Jeshi la Polisi: Hali ya usalama ni shwari Tanzania

December 10, 2025 1:38 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Lawataka wananchi kuzingatia sheria na maelekezo ya vyombo vya ulinzi na usalama. 

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Tanzania limesema hali ya usalama nchini imeendelea kuwa shwari, kufuatia hatua mbalimbali zilizochukuliwa usiku wa kuamkia leo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.

Taarifa ya Msemaji wa Jeshi la Polisi DCP David Misime, iliyotolewa leo Disemba 10, 2025 inasema jeshi hilo lilifanya operesheni ya kuimarisha usalama usiku wa kuamkia leo iliyobainisha kuwa nchi ipo salama.

“Kama tulivyowapa taarifa iliyokuwa na ahadi ndani yake majira ya saa 6 usiku Desemba 9, 2025 kuamkia leo Desemba 10, 2025 kuwa, kwa ushirikiano na vyombo vingine vya ulinzi na usalama tutaendelea kuimarisha hali ya usalama nchini na kwamba tutaendelea kulinda maisha ya wananchi na mali zao,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ya Jeshi la Polisi inakuja ikiwa ni siku moja tangu kuitishwa kwa maandamano yasiyo na kikomo yaliyopangwa kuanza jana Disemba 9, mwaka huu.

Maandamano hayo ya amani yaliyohamasishwa kwa zaidi ya wiki tatu kupitia mitandao ya kijamii yanalenga kupinga mwenendo wa Uchaguzi Mkuu wa 2025 na kushinikiza uwajibikaji baada ya vurugu zilizoibuka wakati wa maandamano yaliyofanyika Oktoba 29 na siku zilizofuatia.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi kuanzia Disemba 5 mwaka huu lilitangaza kuyazuia maandamano hayo likiimarisha ulinzi katika mikoa mbalimbali ikiwemo jiji la Dar es Salaam suala lililofanya maandamano hayo kushindwa kufanyika.

Pamoja na kushindikana huko, tayari polisi waliripoti kuwashikilia watuhumiwa kadhaa kwa kuhamasisha maandamano hayo huku likiahidi kuwadhibiti wanaoendelea kuyachochea.

“Kama kuna ambaye atajitokeza na kukaidi kutii sheria za nchi kwa lengo la kuhatarisha usalama wa nchi ili kusimamisha shughuli za kiuchumi na kijamii zisiendelee kama wanavyo hamasishana na kudanganyana tutawadhibiti ili nchi ibaki salama na Watanzania wema na wapenda amani wabaki salama,” imeeleza taarifa hiyo.

Aidha, Jeshi la Polisi limewahakikishia wananchi kuwa litaendelea kulinda usalama wa taifa, maisha ya watu na mali zao ili kuruhusu shughuli za kila siku kuendelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks