi pamoja na malipo ya kila mwezi kutoka kwa wafuasi.
Njia ya matangazo kwenye video
Meta huingiza matangazo kwenye maudhui yaliyochapishwa kwenye ukurasa wa Facebook ambayo huonwa na watazamaji wa maudhui husika.
Kupitia matangazo yanayofahamika kama ‘In-Stream Ads’ muandaaji atapata sehemu ya faida ambayo Meta wameizalisha kutokana na tangazo hilo.
Ufanisi wa mapato kupitia njia hii hutegemea zaidi ubora wa maudhui ya video yaliyoandaliwa ili kuvutia watazamaji wengi zaidi ambapo kadri tangazo linavyotizamwa na watu wengi zaidi ndivyo ambavyo mtengenezaji wa maudhui hulipwa zaidi.
Edmund Mushi, meneja wa sera za Meta akieleza njia zinazotumika na watengezeza kuingiza pesa kwenye kongamano lililofanyika ukumbi wa maktaba mpya UDSM, Agosti 15, 2024| picha na Davis Matambo
Zawadi za watazamaji (‘Token’)
Aidha, njia ya pili ya kupata pesa iliyobainishwa na Meta ni kupitia watazamaji kununua zawadi (Token) na kumpa muandaaji wa maudhui ambaye yeye atazigeuza kuwa pesa.
Ili kupata zawadi, muandaaji atatakiwa kwanza kuruhusu kipengele cha kupokea fedha katika akaunti yake na kuruhusu kupokea token kutoka kwa watazamaji wake.
Njia hii ni kwa maudhui ya mbashara peke yake (live streaming) na hutegemea zaidi uhusiano kati ya muandaaji na watazamaji wake, kadri anavyowashirikisha na kuwapa maudhui bora ndivyo watakavyokuwa tayari kumpa zawadi.
Kutangaza bidhaa au huduma
Hii ni njia iliyozoeleka na wengi, muandaaji wa maudhui hutumia ukurasa wake wa Facebook kutangaza bidhaa au huduma zake mwenyewe, au za watu wengine kama wakala.
Ili kufanikiwa kupitia njia hii, muandaji wa maudhui anapaswa kuchagua bidhaa au huduma inayopendelewa au kuhitajika na hadhira yake na kuiwasilisha kwa namna inayovutia.
Kupitia usajili wa maudhui maalumu (‘Premium Subscriptions’)
Njia nyingine ambayo muandaaji wa maudhui anaweza kuitumia kupata kipato ni kuandaa maudhui maalumu ambayo wafuasi watakaojisajili kupata maudhui hayo watalazimika kulipia kwanza.
Kupitia njia hii wafuasi wa muandaa maudhui humpa ada ya kila mwezi ili kupata maudhui kipekee, kama vile video za nyuma ya pazia (behind the scene), mafunzo, au mazungumzo ya moja kwa moja.
Ili kupata wafuasi watakao jisajili kupata maudhui hayo muandaaji anapaswa kuhakikisha maudhui yake ni ya pekee kustahili ada wanayolipa wafuasi wake.
Ushirikiano wa kurasa ‘partnership’
Njia hii huhusisha makubaliano binafsi kati ya mzalisha maudhui na kampuni inayotaka kuweka matangazo ya bidhaa au huduma kwenye ukurasa wake, au kua anasambaza maudhui ambayo yamebainishwa kulipiwa na kampuni husika.
Jinsi ya kuandaa maudhui bora
Kwa mujibu wa Mushi waandaa maudhui mara zote wanapaswa kuzingatia ubora wa maudhui yao, kuhakikisha yanawavutia watazamaji wengi.
“Chapisha maudhui mara kwa mara ili kuwafanya wafuasi waendelee kukufatilia…jenga uhusiano mzuri na watazamaji wako, wajibu maoni yao na chat nao…hakikisha unafuata sheria na miongozo yote ya Meta ili kuepuka akaunti yako kuzuiliwa”, ameongeza Mushi.
Waandaa maudhui wanapaswa kubaki kwenye uhalisia wao kama kutumia sauti zao bila ya kuwaiga wengine, kuepuka uzalishaji wa maudhui yatayo gharimu mtazamaji megabaiti nyingi na kusambaza maudhui kwenye muda sahihi.
Kwa upande wake wa Nuzulack Dausen, Mtendaji Mkuu wa Nukta Africa, watengeneza maudhui wanatakiwa kujali lengo la maudhui yao, kuchagua aina ya maudhui, kuthibitisha taarifa wanazopokea, kulinda taswira zao na kuzingatia sheria na taratibu za nchi.
Dausen amebainisha kuwa, mafanikio katika ulimwengu wa digiti yanahitaji uvumilivu, ubunifu, na kujitolea na sio kutarajia mafanikio ya haraka.
Nuzulack Dausen, CEO wa Nukta Africa akitoa ushauri kwa watengeneza maudhui kwenye ukumbi wa maktaba mpya UDSM, Agosti 15, 2024| picha na Davis Matambo
“Kuna dhana kwamba ukifungua akaunti ya mtandao wa kijamii, unatoboa upesi, mimi nina miaka 15 kwenye media…naweza nikakwambia sio rahisi hivyo tunavyofikiria…Kama mimi nimechagua uzalishaji maudhui ndio sehemu ya maisha, ni vizuri kuangalia mbinu zaidi ya moja ya kuingiza fedha,” amesema Dausen.
Njia tofauti kwa watengeneza maudhui kuingiza pesa kupitia mtandao wa Facebook zimebainishwa kwenye kongamano lililoandaliwa pamoja kati ya Meta na UNESCO ili kuwaelimisha juu ya fursa na ujuzi wa kidijiti lililofanyika Agosti 15, 2024 kwenye ukumbi wa maktaba mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Pamoja na njia hizo muandaaji wa maudhui anatakiwa kusoma na kuelewa sera za malipo za Meta ili kuelewa vigezo na masharti vinavyotakiwa kuzingatiwa.
Hata hivyo, mbali na Meta na baadhi ya mitandao kuanza kulipa, miongoni mwa changamoto kuu imekuwa ni kupata mfumo rafiki wa kuweza kutoa fedha hizo kwa kuwa kampuni nyingi zinatumia huduma ya PayPal na nyingine ambazo si rahisi kutoa fedha taslimu ukiwa Tanzania.