Erick Kabendera aieleza mahakama alivyofanyiwa vipimo vya X-Ray, damu
- Mwandishi huyo wa habari za uchunguzi, amesema kwa mara ya kwanza jana alifikishwa katika hospitali ya Rufaa ya Amana na kufanyiwa kipimo vya X-Ray kwenye mgongo na vipimo vya damu.
- Majibu ya kipimo cha X-Ray yametoka, anasubiri ya vipimo vya damu.
- Kesi yake imeahirishwa hadi Oktoba 1, 2019 itakapotajwa tena.
Dar es Salaam. Mwandishi wa habari za uchunguzi, Erick Kabendera ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkaazi Kisutu kuwa kwa mara ya kwanza jana alifikishwa katika hospitali ya Rufaa ya Amana na kufanyiwa kipimo vya X-Ray kwenye mgongo na vipimo vya damu.
Kabendera ambaye anaandikia vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi alifikishwa mahakamani Agosti 5, 2019 akikabiliwa na mashtaka matatu ya kuongoza genge la uhalifu, kukwepa kodi na utakatishaji fedha kiasi cha Sh173.24 milioni.
Akizungumza leo (Septemba 18, 2019) mbele ya Hakimu Mkaazi Mwandamizi, Agustine Rwezile, Kabendera amesema anaendelea kusubiri majibu ya vipimo vya damu yatoke ili aanze kupata matibabu, licha kuwa bado anajisikia maumivu makali kwenye mgongo na mguu wake.
“Jana nilipelekwa hospitali ya Amana na nikapimwa X-ray na vipimo vya awali vimeonyesha kuwa nina matatizo ya mgongo. Wamechukua vipimo vingine ambavyo vinaweza kuwa tayari mwishoni mwa wiki, lakini bado napata maumivu makali ya mgongo,” amesema Kabendera.
Soma zaidi:
- Polisi Tanznaia yakiri kumshikilia Mwanahabari Kabendera
- Uhamiaji waeleza sababu za kuendelea kumshikilia Mwanahabari Kabendera
- Mwanahabari Erick Kabendera ashtakiwa kwa utakatishaji fedha, uhujumu uchumi
Wakili wa upande wa utetezi, Jebra Kambole ameiomba mahakama hiyo kuahirishwa kesi hiyo hadi pale watakapokuja kuieleza kuhusu majibu ya vipimo vya damu.
Kutokana na maelezo hayo, Hakimu Mkaazi Mwandamizi, Rwezile ameahirisha shauri hilo hadi Oktoba 1, 2019 ambapo litakapotajwa tena.
Naye Wakili Mwandamizi wa Serikali, Wankyo Saimon amesema shauri lililetwa mahakamni hapo kwa ajili ya kutajwa kwa sababu upepelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika lakini uko katika hatua nzuri.
Kabendera alichukuliwa kwa nguvu nyumbani kwake Mbweni Jijini Dar es Salaam Julai 29, 2019 na watu waliojitambulisha kuwa ni polisi na wakati wote alikuwa akishikiliwa na polisi kabla ya kupandishwa kizimbani Agosti 5 mwaka huu.